Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hassan Elias Masala
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Kwa muda mrefu kumekuwa na zoezi la utafiti katika Kata ya Nditi, Wilayani Nachingwea linalofanywa na kampuni tofauti:- (a) Je, nini hatma ya utafiti huo wa muda mrefu ambao unaleta mashaka kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo? (b) Je, wananchi wa maeneo jirani wanaweza kuruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji mdogo ili waweze kunufaika badala ya kuwa walinzi na vibarua? (c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta watafiti zaidi katika maeneo mengine ya Wilaya hizo kama Kiegei, Marambo, Nditi na kadhalika?
Supplementary Question 1
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru kwa majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini sambamba na hilo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kampuni ambayo ameitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa muda huo wa miaka nane ambao wamekuwa wanafanya utafiti, wamekuwa wanatumia mashine, wamekuwa wanatumia magari ambayo yamekuwa yanaharibu barabara zinazounganisha, Nditi, Nero, Namakwia pamoja na Lionja.
Je, Mheshimiwa Waziri ananiambia nini kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea juu ya fidia ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unafanywa na kampuni hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni eneo la upatikanaji wa leseni. Wananchi walio wengi wanaozunguka Wilaya ya Nachingwea wana kipato cha chini na wanatamani kujinufaisha na rasilimali ambazo zinapatikana katika maeneo yao kama taarifa inavyojionesha, lakini upatikanaji wa leseni hizi umekuwa na mlolongo mkubwa.
Je, Wizara inaweka utaratibu gani rahisi ambao utawawezesha watu wa Nachingwea kujimilikisha na kupata leseni waweze kuchimba wao wenyewe badala ya kuwa vibarua? Ahsante sana.
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ameulizia kuhusu uharibifu wa barabara na miundombinu kutokana na shughuli za utafiti. Shughuli za utafutaji ziko za aina tatu. Shughuli ya kwanza kabisa ambayo hufanywa na mtafiti wa madini ni kufanya utafiti angani. Utafiti wa aina hii haugusi ardhi na hauhitaji fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafutaji wa pili ni ule ambao wanaweza wakatumia mimea pamoja na miamba kwa kugusa tu juu ya ardhi na wenyewe hauharibu mazingira, lakini utafiti wa tatu, ni ule ambao mtafiti anahitaji kufanya drilling. Anapofanya drilling sasa anaharibu miundombinu ya barabara na ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huo sasa, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, taratibu za fidia kwanza kabisa, kama kuna miundombinu imeharibika kwa taratibu za utafiti na uchimbaji, Sheria ya Madini inatoa kifungu cha 96 kuhakikisha kwamba mwenye leseni ya utafutaji au ya uchimbaji wanakaa na mmiliki wa miundombinu kukubaliana aina ya uharibifu na viwango vya fidia. Ikishindikana fidia kwa taratibu za Sheria ya Madini ya mwaka 2010, basi Sheria za Ardhi za 1999 Namba 4 na Namba 5 ya 1999 Vijijini, hutumika kufanya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri sana wenye miundombinu hiyo wanaoshughulika na utafiti wakae na Kampuni hiyo wangalie uharibifu halafu waangalie namna gani ya kufidiwa barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni upatikanaji wa leseni za utafiti na uchimbaji wa madini. Natumia nafasi hii kuwaambia tu kwamba taratibu zote za kumiliki leseni za uchimbaji na utafutaji mdogo; utafutaji na uchimbaji mkubwa; zote huzingatia Sheria ya Madini. Utaratibu uliopo, kwa Waingereza wanasema ni first come first served. Anayeomba mapema ndiye anayeanza kufikiriwa kupewa leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wetu wa kutoa leseni ni ndani ya siku 14 tangu unapoomba na unaarifiwa. Ukishaarifiwa na wewe unajibu ndani ya siku 14. Pia mtoa leseni, Kamishna wa Madini kwenye ofisi zetu, anatoa leseni ndani ya siku nyingine 28.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nachukua nafasi hii kusema tu kwamba ni kweli kabisa upatikanaji wa leseni kwa utaratibu wa awali umekuwa ukitumika hivyo.
Hata hivyo, mwaka 2015 tumerekebisha Sheria ya Madini ya 2010, tumeingiza sasa kifungu cha waombaji kuomba leseni kwa kielektroniki, kwa kutumia mtandao. Kwa hiyo, unajaza fomu siku hiyo hiyo, unawasilisha fomu siku hiyo hiyo kwa njia ya mtandao na baada ya siku 28 unapata leseni. Kwa hiyo, nawaombe sana wachimbaji wa vijijini pia wanaweza wakatumia utaratibu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tumeboresha leseni kwa kuwegesha karibu na Ofisi za Madini kwenye Kanda zote. Sasa hivi karibu kila mkoa una ofisi tatu au nne za Madini. Kwa hiyo, nashauri basi, ili kupunguza mlolongo wa kuchelewa kupatikana kwa leseni, wananchi walio karibu na Ofisi zetu waende kwenye ofisi zetu ili waombe leseni na kuhudumiwa mapema iwezekanavyo.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved