Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:- Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?

Supplementary Question 1

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali la kwanza; kwa kuwa, Serikali imekiri upungufu wa Walimu katika Wilaya ya Magu, je, itakapoajiri itanipangia Walimu wa kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa bado tuna upungufu hasa wa Walimu wa sayansi. Serikali ina mkakati gani wa kuziba pengo hilo la Walimu wa sayansi?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza kuhusu upungufu wa Walimu napenda nimhakikishie kwanza kwamba angalau Wilaya yake ya Magu ina nafuu kidogo. Kuna baadhi ya Halmashauri zina upungufu wa Walimu kwa chini ya asilimia 60 ya mahitaji. Angalau wilaya yake ina asilimia zaidi ya 70. Kwa hiyo tutakapoajiri tutapanga Walimu kulingana na uwiano wa upungufu uliopo nchi nzima. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kuhusu upungufu wa Walimu wa sayansi; tulikuwa na upungufu wa Walimu wa sayansi kama 19,000. Sasa tumejizatiti, tunaandaa utaratibu wa kuajiri Walimu wa sayansi kama Walimu 6,000 mpaka mwishoni mwa mwezi wa Sita. Tunaamini upungufu wa Walimu wa sayansi mpaka 2020/2021 hatutakuwa nao tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge zima kwamba tumejindaa vya kutosha kuhakikisha kwamba tunapunguza upungufu wa Walimu wote wa sayansi na wa shule za msingi.

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:- Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?

Supplementary Question 2

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la upungufu wa Walimu katika Shule za Msingi Magu ni sawa kabisa na katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Je, Serikali inasemaje sasa kuweza kuhakikisha kwamba, suala hili linafanyiwa kazi?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yaliyopita, ni kwamba chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Rais wetu tunafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba tunapunguza kabisa tatizo la upungufu wa Walimu. Hatuwezi kulipunguza kwa siku moja au kwa mwaka mmoja kwa sababu mahitaji ni makubwa sana kulingana na payroll ya Serikali, lakini tunajitahidi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tunataka tuondokane na upungufu wa Walimu wa sayansi, hadi mwaka 2020/2021 tuwe hatuna upungufu wa Walimu wa sayansi. Kwa upande wa shule za msingi tunataka tupambane kuhakikisha kwamba ndani ya miaka michache ijayo tumepunguza kabisa upungufu wa Walimu wa shule za msingi katika halmashauri zote, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Name

Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:- Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?

Supplementary Question 3

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka kuwaambia tu Waheshimiwa Wabunge kuwa humu ndani kaingia mnyama mkali sana, lakini tuko salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali jana ilitoa kauli kuwa ili Tanzania ifanikiwe katika michezo ni lazima wachezaji wa timu ya youth watoke kwenye shule. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu kwenye shule, ili tuwe na oriented result youth team ya Tanzania? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala na naungana naye kwenye furaha yake ambayo naijua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Zungu kwamba shule yetu au chuo chetu cha michezo pale Malya - Mwanza Serikali inakiboresha; na tutapeleka Walimu kwa awamu ili wakafundishwe, ukiacha wale ambao wanasoma kutoka mashuleni, tunataka tupeleke Walimu ambao watafundishwa masomo ya michezo kwa muda ili waje kuboresha michezo kwenye shule zao wanazofundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tuna Walimu ambao wana uzoefu wa michezo, wengi tu ambao wanafundisha na Walimu wa michezo wako wachache. Nataka nitoe rai kwa Maafisa Elimu wote nchi nzima, kwamba Walimu wetu ambao wanafundisha michezo, wale ambao hawana cheti cha michezo basi wawape kipaumbele kuwapeleka kwenye chuo chetu cha michezo ili hatimaye tupate timu nzuri kwanza ya UMITASHUMTA na timu nzuri ya UMISETA ambayo itakuwa inapambana vizuri na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumeona mwaka huu zimepambana timu zetu za vijana na kushinda huko nje, inawezekana kabisa tukapata Timu ya Taifa bora kabisa kutoka kwenye shule zetu na vyuo vyetu baada ya muda mfupi ujao.

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:- Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?

Supplementary Question 4

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo TAMISEMI na Waziri anafahamu, Halmashauri ya Lushoto ina upungufu wa Walimu 826 wa shule za msingi. Sasa Serikali inatuambia nini kuhusu huu usumbufu ambao umesababishwa na Wizara yenyewe? Ahsante sana.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, ambaye juzi alikuwa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nikanushe kwamba upungufu wa Walimu haujasababishwa na Wizara yetu kwa sababu upungufu wa watumishi uko kwenye kila sekta na si sekta ya elimu peke yake. Tunafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba tunapunguza upungufu wa watumishi kwa Serikali nzima kwa sekta zote. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba tutakapokuwa tunaajiri na tutakapokuwa tunahamisha Walimu Halmashauri yake na Jimbo lake la Lushoto hatutaliacha nyuma.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:- Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?

Supplementary Question 5

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika kuziimarisha tawala za mikoa ni pamoja na kuziruhusu na kuzipa uwezo wa kufanya maamuzi yake zenyewe, ikiwemo kuwapangia vituo watumishi wapya ambao wanaajiriwa. Hata hivyo, lakini hivi karibuni Serikali mmebadilisha utaratibu, wanaoajiriwa hasa walimu mnawapangia vituo kutoka makao makuu, wenyewe, badala ya kupangiwa kule kwenye halmashauri ambako ndiko wanakojua mahitaji ya Walimu katika maeneo yao. Kwa nini Serikali wamepora madaraka ya Tawala za Mikoa, hasa Halmashauri, kupanga vituo vya watumishi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliokuwa unatumika zamani ulikuwa ni kwamba Serikali ikishaajiri basi lile rundo la waajiriwa au idadi ya waajiriwa inapelekwa katika halmashauri. Hapo inakuwa ni kazi ya halmashauri kuwapangia mahali pa kwenda kufanya kazi au vituo vya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopatikana kutokana na utaratibu huo ambao wenzetu walipata shida sana kuudhibiti ni vi-memo, vikiwemo vi-memo vya Wabunge. Akishapelekwa katika halmashauri fulani ki-memo kinafuata bwana huyo ni wa kwangu kwa hiyo msimpangie mbali na mji. Kwa hiyo unakuta Walimu wengi walipangiwa katika maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya, katika maeneo ya miji hasa wanawake, sitaki kueleza sababu kwa sababu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Nnauye kwamba baada ya kupata changamoto hiyo sasa Serikali imeamua kwamba tunapowapeleka; kwa sababu Maafisa Elimu wanakuwa wameleta yale mahitaji ya kila shule katika halmashauri yake; tunajua kwamba Yaleyale Puna wana Walimu saba, tunajua kwamba Pemba Mnazi wana Walimu watatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunajua kwamba kutoka makao makuu tupeleke Walimu watano Pemba Mnazi na tupeleke Walimu wawili Yaleyale Puna ili kusudi shule za pembezoni nazo zipate Walimu badala ya kupeleka vi-memo kwa Afisa Elimu. Ki-memo cha Mbunge kina nguvu sana kwa Afisa Elimu lakini ukileta kiā€“memo kwangu kinadunda tu, wala hakiwezi kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Nape Nnauye wala asipate wasiwasi, tunafanya hivyo kwa ajili ya kuangalia kwamba kunakuwa na usawa mkubwa kwa wale ambao wana uhitaji mkubwa wa kupewa Walimu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:- Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?

Supplementary Question 6

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Sekta za Elimu na Afya ni sekta ambazo zinaongoza kwa upungufu wa watumishi hapa nchini na tunaelewa Sekta ya Elimu inaandaa rasilimali watu wa Taifa na Sekta ya Afya inaenda kuhudumia hii rasilimali watu ili Taifa liweze kusonga mbele. Hata hivyo, upungufu umekuwa mkubwa sana kwenye hizi sekta mbili hasa. Nini mkakati wa Serikali wa muda mfupi na wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba sekta hizi angalau kwa asilimia 60 mpaka 70 zinapata watumishi?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, nadhani nimepatia sasa maana huwa ninakosea kosea sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii najibu kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kwa niaba ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, ambaye ni baba yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hadi sasa imetoa kibali cha kuajiri watumishi 52,000. Katika hao watumishi 52,000 kipaumbele kikubwa kimeelekezwa kwenye sekta hizi mbili, Sekta ya Elimu na Sekta ya Afya ambazo kwa pamoja zitakuwa na waajiriwa wapya wapatao 33,000 ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya waajiriwa wote ambao wataajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Paresso na Waheshimiwa Wabunge wote wa-support huu mchakato unaoendelea ambao utapunguza sana mahitaji au upungufu wa watumishi katika sekta hizi mbili ambazo ni muhimu sana katika nchi yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.