Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:- Jimbo la Mpwapwa lina tarafa mbili, yaani Tarafa ya Mpwapwa na Tarafa ya Mima, lakini tangu kuanzishwa kwa Tarafa ya Mima hakuna miundombinu yoyote iliyojengwa kama vile Ofisi ya Tarafa na vyumba vya watumishi:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Ofisi ya Afisa Tarafa na za watendaji wengine wa ngazi ya tarafa?

Supplementary Question 1

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze vijana wetu wa Timu ya Simba, wamefanya kazi nzuri sana ya kutwaa ubingwa kabla ya mechi zingine hawajacheza, hongereni sana. (Makofi/ vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili; mwaka 2011 aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Mizengo Pinda alitangaza kwamba Mima sasa ni Tarafa itakayokuwa na Kata za Berege, Kitemo, Mima, Ihondwe na Mkanana. Sasa ni miaka 11 hakuna hata jengo; na hizo Sh.50,000,000 sijaziona. Sasa nataka nimuulize swali Mheshimiwa Naibu Waziri, haya yalikuwa ni matamshi ya mdomo tu au hiyo tarafa ipo kwenye Gazeti la Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Tarafa hii ya Mima ina miundombinu mibovu sana; barabara zote hazipitiki, kuanzia Gulwe kuja Berege, Chitemo, hapa Mima Sazima, Igweji Moja, Igweji Mbili mpaka Seruka na kutoka Igweji moja kwenda Ihondwe njia ya mkato hazipitiki. Je, Mheshimiwa Waziri ana maelezo gani kwa wananchi wa Jimbo la Mpwapwa na hasa Tarafa ya Mima?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia angalia labda kuna Waziri amesimama lakini basi nitaendelea kulijibu mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje ni maswali magumu, na mimi napenda kuyajibu kama ifuatavyo. Ni kweli kwamba Mheshimiwa Mizengo Pinda alitangaza Tarafa ya Mima kuwa Tarafa mwaka 2011, wakati huo alikuwa Waziri Mkuu lakini ndiye alikuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba Tarafa ya Mima sawasawa na Tarafa nyingine imetangazwa kwenye Gazeti la Serikali na ndiyo maana akateuliwa Afisa Tarafa Maalum kwa ajili ya tarafa hiyo, kwa hiyo tunaitambua. Hizi Sh.50,000,000 amesema hajaziona, ni kweli hajaziona kwa sababu bado hazijapelekwa. Tunajiandaa kuzipeleka hivi karibuni na tumemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri kwamba atakapopata hizi fedha azi-commit haraka kwenye kazi ili kusudi kazi iweze kufanyika ya kujenga Ofisi ya Afisa Tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusu miundombinu; nchi yetu imekumbwa na matatizo makubwa sana hivi karibuni baada ya mvua kubwa kunyesha, maeneo mengi sana miundombinu imeharibika. Kwa hiyo hili najua ni swali la Wabunge wengi, lakini kwa Mima anaulizia kwa sababu kwa kweli kuna barabara huko hazijawahi kutobolewa na mambo mengine mengi na kazi ya kutoboa barabara ni kazi ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana nikitoka hapa Bungeni niweze kumtuma Mkurugenzi wetu wa Miundombinu atembelee Tarafa ya Mima. Baada ya hapo tutapata majibu mazuri zaidi.