Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Upendo Furaha Peneza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawapatia wachimbaji wadogo wadogo maeneo yaliyopimwa na kuwa na uwepo wa madini kama dhahabu, ikiwemo Moroko katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine yenye madini nchini?
Supplementary Question 1
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka 2016, Serikali ilitoa Kauli kupitia Naibu Waziri wa Madini kipindi hicho Mheshimiwa Dkt. Merdad Kalemani, kuwa Serikali inafanya mazungumzo na Geita Gold Mine ili uweze kupunguza baadhi ya maeneo ambayo yako katika leseni yake. Swali la kwanza, napenda kujua kwamba, hayo mazungumzo yamefikia wapi ili wananchi walau waweze kupata maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wachimbaji wadogo wadogo Geita kati ya malalamiko ambayo wamekuwa nayo ni pamoja na maeneo yanayotengwa dhahabu kuwa mbali sana na kutokana na vifaa vyao duni wanashindwa kuweza kuzifikia. Serikali kupitia corporate social responsibility kwa maana ya huduma za jamii ambayo mgodi umekuwa ukitoa kama vitu vya afya na vinginevyo, haioni kwamba ni muhimu sasa ikatoa mwongozo kwa Geita Gold Mine na maeneo mengine ili katika upande wa corporate social responsibility kuwajibika kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo yao hata katika ule msimu wa kupasua miamba ili walau waweze kuzifikia dhahabu katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Upendo Peneza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lile alilolizungumza la mazungumzo kati ya Serikali na Mgodi wa GGM kuwapatia maeneo ya kuchimba wachimbaji wadogo, ni kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo hayo kwa maeneo mbalimbali ambayo migodi inaona kwamba inaweza kuyaachia kuwapatia wachimbaji wadogo. Hii siyo kwa GGM peke yake tu, wachimbaji na wenye leseni wengi kuna mahali tunazungumza nao ili waweze kuachia maeneo ya wachimbaji wadogo. Hii itawasaidia wale wanaochimba wenye leseni kuwa na mahusiano mazuri na jamii. Kwa sababu haina maana yoyote kama anachimba halafu kuna uvamizi unaendelea. Kwa hiyo, ili kudhibiti hilo, ni vizuri wakaangalia eneo fulani wawagawie wachimbaji wadogo ili kuwe na amani kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili juu ya matumizi ya CSR kwa ajili ya kuasaidia wachimbaji wadogo. Sheria na Kanuni mpya ya Madini CSR kwa sasa mpango unaandaliwa na mwenye leseni lakini mpango huo unapelekwa kwenye halmashauri, halmashauri yenyewe wajibu wake ni ku- approve kuona kwamba hicho wanachotaka kukifanya wanakihitaji. Kwa hiyo, naomba halmashauri pamoja na wenye migodi wakae chini wazungumze waone kama kipaumbele chao ni kutumia CSR kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wanaweza kufanya hivyo. Hata hivyo, Mgodi wa GGM umefanya kazi kubwa sana, tunajenga kituo cha mfano kule Rwamgasa cha uchenjuaji, Mgodi wa GGM umetoa fedha kwa ajili ya kusaidia kazi hiyo.
Name
Joseph Kasheku Musukuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Primary Question
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawapatia wachimbaji wadogo wadogo maeneo yaliyopimwa na kuwa na uwepo wa madini kama dhahabu, ikiwemo Moroko katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine yenye madini nchini?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Niipongeze sana Wizara ya Madini kwa kipindi cha mpito toka Mheshimiwa Rais aliposema leseni ambazo hazifanyiwi kazi na watu wanaomiliki leseni nyingi na zinazoisha waruhusiwe wachimbaji wadogo waweze kuchimba. Mkoa wa Geita una raha kwa kuachiwa maeneo ya Rwamgasa, Nyakafulu, Stamico, Tembo-Mine na Bingwa. Je, Wizara ni lini mtawamilikisha wachimbaji wadogo ambao tayari wako kwenye maeneo ambayo yalikuwa leseni zake zimeisha na nyingine hazitumiki? (Makofi)
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anawapenda wachimbaji wadogo. Kwa kweli ametuelekeza tuwalee wachimbaji wadogo, tuwasimamie na tuwasaidie waweze kuchimba kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maeneo ambayo wameweza kupatiwa kwa ajili ya uchimbaji, ili tuweze kuwahalalisha ni lazima tuwapatie leseni. Naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba ndani ya wiki hii tunayo maombi zaidi ya 8,000 ya uchimbaji mdogo tunaanza kutoa leseni. Ahsante.
Name
Alex Raphael Gashaza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Primary Question
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawapatia wachimbaji wadogo wadogo maeneo yaliyopimwa na kuwa na uwepo wa madini kama dhahabu, ikiwemo Moroko katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine yenye madini nchini?
Supplementary Question 3
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi, ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa miongoni mwa Retention License zilizofutwa ni pamoja na Retention License No. 0001/2009 ambayo ilikuwa inamilikiwa na Kabanga Nikel Company Limited. Kwa kuwa sababu zilizokuwa zimesababisha Kabanga Nikel wasiweze kuanza kuchimba ni kutokana na bei ya nikel kushuka lakini pia miundombinu ya usafirishaji kwa maana ya reli na Ngara kutokuwa na umeme wa uhakika. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Tanzania na hususan wananchi wa Jimbo la Ngara, ambao walikuwa wanategemea mgodi huu kama ungeanza wangeweza kupata ajira na kuinua kipato chao?
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Alex Gashaza, Mbunge wa Ngara. Kabla sijajibu, niseme tu kwamba, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Alex Gashaza kwa ufuatiliaji wake kwenye mradi huu wa Kabanga Nikel, kwa kweli, amekuwa mtu ambaye kila mara anataka kujua nini kinchoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo jana Naibu Waziri wa Madini, Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Waziri walivyojibu, walieleza juu ya ufutwaji wa leseni zote za retention. Nataka niendelee kumwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba leseni hizi zote za retention zimefutwa kwa mujibu wa sheria na Serikali sasa inaangalia namna bora ya kuzisimamia leseni hizo ambazo zimerudishwa Serikalini.