Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Masoud Abdalla Salim
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtambile
Primary Question
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:- Serikali iliunda Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa Ibara 133 ya Katiba kupitia Sheria Na.15 ya Mwaka 1984 ili kila upande usimamie uchumi wake na uchumi wa Muungano usimamiwe na chombo cha Muungano:- • Je, ni kwa nini miaka 33 sasa Akaunti hiyo haijafanya kazi yake? • Je, gharama kiasi gani imetumika kuanzisha taasisi ambayo haina faida yoyote?
Supplementary Question 1
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru lakini nasikitika na majibu haya kwani ni majibu yale yale ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakitolewa hapa Bungeni na imekuwa kidogo hayaleti taswira nzuri kwa pande mbili za Muungano. Nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, katika majibu yake anasema kwamba Tume ya Pamoja haijaanza kufanya kazi kwa kuwa majadiliano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mapendekezo ya Tume hayajakamilika. Miaka yote hiyo mapendekezo wanajadiliana kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa mpewe muda gani? Mtuambie wananchi wanataka kusikia leo, mupewe muda gani mtaweza kukamilisha hayo mapendekezo? Ni miaka 33 ya Tume lakini tangu mapendekezo mwaka 2003 ni miaka kadhaa sasa, lakini hakuna kitu na wakati huo mnaendelea kutumia bilioni 31 point; mtuambie mnataka muda gani hasa, nusu karne au karne moja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Serikali yanasema kwa makini sana, Tume ya Pamoja ya Fedha imeandaa rasimu ya Mwongozo wa uendeshaji wa Akaunti ya Fedha ya Pamoja ambao unatarajiwa kutekelezwa mara baada ya majadiliano ya pande mbili za Muungano yatakapokamilika. Wameandaa rasimu sasa, miaka yote hiyo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atuambie maeneo machache ya rasimu hiyo, maana hakuna anayeamini tunaona ni kiini macho, kizungumkuti, tuambie hayo maeneo machache.
Mheshimiwa Spika, maeneo machache ya rasimu yaliyotayarishwa ni yapi? Kwa sababu tayari wameshaandaa rasimu lakini hakuna anayeamini, tunaona haya ni majibu tu ya kizungumkuti, kiini macho, kusadikika, tuambie hilo.
Name
Kangi Alphaxard Lugola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, napenda kuongezea majibu ambayo yamejibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Majibu ambayo sisi kama Serikali tunaamini yalikuwa ni majibu mazuri, majibu yanayojitosheleza, lakini kwa kiu ya Mheshimiwa Masoud anasema bado Serikali haina dhamira ya kuhakikisha kwamba hiyo Akaunti ya Fedha ya Pamoja inaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu ambayo ilipitishwa na Bunge hili, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, aliliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwezi wa Aprili, tarehe 22, Kamati ya Pamoja ambayo inahusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Muungano watakaa kwa ajili ya kuchambua mapendekezo ambayo yametoka kwenye Tume ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya Mheshimiwa Rais wa nchi yetu ilikuwa ahudhurie Mkutano wa Commonwealth kule London, Uingereza, lakini akawa amemtuma Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye ndiye Mwenyekiti wa hicho kikao cha Kamati ya Pamoja, kwa hiyo, matokeo yake kikao kile hakikufanyika. Aliporudi wakati kikao kile kilikuwa kimeandaliwa tena, akatumwa na Mheshimiwa Rais kwenda kwenye Mkutano wa SADC.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yale yote aliyoyasema tuko katika hatua nzuri. Mapendekezo yalishawasilishwa kwenye ile Kamati, ni uchambuzi tu ambao ukishafanyika yale maeneo ambayo alikuwa anasema ni maeneo gani yataweza kufanyiwa kazi na Mheshimiwa Mbunge atayafahamu. Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Name
Khatib Said Haji
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:- Serikali iliunda Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa Ibara 133 ya Katiba kupitia Sheria Na.15 ya Mwaka 1984 ili kila upande usimamie uchumi wake na uchumi wa Muungano usimamiwe na chombo cha Muungano:- • Je, ni kwa nini miaka 33 sasa Akaunti hiyo haijafanya kazi yake? • Je, gharama kiasi gani imetumika kuanzisha taasisi ambayo haina faida yoyote?
Supplementary Question 2
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Jambo hili ni la muda mrefu na limekuwa likijitokeza kila mara. Si aibu wala si ajabu kwa lile linalotushinda tukawa wakweli na tukafanya lingine tunaloliweza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, haikuwa aibu kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hilo limefanyika; na hili la Akaunti ya Pamoja kama linatushinda ni kwa nini lisiondolewe na tukatafuta njia nyingine au utaratibu utakaotuwezesha kuliendesha jambo hili katika mustakabali huo, badala ya kuendelea kuvunja Katiba kwa kutotimiza takwa hili la kikatiba? Ahsante.
Name
Kangi Alphaxard Lugola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khatib, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, masuala ya Muungano na zile changamoto zake tulishasema hapa Bungeni, changamoto zile 15 ambazo tulikuwanazo tayari 11 zimeshapatiwa ufumbuzi tumebaki na nne tu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii Akaunti ya Fedha ya Pamoja anayoizungumzia tusipokuwa makini na jambo hili, tusipokuwa na maridhiano, tunaweza tukaingia kwenye matatizo ambayo yatasababisha Watanzania kuanza kusema kwamba, afadhali hata hiyo Akaunti tusingekuwanayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko kwenye uendeshaji wa gari, tunapokuta kuna kibao kimeandikwa hapa uendeshe speed 50 au 80 na sisi hatuna budi kufanya hivyo. Katika jambo hili kuna umakini mkubwa ambao unatakiwa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Khatib Serikali ina dhamira ya dhati na wala hatuna kigugumizi na hatuna sababu yoyote ya kuuaibisha Muungano kwa sababu tulishaungana, haya mambo mengine yote haya tutayashughulikia vizuri. Atupe nafasi kwa sababu tumesema kile kikao kitafanyika, asiwe na haraka. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved