Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Wilaya ya Ukerewe inajumuisha visiwa 38 na kati ya hivyo, visiwa 15 hutumika kwa makazi ya kudumu lakini huduma za kijamiii hasa afya siyo nzuri:- (a) Je, Serikali inachukua hatua zipi za makusudi za kunusuru maisha ya watu hasa akinamama wajawazito na watoto wanaokufa kutokana na ukosefu wa huduma bora za afya katika visiwa hivyo? (b) Je, ni lini Maabara katika kituo cha afya Bwisya katika Kisiwa cha Ukara itakamilika na kupewa wataalam ili kutoa huduma ya upasuaji kunusuru maisha ya wananchi wa kisiwa hicho na visiwa vya jirani?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe masikitiko yangu kwamba Serikali haina takwimu sahihi ili kuweka kumbukumbu vizuri, Ukerewe tuna zahanati 29 na vituo vya afya vitatu. Kwa kuwa, suala la kupatikana kwa wataalam kwenye kituo cha afya cha Bwisya limekuwa ni la muda mrefu, niiombe sasa Wizara au Serikali kwa ujumla itoe commitment kwa sababu akinamama wengi sana wanapoteza maisha kwenye eneo lile, lini hasa ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana na kituo hiki kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Ukerewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri miaka miwili iliyopita ilijitahidi kujenga kituo cha afya cha Nakatunguru ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, lakini kituo hiki bado hakijaanza. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa vifaa na wataalam ili kituo hiki kiweze kuanza kutoa huduma na kwa maana hiyo kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni wazi tunaelewa jiografia ya Ukerewe kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema katika jibu langu la awali ni kweli, jiografia ya Ukerewe ina changamoto kubwa sana na Ukerewe tunaifananisha na Rufiji ambapo kuna deltas mbalimbali kiasi kwamba huduma za kijamii zinakuwa ni ngumu. Mheshimiwa Mbunge najua kwamba, siyo huduma ya afya peke yake, hata huduma ya elimu ina changamoto kubwa katika visiwa vile. Kwa hiyo, Serikali ina kila sababu ya kuangalia ni jinsi gani tunaweka kipaumbele katika visiwa vya Ukerewe ili hali ya kiafya iendelee vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la upatikanaji wa wataalam, naomba nikwambie kwamba sasa hivi tuko katika mchakato na siyo muda mrefu sana tutaajiri wataalam. Niwashukuru sana watu wa Ukerewe. Katika ile hospitali ya Nansio kuna vijana watano pale ambao ni Madaktari graduates wanajitolea na baada ya mawasiliano wameonesha wazi kwamba wale vijana wanataka kubaki kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie hili kwanza, kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutakapokwenda katika mchakato wa kuwapeleka wale Madaktari watano tutahakikisha wanabaki kule Ukerewe kwa ajili ya huduma ya afya. Kwa hiyo, mchakato wa upatikanaji wa Madaktari tunaufanya kabla hatujatoka katika Bunge hili, wataalam hao watakuwa wameshakwenda siyo Ukerewe peke yake, isipokuwa na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amesema kuna changamoto katika zahanati inayojengwa Nyakatungu. Naomba nimwambie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nitakuwa na hamu sana mara baada ya Bunge hili, niweze kufika Ukerewe nijue jiografia ya Ukerewe na kupanga mikakati tukiwa field kule, kuona tutafanyaje kutatua tatizo la afya la watu wa Ukerewe. Itanipa faida kubwa zaidi siyo afya peke yake, nitaangalia hata sekta ya elimu ambayo siku moja nimeona katika TV watoto wanavuka na boti kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kupata huduma ya elimu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved