Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Pamoja na nia nzuri ya Serikali kudhibiti ulimbikizaji wa madeni lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kila siku katika Idara za Halmashauri za Wilaya zinazopokea ruzuku ya matumizi ya kawaida toka Serikalini:- Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka fedha za ruzuku katika Halmashauri za Wilaya kama zilivyopitishwa na Bunge?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inapeleka fedha Halmashauri kulingana na makusanyo lakini kumekuwepo na malimbikizo ya madeni yanayotokana na stahiki za watumishi kama gharama za mazishi, matibabu yasiyo ya Bima za Afya, gharama za kufungasha mizigo kwa wastaafu, masomo na likizo. Je, ni lini Serikali italipa madeni ya mwaka 2016/2017 yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Januari, 2018? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali ilipunguza ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka asilimia 100 kwenda asilimia 40, mafungu niliyoyataja yanaonekana kuelemewa. Je, Serikali haioni ipo haja ya kufanya mapitio katika mafungu niliyoyataja na kuweza kuyaongezea bajeti? Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza la kulipa madeni ambayo yameshahakikiwa, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu imekuwa ikilipa madeni yote ambayo yamehakikiwa kwa ajili ya watumishi wetu. Kama ambavyo nimekuwa nikiliarifu Bunge lako Tukufu ni mwezi Aprili tu Serikali yetu ililipa zaidi ya shilingi bilioni 43 kwa ajili ya madai mbalimbali ya watumishi wetu katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongezewa kwa bajeti katika mafungu aliyoyataja Mheshimiwa Leah Komanya, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba katika mafungu ambayo tunayapa kipaumbele kuyapatia fedha za ruzuku ni Mafungu ya Utawala ambayo ndiyo yanashughulikia haya matatizo aliyoyasema kama gharama za mazishi na gharama za uhamisho. Kwa mfano, kwa mwaka huu 2017/2018 tuliomaliza tulikuwa na bajeti ya Sh.27,447,000,000. Kati ya hizi shilingi bilioni 27, Serikali yetu ilipeleka shilingi bilioni 22 kulingana na mahitaji yaliyoletwa kutoka kwenye Halmashauri zetu ambayo ni zaidi ya asilimia 90 ya bajeti ambayo ilikuwa imepangwa. Hili lilikuwa ni Fungu la Utawala ambalo ndilo linaloshughulika na madai mbalimbali aliyoyataja Mheshimiwa Leah Komanya.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo tunatoa kipaumbele kupeleka fedha za ruzuku ni katika Fungu la Elimu ambapo Serikali yetu imekuwa ikiajiri Walimu na tunahakikisha Walimu wetu wanalipwa pesa zao kabla hawajafika kwenye vituo vyao vya kazi au wanapofika tu kwenye vituo vyao vya kazi. Kwa mfano, kwa mwaka 2017/ 2018 tulipanga kupeleka shilingi bilioni 116 na tukapeleka zaidi ya shilingi bilioni 111 kulingana na mahitaji yaliyoletwa kutoka kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tunajua umuhimu wa mafungu haya na tunayapa kipaumbele katika kuyapelekea fedha za ruzuku.