Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janet Zebedayo Mbene

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ileje

Primary Question

MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:- Ileje iliwahi kuwa katika Wilaya zilizoongoza kwa ufaulu wa wanafunzi, lakini miaka ya hivi karibuni ufaulu umeshuka na hii ni kutokana na miundombinu mibovu ya mazingira ya kufundishia:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa inaboresha miundombinu yote muhimu kwa utoaji wa elimu? (b) Je, Serikali iko tayari kujaza pengo la Walimu liliko hivi sasa?

Supplementary Question 1

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini vile vile Ileje ina changamoto kubwa sana ya shule ya sekondari ya bweni ya wasichana. In fact hakuna shule ya bweni ya wasichana peke yake, hii inaleta changamoto kubwa kwa watoto kusafiri kwenda Wilaya nyingine au Mikoa mingine na ni gharama kubwa kwa wazazi na inaleta usumbufu. Watoto wengine wameshindwa hata kumaliza masomo yao. Je, Serikali iko tayari kutusaidia kujenga shule ya bweni ya wasichana kwa kuchangia nguvu na wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Ileje vile vile ni katika wilaya ambazo hazina vyuo vya ufundi vya aina yoyote. Tumejitahidi sana, tumepata mfadhili ametujengea VETA, hivi sasa karibu imalizike. Je, Serikali iko tayari kuchukua ile VETA kuiendesha, kuiwekea vifaa na kuwalipa Walimu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kukosekana kwa shule ya wasichana; tukiri wazi, ni katika miongoni mwa changamoto kubwa sana inayoikabili nchi yetu na kusababisha tatizo la ujauzito kwa vijana wetu ambao kwa njia moja au nyingine wanaposafiri kutoka majumbani mwao kwenda shuleni, katikati huwa wanakumbana na changamoto kubwa sana za ushawishi. Hili nimpongeze Mbunge huyu kwa kuona kwamba kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba wasichana wanatengenezewa eneo maalum kwa ajili ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu watu wa Ileje wameshaanza hili na sisi kwa njia moja au nyingine, tutashirikiana nao kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba tunapata wasichana wengi ambao kesho na keshokutwa watakuwa viongozi wa nchi yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutashirikiana na Jimbo lako na Wilaya yako katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba wasichana wanathaminiwa na kupata elimu bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze ninyi kwa kufanya harakati kubwa na kupata wadau mbalimbali walioshiriki mpaka kujenga hiki chuo cha VETA. Ofisi ya Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu tutaangalia jinsi gani tutafanya ili kuangalia jinsi gani chuo hicho kiweze kutumika kwa upana wake ili kuwafanya Watanzania hasa watoto wa Ileje na maeneo jirani waweze kupata elimu hiyo. Naomba tulichukue hilo kwa ajili ya kulifanyia kazi ofisini kwetu na Wizara ya Elimu.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, TAMISEMI, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbene na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano itawachukulia hatua za kisheria wanaume wote wanaowapa ujauzito watoto wa shule. Hatutakuwa na msalie Mtume, wanawake wamejaa mitaani ambao siyo wanafunzi, kwa hiyo hatutacheka na mwanaume yeyote ambae anawapa ujauzito watoto wa shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Kata na Mikoa kuwafuatilia wanaume wote hao na kuhakikisha wanafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba niongeze jibu la swali linalohusiana na VETA kwa Mheshimiwa Janet Mbene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wananchi hao wana majengo mazuri ambayo yalijengwa kwa kushirikiana na wafadhili wa JICA lakini hata kwa kuwatumia VETA walishakwenda wakakagua na wakaona yanakidhi viwango, isipokuwa sasa baada ya kutuandikia na kuona kwamba tuweze kukichukua, tulichowafahamisha kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Ndugu Rosemary Staki Senyamule wanachotakiwa ni kwanza eneo hilo lipimwe na kwa kuwa kile chuo kilikuwa kinamilikiwa na NGO, tunawaomba wakabidhi rasmi kwa Halmashauri. Halmashauri kupitia vikao vyake vya kisheria viridhie na kupitia kwenye RCC ili sasa hati hiyo ikishakuwa tayari ambayo pia ni pamoja na kuongeza kidogo eneo la chuo hicho, tutakuwa tayari kukichukua na kukifanya kiwe chuo cha Wilaya ya Ileje. Tunampongeza sana Mheshimiwa Janet Mbene kwa jitihada anazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.