Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Busanda
Primary Question
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:- Katika kutekeleza Mkataba wa Corporate Social Responsibility (CSR), Mgodi wa GGM unatumia bei za manunuzi kutoka nchi ya Afrika Kusini, mfano bei ya bati moja ni shilingi 81,000 na bei ya mfuko wa saruji ni shilingi 48,000. Je, kwa nini Serikali isiziite pande hizi mbili, Mgodi wa GGM na Halmashauri ili iweze kumaliza mgogoro huo na kuweka utaratibu mzuri?
Supplementary Question 1
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Menyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Inaonesha kwamba amefuatilia kweli katika Halmashauri ya Wilaya jinsi ambavyo imefanya kazi imekaa na GGM. Lakini vilevile niishukuru GGM kwa kuanza kutekeleza uwajibikaji wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 katika kipengele cha 105.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kuna baadhi ya makampuni ya uwekezaji katika sekta ya madini ambayo mpaka sasa hayajaanza kufanya utekelezaji wa sheria hii. Kwa mfano Mgodi ule wa Bacliff pale hawajaanza kufanya utekelezaji. Je, Serikai inasemaje sasa kwa makampuni ambayo hayajaanza kufanya utekelezaji wa sheria hii mpaka sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mgodi wa Bulyanhulu ambao uko Kahama umepakana sana na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, hasa katika Jimbo la Busanda katika Kata ya Butobela kule Nyakagwe pamoja na Kata ya Bukoli na wananchi walioko jirani na maeneo haya wananufaika, hasa wale wa Kahama, lakini wale wa upande wa Geita sasa ambao nimewataja wa Nyakagwe na Bukoli ni kilometa mbili tu kutoka kwenye mgodi ule lakini hawanufaiki chochote.
Je, Serikali inasemaje sasa kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Busanda pia, hasa wa maeneo ya Bukoli pamoja na Nyakago wanafaidika na mgodi uliopo Bulyanhulu ambao uko jirani sana na sisi?
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba Mgodi wa Bacliff ni kweli kabisa haujatoa CSR Plan yao kutokana na mujibu wa sheria inavyosema. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Mgodi ule wa Bacliff mpaka sasa hivi hawajaanza uzalishaji. Kwa hiyo watakapokwenda katika uzalishaji ni lazima watupe CSR Plan yao na CSR Plan yao lazima iwe shirikishi kwa kushirikiana na Halmashauri husika waangalie namna gani wataweza kui- finance miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya au Halmamshauri hiyo.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na wasiwasi, mradi huu wa Bacliff utakapoanza kufanya kazi basi lazima sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba wamekuja na CSR Plan yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kwa kampuni yoyote, nipende kutoa wito kwa makampuni yoyote ya uwekezaji, makampuni yote ambayo yanawekeza katika sekta ya madini ni lazima yatii sheria na taratibu zilizowekwa. Sheria ya mwaka 2017 na Kanuni zake za mwaka 2018 zinahitaji kila kampuni ilete CSR Plan yao kuhakikisha kwamba wanashirikiana na jamii au Halmshauri husika katika kuratibu na kuhakikisha kuwa wanatoa fedha katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni za mwaka 2018 zinasema kuna masuala ya local content plan pamoja na kile kiapo cha uaminifu. Ni lazima kila kampuni ikamilishe yale mambo ambayo yameainishwa katika kanuni za mwaka 2018, bila kufanya hivyo sisi kama Wizara hatutasita kuchukua hatua katika kampuni zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kuhusiana na wale watu ambao wamepakana na Wilaya ya Kahama na hasa ambao wapo karibu na Mgodi wa Bulyankulu, sisi tunafuata sheria. Sheria ndiyo zinazosema kwamba halmashauri husika iweze kufaidika kwa maana ya kupata service levy. Lakini vilevile nitoe tu wito kwa Mgodi wa Bulyankulu, kama inawezekana kata ambazo ziko karibu na mgodi huo basi waweze kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kwa kuwapa ajira kupitia ile kanuni yetu sisi ya local content kwa maana ya kuwajali Watanzania wanaoishi karibu na maeneo yale kwa kuwapa ajira lakini vilevile kuwapa fursa ya kuweza kuuza bidhaa na kuuza huduma mbalimbali katika mgodi huo. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved