Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Muhammed Amour Muhammed
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Bumbwini
Primary Question
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:- Kwa kipindi cha kirefu sasa nchi yetu imekuwa ikipeleka Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) nje ya nchi ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha misiba mikubwa sana kwa Askari wetu:- Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kadhia hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Majibu ya Serikali hayatoshelezi, ni afadhali tu kidogo. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mengine mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuna kauli mitaani zinasemwa na Watanzania kwamba Tanzania inashiriki hasa hasa kwa maslahi binafsi ya kukomba mali za DRC kwa mfano. Je, Serikali ina matamshi gani kwa lengo la kuwaosha Watanzania kutokana na tuhuma hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jeshi letu linapopigwa kwenye vita hasa pale DRC kuna kauli pia kwa Watanzania wanaamini kwamba Jeshi la Uganda linashiriki katika kulipiga Jeshi la Tanzania kwa kuwa wakati fulani kihistoria Waganda na Watanzania walipapurana kivita. Je, ni ipi kauli ya Serikali kuhusiana na kadhia hii? Ahsante.
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa bahati mbaya sana maneno kama haya yanatolewa na Watanzania ambao kwa kweli wanatakiwa wao wawe wazalendo na kuweza kupongeza juhudi za Serikali za kuwasaidia wenzetu ambao wako katika hali ambayo haina amani katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna suala la kukomba mali za DRC kwa maslahi binafsi, halipo. Tanzania haishughuliki na kuchukua chochote sehemu yoyote wanayolinda amani. Majeshi yetu yako kule kusaidia kurudisha hali ya amani, kuwalinda wananchi dhidi ya waasi ambao wanapigana katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Jeshi la Uganda linashiriki katika kuwapiga Watanzania pia halina ukweli wa aina yoyote. Matukio yote yaliyotokea tuna ushahidi wa kutosha kwamba ni vikundi vya waasi. Mwanzoni walikuwa M.23 na sasa hivi kuna vikundi vingine ambavyo vinatokea katika nchi mbalimbali za jirani pale lakini hakuna ukweli kwamba Majeshi ya Uganda yanashiriki katika kuwapiga askari wa Tanzania. (Makofi)
Name
Masoud Abdalla Salim
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtambile
Primary Question
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:- Kwa kipindi cha kirefu sasa nchi yetu imekuwa ikipeleka Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) nje ya nchi ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha misiba mikubwa sana kwa Askari wetu:- Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kadhia hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. MASOUD ABDALLAH SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna vikundi vya waasi ambavyo vinapelekea kufanya hujuma kwa Vikosi vyetu vya Kulinda Amani DRC - Kongo na maeneo mengine na pale inapotokea maafa kwa hawa askari wetu kupoteza maisha huwa kuna malipo maalum kutoka Umoja wa Mataifa lakini hata Serikali yetu nayo huwa kuna kiwango cha fedha ambacho wanatoa. Je, Serikali hasa ina mkakati gani wa ziada kuleta Muswada hapa Bungeni kuongeza muda wa kulipa wajane au wagane pale ambapo wanajeshi wanapoteza maisha katika kulinda amani DRC Kongo na Sudan Kusini na maeneo mengine? (Makofi)
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Umoja wa Mataifa na Serikali ya Tanzania imekuwa ikilipa mafao yanayohusiana na ushiriki wa askari wetu katika Ulinzi wa Amani sehemu mbalimbali. Vinapotokea vifo basi kuna fedha maalum na kuna viwango maalum vilivyopangwa ambavyo hutolewa na Umoja wa Mataifa na Tanzania sisi tunatoa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi na Kanuni za Majeshi zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza fedha kwa wajane, ni suala ambalo tunalitafakari kwa madhumuni ya kuweza kuboresha maslahi yote kwa ujumla siyo moja moja. Kwa sababu kuna maslahi mengi ambayo wanajeshi hawa wanatakiwa wayapate. Sasa hivi Sheria ya Ulinzi wa Taifa inapitiwa pamoja na Kanuni zake ili kuangalia ni viwango gani vya maslahi gani ambavyo vimepitwa na wakati ili viweze kuboreshwa kwa pamoja.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved