Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. HADJI H. MPONDA aliuliza:- Serikali kupitia aliyekuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa agizo la kuweka utatuzi wa kudumu katika migogoro ya ardhi iliyopo baina ya wananchi na Serikali katika maeneo ya vijiji na mapori tengefu. Aidha, katika kampeni zake Wilayani Malinyi Mheshimiwa Rais aliahidi uhaulishwaji wa Buffer Zone ya pPori Tengefu la Kilombero kwa vijiji vinavyopakana ili wawe huru katika shughuli zao, lakini hadi leo hakuna utekelezaji wowote. (a) Je, utekelezaji wa ahadi na agizo hili umefikia wapi? (b) Je, Serikali ina mpango mbadala kwa wananchi wanaoishi kihalali katika maeneo hayo ya Buffer Zone ya Pori Tengefu la Kilombero?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, buffer zone inayozungumziwa hapa katika Bonde la Kilombero ni pana sana, linaanzia kilometa tatu mpaka 12. Mheshimiwa Rais aliahidi angalau kuwasaidia wananchi hawa kipande kidogo tu cha hii buffer zone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili la uwekaji wa mipaka limeshakamilika kwa Wilaya ya Malinyi lakini bado kuna malalamiko mengi yamejitokeza na busara alizotumia Mheshimiwa Waziri wa Maliasili, ameunda tume lakini hata hiyo tume haiwashirikishi kabisa wananchi.
Swali langu, kwa nini sasa Serikali wasione busara kuanzisha upya tena mipaka hiyo kama walivyoanza mwaka 2016 kwa dhana ya kuwashirikisha wananchi kwa kikamilifu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi hawa sasa wanatoka kule kwenye buffer zone wanarudi kwenye ardhi ya vijiji, ardhi ya vijiji ndiyo vyanzo vya mito ambayo inatiririsha maji kwenye Mto Kilombero.
Sasa, je, Serikali ina mpango gani mahusus (commitment) kupitia taasisi zake za TAWA au TANAPA kuwezesha Wilaya ya Malinyi kutengeneza schemes za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo na mifugo katika eneo hili ili kuendeleza ustawi wa hilo Bonde la Kilombero? (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza kwa jinsia ambavyo amekuwa akilifuatilia hili suala na ambavyo amekuwa akishirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushirikishwaji wa wananchi ni suala pana na ni suala ambalo pengine bado linahitaji ufafanuzi; lakini tuna lengo kubwa kwamba lazima wananchi wote wa maeneo yote kwenye migogoro washirikishwe kikamilifu kupitia wananchi, viongozi wao, Serikali kwa ujumla na wadau wengine wote lazima washirikishwe na hilo ndiyo tumekuwa tukilifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, katika Wilaya ya Malinyi wakati tunaweka mipaka tulifanya vikao 27 na wananchi wakaelimishwa kwa nini tunahitaji kuhifadhi eneo lile na kwa nini lazima kuwe na buffer zone. Katika hivyo vikao tukafanya mikutano 12 na wananchi na katika hao wananchi walioshiriki katika hilo walikuwa ni 1,382; kwa hiyo, kwa ujumla walishirikishwa kwa mapana na marefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama kuna upungufu, namuomba Mheshimiwa Mbunge basi tutakaa tena tuangalie kama kunahitaji ushirikishwaji wa zaidi ya hapo basi tutafanya kama alivyoomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la scheme ya umwagiliaji; ni kweli kabisa kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya maji katika eneo lote zima katika Ramsar Sites.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunataka tuhakikishe kwamba lazima kuwe na matumizi endelevu ya maji katika lile bonde kwa sababu pale ndipo vyanzo vya maji ya Mto Kilombero ambao ndiyo utaenda kuzalisha umeme mkubwa kule Stiegler’s Gorge, kwa hiyo, lazima tuhifadhi vizuri na tuhakikishe kwamba wananchi wanaelimishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo basi tutashirikiana na wananchi, Serikali, Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Kilimo na kuona ni aina gani ya scheme zianzishwe katika maeneo yale ya juu kusudi wananchi wale waweze kunufaika na ule mradi. Zaidi ya hapo tutashirikiana pia na Bodi ya Bonde la Mto Rufiji ambayo ipo kule kwa ajili ya kuhamasisha na kuhakikisha kwamba wananchi hawaharibu vile vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ninaamini wananchi watafaidika na huu mpango wa scheme ambao Mheshimiwa Mbunge anapendekeza.