Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Josephine Johnson Genzabuke
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. DANIEL NSANZUGWANKO) aliuliza:- Mkoa wa Kigoma hususan Wilaya za Kasulu na Kibondo zimekuwa makazi ya wakimbizi kwa muda mrefu sana. Je, ni lini Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNHCR itakuja na mpango kabambe wa kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na ujio wa wakimbizi hao (a comprehensive plan and support for refugee affected areas)?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sijaridhika sana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na athari kubwa sana zilizoletwa na ujio wa wakimbizi Mkoani Kigoma, ongezeko la watu, miundombinu isiyotosheleza, ni lini hasa mpango kabambe utaletwa? Naomba commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ujio wa wakimbizi ndani ya Mkoa wa Kigoma, Makambi ya Wakimbizi ya Kibondo, Kasulu na Kakonko yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira; je, Serikali inalijua hilo? Ni mikakati gani ya Serikali katika kusaidia Mkoa wa Kigoma kutokana na athari hizo?
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza naona halijawa wazi zaidi, lakini kwa nilivyolielewa, ameuliza kuna mpango gani kabambe? Nadhani alikusudia mipango ambayo Serikali inafanya kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa katika kuhakikisha kwamba shughuli na huduma za maendeleo katika jamii, wananchi ambao wanazunguka makambi yale wanafaidika. Kama hivyo ndiyo, basi nataka nimhakikishie Mheshimwa Mbunge kwamba kuna miradi mingi ambayo imeshatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali na mashirika haya ya kimataifa chini ya UNHCR katika kuboresha huduma za jamii katika maeneo husika, kama ambavyo nimezungumza katika sekta ya afya, masoko, maji, elimu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na mazingira, ni kweli nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba ujio wa wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma kwenye makambi yetu umeleta athari kwenye eneo la mazingira. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana Serikali imechukua jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kwamba inakabiliana na changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika mambo ambayo tumefanya, kwanza ni matumizi ya majiko ambayo wanaita majiko ya ubunifu, ambayo sasa hivi badala ya kutumia kuni kukata miti ovyo, aina ya upikaji na uandaaji wa chakula kwa wakimbizi umebadilika kwa kutumia teknolojia ambazo zinapunguza athari kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ukataji miti ambapo fito zilikuwa zikitumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, umepungua kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi nyumba ambazo zinajengwa ni za kudumu kwa kutumia matofali, pamoja na kutoa elimu kwa wakimbizi na jamii husika juu ya umuhimu wa kuweza kudhibiti mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali imekuwa ikifanya kuhakikisha kwamba athari ya mazingira inapatiwa ufumbuzi katika maeneo hayo ambayo yana makambi ya wakimbizi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved