Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 1
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali ya nyongeza. Kwanza kabisa nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amenipatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefungua mradi wa REGROW ambao utafanya kazi ya kukuza utalii wa ukanda wa Kusini ukiwemo Mkoa wa Iringa; je, Serikali ina mkakati gani wa kujengea uwezo wananchi waliopo katika mkoa wetu ili watumie vizuri fursa hiyo kujiajiri na kuweza kujipatia kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nje ya maeneo ya utalii kuna historia kubwa za machifu akiwemo Mtwa Mkwawa, lakini kuna Kituo cha Kalenga, eneo la Mlambati ambapo Mwalimu Nyerere aliweka jiwe la msingi mwaka 1998 kama ukumbusho wa miaka mia moja.
Je, ni lini Serikali itachukua ya kuyaboresha kwa ajili ya kuvutia watalii na kuhakikisha kwamba pesa inayopatikana katika maeneo hayo, inawasaidia wananchi wanaozunguka eneo hilo? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kabla sijajibu haya maswali nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza kwa jinsi ambavyo amesimama imara katika kuupigania Mkoa wa Iringa, lakini pia alipigania sana kuhakikisha kwamba Kituo cha Utalii kinajengwa pale Kihesa, Kilolo. Kwa kweli nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ameuliza; je, tuna utaratibu gani wa kuhakikisha tunawajengea uwezo? Naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba katika mradi mkubwa ambao tunaenda kuutekeleza Mikoa ya Kusini unaohusu hifadhi nne yaani Udzungwa, Mikumi, Ruaha pamoja na Selous ya Kaskazini, tuna utaratibu wa kuimarisha miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi wa Mkoa wa Iringa waweze kufaidika na huu mradi, ni lazima wajengewe uwezo ili waelewe umuhimu wa kuuendeleza utalii na wawe tayari kuwakarimu watalii watakaokuwa wanatembelea katika Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivi sasa tuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba, kwanza tunawaelimisha namna ya kuanzisha makampuni ya kitalii ya kuongoza watalii, lakini pili, namna watakavyowakarimu pamoja na kuwaonyesha mambo mbalimbali ambayo yapo katika Mkoa wa Iringa ukiwemo utamaduni wa Iringa na tatu, ni pamoja na kuwapokea na kuwakarimu katika hoteli mbalimbali. Kwa hiyo, hii mipango yote tutaitekeleza katika mwaka wa fedha huu unaoanza Julai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kile Kituo cha Kalenga, kama alivyosema kweli kabisa miundombinu bado haitoshelezi. Hivi sasa tuna mpango kabambe wa kuhakikisha barabara ya lami inajengwa kutoka Iringa hadi kwenye lango kuu la Ruaha. Wakati tutakapokuwa tunajenga ile barabara, tutaangalia uwezekano wa kuimarisha ile miundombinu, kuchepusha pale kupeleka katika hiki Kituo cha Kalenga kwa sababu ni karibu ili tuhakikishe kwamba nako panafikika kiurahisi. (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 2
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Mbeya una vivutio vya asili kama ulivyo Mkoa wa Iringa na vivutio hivyo vya asili ni kama Mlima Rungwe, Mlima Kejo, Ziwa Nyasa na maeneo mengine kama Maziwa ya Masoko, Kingururu, Iramba pamoja na Daraja la Mungu.
Je, Serikali ina mpango gani kuvitangaza vivutio hivi ili wananchi wanaoishi maeneo hayo waone umuhimu wa uwepo wa vivutio hivyo? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa Mkoa wa Mbeya una vivutio vingi sana kama ulivyo Mkoa wa Iringa na kama ilivyo mikoa mingi. Hivi sasa kama nilivyosema, tunayo mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba vivutio vyote nchi nzima vinatangazwa. Nimesema tutaanzisha studio ya kutangaza na tutaanzisha channel ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mikakati hii, maeneo yote yenye vivutio vya utalii Mkoa wa Mbeya nayo yataingizwa katika huo mpango kabambe wa kutangaza ili kusudi watalii mbalimbali waweze kujua Tanzania na Mkoa wa Mbeya kuna nini? Nina uhakika Mheshimiwa Mbunge atafaidika sana hasa baada ya kuanza kutangaza maeneo haya. (Makofi)
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 3
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa Mkoa wa Mtwara una vituo vingi sana vya kitalii, kwa mfano, ile beach ya Msimbati ambayo inaweza kuendesha gari, kuna Shimo la Mungu kule Newala, lakini vilevile Newala kuna Kituo cha Utamaduni wa Kimakonde na Mji maarufu wa asili Mikindani.
Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kutangaza vivutio hivi? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika sehemu za Newala pamoja na Mikindani na maeneo mengine ya Mtwara yana vivutio vingi vya asili, maliasili na vitu vingi kwa kweli, hivi sasa naomba niseme tu kwamba tumechukua jitihada za kuhakikisha tunatangaza vyote kwa kushirikiana na Halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatangaza maeneo yote hayo na Mji wa Mikindani tutahakikisha kwamba tunautangaza ipasavyo kwa sababu una historia ndefu na nzuri ambayo nina uhakika watalii wengi watavutiwa kwenda kutembelea katika hilo eneo. (Makofi)
Name
Martha Moses Mlata
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 4
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mikoa ya Singida, Simiyu, Tabora na Shinyanga pia ina vivutio vyake; ukienda utakutana na akina Mtemi Chenge, Chifu Mayenga, Mtemi Gerege na wengine wengi.
Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembea mikoa hiyo ili tumwonyeshe vivutio hivyo aweze kuviingiza kwenye ramani ya utalii kwenye mikoa hiyo? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika mikoa yote aliyoitaja ina vitu vingi na ina historia ndefu ya utamaduni wa Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba nipo tayari wakati wowote kuongozana kwenda kutembelea mikoa hiyo na nitaomba wakati naenda tuongozane naye ili kusudi aweze kunionesha maeneo yote hayo na Serikali iweze kuyachukua na kuyatangaza ipasavyo. (Makofi)
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 5
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam lina vivutio vingi vya utalii kama vile Daraja la Kigamboni, Hospitali ya Ocean Road, Uwanja wa Uhuru, Magomeni pale kuna Nyumba ya Mwalimu Nyerere, Karimjee Hall na Makumbusho ya Taifa. (Makofi)
Je, Serikali imejipanga vipi katika kulisaidia Jiji la Dar es Salaam ambao wameanza zoezi hilo la kutangaza vivutio vya utalii kulipa nguvu ili waweze kufanya vizuri zaidi? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Dar es Salaam nayo ni miongoni mwa mikoa ambayo ina vivutio vingi vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, ndiyo maana tulianza na mkakati wa kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inatangazwa na tunaanzisha vituo vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshirikiana na Mkoa kuhakikisha kwamba tunaanzisha basi maalum ambalo litakuwa linatembelea vituo vyote, kuanzia pale Makumbusho, Magomeni na maeneo mengine yote aliyoyataja kwamba yanatangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tutaendeleza hizi jitihada ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba lile daraja letu la Kigamboni sasa linatumika kama mojawapo ya kivutio cha utalii. (Makofi)
Name
Lucy Fidelis Owenya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 6
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Moshi Vijijini Kata ya Mbokomu, tumekuwa tukizungumza mara nyingi kwamba kuna mti mkubwa sana ambao ni kivutio cha utalii pale; lakini Serikali haijachukua jitihada zozote kwenda kuutangaza mti ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kujua Mheshimiwa Waziri ana mkakati gani wa kuhakikisha wanautangaza mti ule uwe ni moja ya kivutio cha utalii katika Mkoa wa Kilimanjaro?
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nilikuwa sina taarifa kama kuna mti mkubwa wa namna hiyo, lakini naamini kabisa kama kuna mti mkubwa wa namna hiyo, basi itakuwa ni kivutio kizuri sana cha utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutachukua hatua za kuhakikisha kwamba kwanza nautembelea, lakini la pili, tuweze kuutangaza kusudi wananchi waweze kujua kwamba kuna mti mkubwa ambao ni kivutio kizuri sana katika Mkoa wa Kilimanjaro na katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo naomba niliseme, nchi ya Tanzania ni nchi tajiri sana ambayo ina vivutio vingi sana. Tukiwekeza, tutaweza kuivusha nchi hii na tutaweza kuisogeza mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tushirikiane Wabunge wote kuhakikisha vivutio vyote tunavitangaza kwa pamoja ikiwemo…
kwenye Instagram na Facebook mlizonazo muweke picha cha utalii. (Makofi)
Name
Willy Qulwi Qambalo
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Karatu
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 7
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Kata ya Buger na TANAPA, pia Vijiji vya Lositete, Upper kitete, Silahamo na Endamagang na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa migogoro ya muda mrefu ambayo haipati utatuzi.
Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari baada ya Bunge hili kuja Karatu ili kuongoza majadiliano ya kumaliza mgogoro huo?
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika lile eneo kuna baadhi ya migogoro ambayo imejitokeza na imekuwepo kwa muda mrefu, ninaomba niseme tu kwamba niko tayari pale ambapo tutapanga ratiba vizuri mimi na wewe tuende tukaangalie, tukawasikilize wananchi ili tuone ni namna gani tunaweza kutatua hiyo migogoro iliyopo.
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
Supplementary Question 8
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, urithi mkubwa wa Taifa letu unapotea. Ngoma zetu zinapotea, lugha zetu za asili zinapotea, vyakula vyetu vinapotea. Wewe ni Chifu, unafahamu hazina kubwa ambayo Machifu walikuwa nayo, mavazi yao, vyombo vyao vya nyumbani, samani zao na vyote hivi vinaweza vikavutia utalii kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni kwa nini usiwepo mkakati wa kila Halmashauri au kila Wilaya kujenga jumba la makumbusho na kwa sababu hiyo Viongozi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kuhamasisha wananchi ili vitu vyote vya asili vikakusanywa, kwanza kwa ajili ya elimu ya watoto wetu, lakini kwa ajili pia ya kuvutia utalii ikiwa ni pamoja na kuleta mashindano ya ngoma za asili ambazo zina mafunzo mengi sana kwa Taifa letu? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge mzuri sana ambaye amekuwa akifuatilia sana mambo ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niseme tu kwamba kama ulivyosema ni kweli kabisa tunayo mikakati mingi ambayo tunataka kuitekeleza. Lakini kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwa utaratibu wake aliyoanzisha wa kuhakikisha kwamba anashindanisha ngoma za asili, na hili ndilo tunalolitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi katika mkakati wa kuhakikisha kwamba hili tunalitekeleza, tumeamua kwamba mwezi wa Septemba kila mwaka, nchi ya Tanzania Mikoa yote, Halmashauri zote, zitakuwa zinasherehekea Mwezi wa Urithi wa Utamaduni wetu. Kwa hiyo, ngoma mbalimbali zitashiriki katika Kanda, katika Mikoa, kuhakikisha Watanzania wanakumbuka utamaduni wao. Nami ninaamini kabisa tukitekeleza hili kwa pamoja basi vitu vyote vile, mali kale zote zitaweza kubainishwa na kuweza kuelimishwa na wananchi wote wataweza kuvibaini vizuri kabisa. (Makofi)