Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Martha Moses Mlata
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA M. MLATA (K.n.y. MHE. AISHAROSE N. MATEMBE) aliuliza:- Sanaa ya Maigizo na muziki ni miongoni mwa Sekta zinazochangia asilimia kubwa ya vijana kujiajiri lakini kuna Vyuo vichache nchini vinavyotoa elimu hiyo ya sanaa ya muziki na maigizo ambavyo ni Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku masharti yake yakiwa ni changamoto kwa vijana wa mikoani:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha matawi ya Vyuo hivyo kwenye Kanda ama Mikoa ili kuongeza fursa zaidi kwa vijana?
Supplementary Question 1
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Naibu Waziri na naipongeza Serikali kwa sababu imeendelea kuimarisha sana Sekta hii ya Sanaa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa sasa Serikali inatambua umuhimu wa vijana kujiajiri kupitia sanaa; je, haioni sasa umefika wakati muafaka kuboresha vitengo vya Maafisa Utamaduni ambao kwa sasa hawana vitendea kazi. Ili waweze kuwapatia magari na fedha kwa ajili ya kuwafikia vijana hasa walioko vijijini na wenye vipaji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi sasa wamejitokeza kuonesha ufundi stadi wao katika sanaa mbalimbali, lakini kuna uharamia mkubwa sana katika mitandao, kuna fedha nyingi zimebaki kule. Je, Serikali haioni sasa umefika wakati muafaka wa kurasimisha zile kompyuta ambazo zinatumika kuuza miziki ya Wasanii, ili Serikali yenyewe ipate mapato, lakini na Vijana waweze kupata mapato kupitia mitandao hiyo? Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza kwa sababu amekuwa ni mpambanaji mkubwa sana ndani ya Bunge ya masuala yote ambayo yanahusu Sanaa pamoja na Wasanii.
Mheshimiwa Spika, sasa nikija katika swali lake ambalo ametaka kujua Serikali ina mpango gani katika kuboresha maslahi ya Maafisa Utamaduni Nchini. Nikiri kwamba sisi kama Serikali tunatambua kwamba, Maafisa Utamaduni nchini kote wanafanya kazi kwenye mazingira magumu. Hata hivyo, kwa sababu tunatambua pia kwamba sisi kama Wizara ya Habari, Maafisa Utamaduni wako kwenye Wizara ya Habari Kisera, lakini kiutendaji wanawajibika chini ya Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba tunaboresha, mazingira ya Maafisa Utamaduni nchini. Kama haitoshi nimhakikishie kwamba kwa sasa hivi, Wizara ipo katika hatua za mwisho kabisa za kuhuisha na kuboresha ile Sera yetu ya Utamaduni ya mwaka 1997 ili basi iweze kuendena na mazingira ya sasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ameuliza kuhusiana na kurasimisha kompyuta ili kuweza kutunza haki za Wasanii. Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba, tunatambua kabisa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana ya wizi wa kazi za sanaa. Sisi kama Serikali zipo jitihada mbalimbali ambazo tumezichukua katika kukabiliana na uharamia huo wa kazi za sanaa nchini. Si tu katika kurasimisha kompyuta, lakini kuna jitihada mbalimbali mojawapo ikiwa ni kutoa elimu kwa Wasanii wetu ili waweze kujua ni namna gani ya kuweza kuhifadhi kazi zao, lakini vile vile waweze kusimamia haki zao, kwa sababu changamoto kubwa imekuwa ni wao wanaingia mikataba ambayo haizingatii maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo kama Wizara tumefanya, ni kuhakikisha kwamba, sasa hivi tumeunda Kamati ambayo inapitia Mikataba yote ya Wasanii. Ni hivi juzi tu tumeshuhudia Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe akilivalia njuga suala la Mzee Majuto kudhulumiwa haki yake na nimhakikishie kwamba kwa sasa hivi tumefika kwenye hatua nzuri. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba Kamati hiyo itakapokamilisha kupitia hiyo mikataba yote ya Wasanii nchini, Wasanii wataweza kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi mwisho kabisa kwa sasa hivi, Wizara tuko katika kwenye mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Viwanda ili basi ile Idara ya COSOTA iweze kurudishwa kwenye Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni.
Ili basi matatizo yote ambayo yanawahusu Wasanii yaweze kushughulikiwa na Wizara Moja. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru.
Name
Mussa Ramadhani Sima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. MARTHA M. MLATA (K.n.y. MHE. AISHAROSE N. MATEMBE) aliuliza:- Sanaa ya Maigizo na muziki ni miongoni mwa Sekta zinazochangia asilimia kubwa ya vijana kujiajiri lakini kuna Vyuo vichache nchini vinavyotoa elimu hiyo ya sanaa ya muziki na maigizo ambavyo ni Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku masharti yake yakiwa ni changamoto kwa vijana wa mikoani:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha matawi ya Vyuo hivyo kwenye Kanda ama Mikoa ili kuongeza fursa zaidi kwa vijana?
Supplementary Question 2
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto kubwa inajitokeza kutokana na uhaba wa hawa Maafisa Utamaduni kwenye halmashauri zetu. Sasa Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Utamaduni ili kuweza kukidhi haja ya Sanaa. Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba, hapo nyuma kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya Maafisa Utamaduni kwenye halmashauri zetu, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, halmashauri nyingi zilishaandika barua ya kuomba vibali kutoka Utumishi vya kuweza kuajiri Maafisa Utamaduni. Mpaka sasa hivi karibu halmashauri nyingi zina Maafisa Utamaduni.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi sisi kama Wizara, tunaendelea na mchakato wa kuonesha kwamba tunaajiri Maafisa Utamaduni wapya, hususani katika Mikoa na Halmashauri ambazo ni mpya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo hilo kwa kiasi kikubwa sana limeshashughulikiwa na Wizara yetu ya Habari, nadhani hata Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved