Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maryam Salum Msabaha
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Sekta ya Utalii imekuwa ikitoa ajira kwa vijana wetu wa Visiwani na Tanzania Bara; kutetereka kwa sekta hii kumesababisha kupungua kwa ajira kwa kiasi kikubwa na vijana kurudi mitaani; Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha na kuboresha sekta hii ili ajira zipatikane kwa wingi?
Supplementary Question 1
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na Serikali kutoa elimu katika sekta hii ya vyuo vya utalii, lakini wamekuwa wakichukua wanafunzi ambao wamefeli au wanapata division four na kutofanya vizuri katika vyuo vingi na kusababisha hoteli nyingi za kitalii kuajiri wafanyakazi kutoka nje. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha vyuo vya utalii ili kuhakikisha wanachukua wale wanafunzi ambao wanafanya vizuri ili sekta hii iweze kufanya vizuri katika anga za kimataifa na hapa nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wenzetu Kenya, kwa mfano unatokea London unafika Airport ya Kenya, watalii wengi wanashuka sana Kenya na unaona ni namna gani wenzetu wamejitangaza katika sekta hii ya utalii na kupunguza tozo katika suala la utalii. Nauliza Serikali, je, haini sasa kuna umuhimu wa kupunguza kodi katika sekta hizi za utalii ili tuweze kufanya vizuri na kuingiza Pato la Taifa? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kumekuwa na upungufu wa wataalam katika Sekta hii ya Utalii na ndiyo maana kwa kuliona hilo, Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba kwanza tunakiimarisha chuo chetu cha utalii ili kiweze kutoa mafunzo. Kwa hivi sasa kilikuwa kinatoa mafunzo katika ngazi ya stashahada na astashahada, lakini kuanzia mwaka 2019 kwa ushirikiano pamoja na chuo cha Canada (Vancouver) tumeamua kwamba sasa tuanzishe programme ya kutoa degree, degree hizo zitasaidia kuandaa wataalam mbalimbali ambao watashiriki katika sekta ya utalii. Baadhi ya degree ambazo tunategemea kuzianza ni hizi zifuatazo:-
(i) Digrii ya ukarimu (degree in hospitality operations) ;
(ii) Digrii ya Utalii (degree in travel and tourism management) na
(iii) Digrii ya Utaratibu wa Matukio (degree in events management)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hizi degree tatu zitakapoanza ni imani yetu kwamba tutakuwa tunaweza kupata wataalam wale ambao sasa watakuwa wanatoka hapa hapa nchini na kuweza kuhudumia vizuri sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pia tunawahamasisha wawekezaji katika vyuo vingine vya binafsi waweze kuwekeza katika eneo hili kwa sababu sasa hivi mahitaji bado ni makubwa na wataalam bado ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwamba tunachukua wale waliofeli, si kweli. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo katika nchi hii, watu wote waliomaliza hata kama yuko division four kama ana āDā nne na kuendelea anaruhusiwa kujifunza na ngazi ya cheti (astashahada) na akifaulu anaendelea katika ngazi ya stashahada. Kwa hiyo, nadhani kwamba mkakati huu bado hatuchukui wale ambao ni failure, tunachukua wale ambao wana sifa za kujiunga na hivi vyuo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kuhusu kupunguza kodi katika huduma mbalimbali za utalii; ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba kodi hizi zinapunguzwa ili wawekezaji na watu mbalimbali waweze kushiriki katika hizi shughuli za utalii; na mmesikiliza katika hatua mbalimbali ambazo tumechukua. Hivi sasa bado tunaendelea kutazama ni aina gani za kodi ambazo zinaweza zikapunguzwa zaidi ili kusudi hii sekta iweze kuimarika zaidi nchini. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimependa niongeze majibu ya nyongeza kutokana na majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada tunazofanya za kuongeza kozi ambazo zinatolewa kwenye Chuo chetu cha Utalii lakini pia tunatambua kwamba sekta ya utalii pamoja na kwamba inaajiri watu zaidi ya 1,500,000 Chuo chetu cha Utalii toka kimeanza kimetoa wahitimu wasiozidi 5,000. Kwa maana hiyo wanaofanya kazi kwenye hoteli si lazima kwamba wanatoka kwenye chuo chetu cha utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hilo na kwa kutambua kwamba kuna wadau wengine ambao wanatoa taaluma ambazo zinatumika kutoa huduma kwenye sekta ya utalii kama VETA na vyuo vingine ambavyo vimesajiliwa na NACTE, tumeona tuanzishe mtihani wa Kitaifa ambao utaweka standard pamoja zote kwa usawa ili kila anayehitimu atoke kokote kule anakotoka afanye huo mtihani, aingie katika vigezo ambavyo vitakuwa vinatambulika kitaifa na sasa ndiyo aende kuajiriwa kwenye sekta ya utalii. Kwa sababu tunaamini, ili tuweze kupata watalii wengi, ni lazima tuongeze ubora wa huduma tunazotoa ili watalii wapate experience nzuri na wanapoenda kule kwao warudi tena kutalii lakini pia waseme maneno mazuri kwa watu wengine katika cycles of influence zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pamoja na jitihada hizo, tumetunga kanuni za kufanya certification ya professionals wanaotaka kuajiriwa kwenye sekta ya utalii, lakini pia tunaanzisha mafunzo ya Uanagenzi katika hoteli na maeneo yote ya utalii ili ku-boost kidogo quality ya watoa huduma kwenye Sekta ya Utalii. (Makofi)
Name
Daniel Edward Mtuka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Primary Question
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Sekta ya Utalii imekuwa ikitoa ajira kwa vijana wetu wa Visiwani na Tanzania Bara; kutetereka kwa sekta hii kumesababisha kupungua kwa ajira kwa kiasi kikubwa na vijana kurudi mitaani; Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha na kuboresha sekta hii ili ajira zipatikane kwa wingi?
Supplementary Question 2
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kw akunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Manyoni hususan Jimbo la Manyoni Mashariki tunavyo vivutio vingi sana vya utalii. Kwa mfano, tunazo kumbukumbu ya kituo kikubwa cha msafara wa watumwa wa njia ya kati kuanzia Ujiji, Unyanyembe kwenda Bagamoyo, lakini pia tunayo kumbukumbu ya ngome kuu ya Wajerumani iliyotumika kupambana na Mtemi Mkwawa wa huko Uheheni; lakini pia tuna jiwe la picha ya Bikira Maria kule Iseke. Je, Serikali iko tayari kusaidia kutangaza vivutio hivi ili kuinua kiwango cha ajira? Ahsante. (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, mimi mwenyewe juzi Jumamosi nilikuwa kule Wilaya ya Manyoni na nimetembelea katika maeneo yote aliyoyataja na kuona utajiri mkubwa ambao Wilaya ya Manyoni inao hasa katika haya maeneo ambayo ameyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambazo tunategemea kuchukua kama Wizara ni kwamba tutakwenda tutatangaza sasa vivutio vyote vile pamoja na historia nzuri ambayo ipo pale. Kuna jiwe moja ambali linajulikana kama jiwe la mjusi lakini zaidi ya hapo tumefika sehemu ambayo tunaita ndipo kitovu cha nchi hii yaani katikati ya Tanzania. Kuna maeneo mengi sana yenye vivutio vizuri sana kule Manyoni ambayo tutayatangaza sanjari na hatua ambazo tunazichukua katika kutangaza utalii katika maeneo yote nchini. (Makofi)
Name
Risala Said Kabongo
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Sekta ya Utalii imekuwa ikitoa ajira kwa vijana wetu wa Visiwani na Tanzania Bara; kutetereka kwa sekta hii kumesababisha kupungua kwa ajira kwa kiasi kikubwa na vijana kurudi mitaani; Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha na kuboresha sekta hii ili ajira zipatikane kwa wingi?
Supplementary Question 3
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wamiliki wengi wa hoteli za kitalii wanatumia wanafunzi waliopo kwenye mafunzo ya vitendo kufanya kazi za kuhudumia watalii na baada ya muda huo hawaajiriwi. Mchezo huu unasababisha ukosefu wa ajira kwa wahitimu kwa muda mrefu na kuikosesha Serikali mapato. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua taizo hili? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza yeye mwenyewe ni mhifadhi mzuri sana, kwa hiyo nampongeza sana kwa kuwa mhifadhi mzuri na naamini atatumia taaluma yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwamba, hoteli nyingi zimekuwa kweli zinawapokea vijana wanaotoka katika vyuo mbalimbali kwa ajili ya kupata field yaani kupata uzoefu ili waweze kwenda kuajirika katika maeneo mbalimbali. Hii ni hatua nzuri. Kwa hiyo, nafikiri hii ni ya kui- encourage zaidi ili kusudi hoteli nyingi zipokee hao vijana wetu, wafundishwe namna ya kufanya kazi kwa vitendo ili wanapoajiriwa pale waweze kutumia taaluma zao vizuri na waweze kufanya kazi ya kutoa huduma ile ambayo inastahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kuhusu ajira, ni kwamba tutaendelea kuhamasisha wawekezaji na hoteli mbalimbali ili ziweze kuwapokea vijana wetu ambao wamehitimu katika vyuo mbalimbali ili waweze kuajiriwa na waweze kutoa ile huduma nzuri. Pamoja na yale majibu ambayo Mheshimiwa Waziri ameshayatoa, basi jitihada hizi tunaamini kabisa kwamba zitasaidia sana katika kuboresha suala la ajira hapa nchini. (Makofi)