Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Albert Ntabaliba Obama
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 1
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Kwanza napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza kabisa Wizara hii inafanya kazi kubwa na ya kutukuka, lakini ni ukweli unaojulikana kwamba sisi katika Mkoa wa Kigoma na Katavi na hasa wananchi wangu wa Buhigwe umeme umechelewa kufika. Hivyo kwa commitment hii sasa ya Serikali kwamba ule mgogoro mtakuwa mmeumaliza kwamba Mei Mkandarasi atakuwa site. Kwanza kwa hatua hiyo kwa niaba ya wananchi wa Buhigwe na Mkoa wa Kigoma tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; viko vijiji kama ulivyovitaja mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba vimeshapatiwa umeme lakini kwenye vitongoji umeme bado haujaenda. Nataka kufahamu mkandarasi huyu atakayeenda kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyobaki je, atapeleka kwenye vitongoji, kwenye vijiji ambavyo tayari vimeshapewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, nini commitment ya Serikali kwa sababu sisi mmetucheleweshea umeme kwa muda mrefu na wananchi wangu wanahitaji umeme kwenye vijiji vyao. Je, mkandarasi hamtaweza kumkwamisha kwamba hamna hela? Naomba commitment ya Serikali.
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwape pole wakazi wa Mikoa ya Kigoma na Katavi, lakini niwashukuru sana Wabunge wa maeneo hayo ya Mkoa wa Kigoma, Jimbo la Buhigwe, Kasulu, Uvinza pamoja na Kigoma Vijijini pamoja na majimbo ya Mkoa wa Katavi kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia suala hili na kuwa na matumaini na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati pia nimepokea pongezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake yalikuwa mawili ambalo moja lilijielekeza vijiji ambavyo vimepatiwa umeme kama ambavyo jibu langu la msingi limesema, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo ambayo Serikali inatambua yapo maeneo ya vijiji yalipata umeme lakini vipo vitongoji havikupata huduma hiyo na ndiyo maana Serikali imekuwa ikitekeleza mradi wa densification yaani ujazilizi na kwa sasa kwa mwaka unaokuja wa fedha 2018/2019 Serikali imeandaa mpango wa densification awamu ya pili ambayo itaenda kwenye mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa huu wa Kigoma. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi ambao wote vitongoji ambavyo havina umeme kwenye vijiji vyenye umeme vitapatiwa huduma hiyo kupitia mradi wa densification.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge mkandarasi huyu atakapoanza kazi Mei, 2018 hatakwamishwa kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Fedha mpaka sasa imeshatoa pesa zaidi ya shilingi bilioni 221 ambavyo imetokana na chanzo hiki cha umeme (REA) ambao umetokana na tozo ya mafuta. Kwa hiyo, nimthibitishie Mbunge kwamba tatizo la pesa halipo, asante. (Makofi)
Name
Richard Mganga Ndassa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 2
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, tarehe 13 Julai, 2017 aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ambaye sasa ni Waziri wa Nishati alikuja kuzindua Mradi wa REA III katika Kijiji cha Nyamatala, Kata ya Ngula lakini hadi leo ni miezi saba hakuna hata eneo moja umeme umeshawaka. Nataka nipate majibu ya Serikali miezi saba sio Kitongoji, Kijiji wala Kata na uzinduzi huo ulikuwa kimkoa. Nataka nipate majibu ya Serikali tatizo hasa ni nini na umeme huu utaanza kuwaka lini.
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba ni kweli katika Mkoa wa Mwanza mkandarasi wa Nippo Group Limited yupo kazini na ninaomba nimfahamishe baada ya uzinduzi ule kazi ambazo ziliendelea ni pamoja na tathmini, uchambuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niliarifu Bunge lako kipindi kile ambapo miradi inazinduliwa yapo mahitaji mbalimbali ambapo yalijitokeza kutoka kwa Wabunge kutokana na uhitaji wa nishati hii Vijijini. Kwa hiyo, tathmini ya ilivyokuwa inaendelea kufanyika na maeneo mbalimbali ambako wakandarasi walikuwepo, vipo Vijiji pia vya nyongeza pia vimeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu kwamba kwa Mkoa wa Mwanza mpaka sasa mkandarasi yule ameshawasha Vijiji sita lakini naomba nimwelekeze Mkandarasi Nippo tulitoa maelekezo kwa wakandarasi wote wafanye kazi katika Wilaya zote, wawe na magenge ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pengine changamoto inayojitokeza mkandarasi huyu yupo katika Wilaya zingine hajafikiwa katika Jimbo lake. Lakini naomba nimthibitishie na wizara kwa awamu hii imepanga kufanya ziara katika Jimbo lake na kazi zitaendelea na kwa sababu mikataba hii inaonyesha na muda wa kazi ni kuanzia kipindi hiki mpaka Novemba, 2019 ndio zinakamilika, naomba nimtoe wasiwasi yeye Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo lake kwamba huduma hii ya umeme vijijini kama ilivyozinduliwa itapatikana kwasababu mkandarasi yupo ndani ya wakati, asante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri katika swali la Mheshimiwa Ndassa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Ndassa kwa kweli wakati tunakwenda kuzindua alifanya kazi kubwa sana, lakini nimpe taarifa katika Jimbo lake tayari wakandarasi wapo katika Kijiji cha Nyamatara na Nyambiti; na Nyambiti na Nyamatara kesho wanawasha umeme. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Mheshimiwa Katibu wake na jana tuliwasiliana naye pale Nyamatara wameshasimika nguzo, transfoma wamepeleka juzi na kesho na keshokutwa wataendelea kuwasha kwenye vijiji viwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Nguge pamoja na Nipo katika Mkoa wa Mwanza pia wameshawasha umeme lakini pamoja nahayo nitawasiliana na Mheshimiwa Ndassa tukae naye vizuri ili maeneo mengine vipaumbele tuweze kuwapelekea umeme haraka iwezekanavyo.
Name
Hasna Sudi Katunda Mwilima
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 3
MHE. HASNA MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Kwenye Vijiji vyangu vya Mwakizega, Kabeba na Lilagala tangu Awamu ya II ya REA nguzo zimeshawekwa na taratibu zote zimekamilika. Mradi ule ulitakiwa uzinduliwe mwezi wa pili mwaka jana 2017 lakini kwa masikitiko yangu makubwa Mheshimiwa Waziri umeshakuja Kigoma umepita umeenda Kibondo, wananchi wanauliza maswali, tumewekewa nguzo na transfoma tuizone? Ni lini umeme wa Kata hizi mbili za Mwakizega na Ilagala utawashwa rasmi? (Makofi)
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mwilima kweli nilitembea naye katika maeneo yake. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge huyu kwa sababu kwanza tulienda eneo la Nguruka lililokuwa na shida kubwa tukawasha umeme Nguruka tukiwa pamoja, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo ambayo ameyataja eneo la Ilagala pamoja na Nguruka huyu mkandarasi wa REA Awamu ya Tatu anyekuja kufanya kazi ni kati ya maeneo ambayo ataanzia kuyafanyia kazi na kuyawashia umeme. Kwa hiyo, nimpe tu pongezi Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira wakati…
...mkandarasi tunampata katika mwezi huu kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza, tarehe 5 Mei ataanza kazi katika maeneo hayo na maeneo yatakayowashwa ni pamoja na Ilagala pamoja na Nguruka maeneo yaliyobaki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira tutafanya kazi pamoja.
Name
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 4
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme Kigoma ni wingi wa umeme na bahati mbaya sana Kigoma bado haijaunganishwa na Gridi ya Taifa na hata mpango ambao ulisainiwa kwa msaada wa Serikali ya Korea ambao Waziri wa Fedha alisaini takribani mwaka na nusu uliopita bado kabisa kuanza kutekelezwa. Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Mto Malagarasi, Igamba III ambao ndio jawabu la kudumu la umeme katika Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
Name
Dr. Faustine Engelbert Ndugulile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe sahihisho kidogo sio Malagarasi Igamba III; ni Malagarasi Igamba II. Baada ya kusema hayo sasa ni kweli kabisa mradi wa Malagarasi ilikuwa kwanza utekelezwe wakati wa mradi wa MCC mwaka 2008, lakini ikaonekana kwamba kulikuwa kuna matatizo ya REA species.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe taarifa katika Bunge lako tukufu ni kweli kabisa mradi huu sasa utaanza kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha na tumeshatenga fedha na juzi Mheshimiwa Zitto nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge tulikuwa nao wakati tunakamilisha majadiliano ya Benki ya Maendeleo ya Dunia kwa ajili ya kufadhili mradi huo na zinahitaji dola milioni 149.5 kwa ajili ya kuutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Mbunge mradi huu unakwenda kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha, ahsante sana. (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 5
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Jimbo la Ukonga na tukafanya mikutano mpaka saa moja usiku, namshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu nijue kwamba Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme ambayo Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wanafahamu. ningependa nijue katika hii mipango ya REA ambayo inaendelea Ukonga nao wategemee nini? Ahsante.
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Na mimi naomba nimpongeze Mbunge Mheshimiwa Waitara ni kweli tulifanya mikutano zaidi ya sita katika Jimbo lake na nimthibitishie baada ya mikutano ile kwa mwaka wa fedha unaokuja 2018/ 2019 Serikali inakuja na mpango wa Peri-urban kwa maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na kisha itaendelea Peri-Urban II. Ahsante.
Name
Victor Kilasile Mwambalaswa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 6
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaishukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara sasa hivi mkandarasi yupo Wilayani Chunya kwa kupeleka umeme REA III, anafanya upimaji katika Vijiji vya Ifumbo, Soweto, Mawelo na vinginevyo. Kuna Kijiji kinaitwa Itumbi katika Kata ya Matundasi, kijiji hiki Serikali kupitia Wizara inajenga kituo cha mafunzo kwa wachimbaji wadogo (center of excellence) lakini Kijiji hiki hakimo kwenye Awamu namba tatu ya kupeleka umeme. Je, Serikali haiwezi kukiangalia Kijiji hiki kwa jicho la pekee na kupeleka umeme katika awamu hii ya tatu?
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge katika swali lake. Kwa kweli kituo cha Matundasi pamoja na Itumbi ni kati ya maeneo ambayo yapo kwenye center of excellence kwa upande wa madini na baada ya kufanya survey Mheshimiwa Mbunge, kijiji kipo kwenye mpango sasa kwa sababu ni maeneo ya vipaumbele kwenye miradi ya maendeleo, kwa hiyo, kipo kwenye mpango wa fedha wa mwaka huu. (Makofi)
Name
Flatei Gregory Massay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 7
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Vijijini lina uhaba sana wa umeme na Mheshimiwa Waziri amefika. Sasa lini atakuja kuwasha umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini na anafahamu kwa sababu amefika na vijiji vingi havina umeme. Atutajie tu lini atafika Jimbo la Mbulu Vijijini kuwasha umeme? Ahsante.
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, vijiji vya Mheshimiwa Mbunge vya Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini vyote vipo kwenye mpango wa REA mwaka huu.
Name
Abdallah Ally Mtolea
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 8
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wanahitaji umeme tena umeme wa uhakika lakini tumekuwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme katika Mkoa mzima wa Dar es Salaam na hasa kule Temeke; na mwaka jana Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi hapa kwamba kufikia Disemba 2017 tatizo la kukatika kwa umeme litakuwa limekwisha, leo ni mwezi wa nne mvua zinanyesha na umeme unakatika sana Jijini Dar es Salaam. Serikali mnatuambia nini kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme? (Makofi)
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Kwanza napenda nitoe taarifa katika Bunge lako hili, katika maeneo ya Mbagala na Gongolamboto kulikuwa na kero kubwa sana ya kukatika kwa umeme, wiki mbili zilizopita tumejenga sub - station imekamilika na kwa hiyo Mbagala sasa nina amini wanapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, umeme huu wa Mbagala ambao ni wa gridi naishukuru sana Serikali yetu, tumeanza sasa kuunganisha umeme wa gridi kutoka Mbagala kwenda Ikwiriri kupitia Kibiti mpaka Somanga Fungu na umeme huu wa Mbagala ambao unatoka kwenye Gridi ya Taifa ndio tunaunganisha katika Mikoa yote ya Mtwara na Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuanzia mwezi uliopita nitoe taarifa katika Bunge lako kwamba hata Mikoa ya Mtwara na Lindi sasa itakuwa inapata umeme wa gridi badala ya umeme wa mashine inayotumia sasa. Hizo mashine zilizopo sasa zitatumika tu kama mashine za ziada. Kwa hiyo nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu inanisaidia sasa kutoa taarifa kwa wananchi wa Mbagala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kukatika kwa umeme kunatokana na sababu nyingi, sio sababu ya kuwepo kwa umeme au miundombinu, wakati mwingine ni kasoro ndogo ndogo, tunakiri kabisa zipo changamoto za maeneo machache kukatika kwa umeme katika baadhi ya nyakati za mida. Tutashirikiana na Waheshimiwa Wabunge kutatua matatizo hayo. Tunachoomba tupate taarifa inapotokea itilafu ya namna hiyo, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa wananchi wa Mbagala kwa sasa wanaendelea kupata umeme wa uhakika zaidi. (Makofi)
Name
Musa Rashid Ntimizi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana. Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
Supplementary Question 9
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali inafanya vizuri sana kwenye umeme vijijini lakini bado tuna tatizo kubwa kwenye umeme mjini ikiwemo Singida Mjini yapo maeneo ambayo hayana umeme. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kutuletea umeme?
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge Sima. Pamoja na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini tulifanya ziara katika Mkoa wa Singida na katika Wilaya ya Singida Mjini tuliona hilo tatizo. Kwa hiyo, nataka niseme ni kweli Serikali inatambua tatizo la uwepo wa ukuaji wa maeneo ya mijini na changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa hiyo, inakuja na mpango wa Peri-Urban ambao utapeleka umeme katika miji inayokua kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019.