Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Anne Kilango Malecela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Primary Question
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:- Barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba Wilaya ya Same ni korofi sana na kusababisha usafiri wa barabara ya Tarafa ya Mamba/Vunta kuwa mgumu:- Je, Serikali inawasaidiaje Wananchi wa Tarafa ya Mamba/Vunta ili waweze kuendelea kiuchumi?
Supplementary Question 1
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, Wilaya ya Same, ni Wilaya ambayo takribani, eneo lake katika Mkoa wa Kilimanjaro ni 40% ya eneo zima la Mkoa wa Kilimanjaro. Lakini Wilaya ya Same mara kwa mara inatengewa pesa kidogo sana inapewa pesa zilizoko chini ya wilaya ambazo ni ndogo zaidi ya wilaya ile. Naomba Serikali ione kwamba haioni umuhimu wa kutenga pesa zinazolingana na ukubwa wa Wilaya ile ya Same ambayo ni takribani 40% ya eneo lote la Mkoa wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili nakuja kwenye barabara hii ya Hedaru – Vunta – Myamba barabara hii ni korofi mno, sijawahi kuona barabara kama hii, Awamu ya Nne niliwanyenyekea hapa Bungeni kwamba barabara ya Mkomazi, Kisiwani Same, waiweke kwa vipande vipande, walifanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa barabara hii yenye kilomita 42.2 hii TARURA Same wamefanya tathmini ya kutengeneza barabara yote kwa ujumla, wakapata ni bilioni 1.8.Je, Serikali hamuoni kwamba kwa sababu wananchi hawa wanahangaika mno mkatengeneza vipande vipande ili mmalize tatizo lote, kuliko mnavyochukua vimilioni viwili vitatu?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kwanza kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza nimpongeze kipekee Mheshimiwa Kilango Malecela jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wake wa Same na sisi sote ni mashahidi Kiwanda kile cha Tangawizi kimejengwa ni kwa ajili ya kazi kubwa aliyofanya yeye.
Mheshimimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mgawanyo wa fedha umekuwa hauendani na uhalisia na hili ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI baada ya kuliona hilo sasa hivi tuna-commission consultant kwa ajili ya kuja na formula nzuri itakayosaidia ili tunapogawa fedha twende na uhalisia. Kwa sababu formula inayotumika ndiyo iliyokuwa inatumika mwanzo kabla TARURA haijaanza kufanya kazi. kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Kilango Malecela na Wabunge wengine tuvute subira kwa sababu tayari consultant anafanya kazi atatuletea majibu na formula ambayo itakuwa nzuri kwa kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili anaona iko haja kwa ajili ya ukorofi wa ile barabara tuanze kujenga kwa kiwango cha lami walau kilometa chache chache at the end tuje tukamilishe kilometa zote 42. Ni wazo jema kwa sababu vinginevyo tunakuwa tunarudia fedha inatumika lakini kwa mazingira na jiografia ya barabara ambayo Mheshimiwa ametaja iko haja kubwa sana.
Name
Eng. James Fransis Mbatia
Sex
Male
Party
NCCR-Mageuzi
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:- Barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba Wilaya ya Same ni korofi sana na kusababisha usafiri wa barabara ya Tarafa ya Mamba/Vunta kuwa mgumu:- Je, Serikali inawasaidiaje Wananchi wa Tarafa ya Mamba/Vunta ili waweze kuendelea kiuchumi?
Supplementary Question 2
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, barabara za Mkoa wa Kilimanjaro zikiweko za Same pamoja na za Vunjo na mkoa wa ujumla ziko kwenye maeneo ya mwinuko. Na barabara zote hizi, zinavyotengenezwa zinawekewa fedha kidogo ambazo sasa haziendani na hali halisia ya soil property au tabia ya barabara hizo. Je Serikali haioni umuhimu, wa kutafuta aina ya material ambayo ni nzuri na ambayo siyo ghari kama ilivyo beachmen ili kuweza kufanya barabara hizo ziweze zikapitika kwa urahisi na kuongeza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo ambalo Mheshimiwa Mbunge anatoa ni wazo jema na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tumekuwa tukifanya majaribio na tumeanzia Wilaya ya Bihalamuro tulienda na Mheshimiwa Mukasa. Kuna stadi ambayo inafanyika namna ya kuweza kujenga barabara kwa gharama nafuu lakini barabara ambazo zitaweza kudumu kwa kipindi kirefu. Kwa hiyo, ni wazo ambalo tunalifanyia kazi hakika baada ya kujiridhisha juu ya uwezo wa barabara hizo kuhimili kudumu ni wazo ambalo tutalifanyia kazi kujenga barabara zetu kwa gharama nafuu lakini ambazo zitadumu kwa muda mrefu.
Name
Deogratias Francis Ngalawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Primary Question
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:- Barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba Wilaya ya Same ni korofi sana na kusababisha usafiri wa barabara ya Tarafa ya Mamba/Vunta kuwa mgumu:- Je, Serikali inawasaidiaje Wananchi wa Tarafa ya Mamba/Vunta ili waweze kuendelea kiuchumi?
Supplementary Question 3
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, Wilaya ya Ludewa eneo la Kandokando mwa Ziwa Nyasa kuna vijiji takribani kumi na mbili, gari, baiskeli wala pikipiki haijawahi kufika huko. Niishukuru Serikali kuna kipande cha Mwambahesa kwenda Makonde, kimeanza kufanyiwa kazi. Je, TARURA inafikiriaje sasa kutuongezea wananchi wa Ludewa hususani waishio kandokando wa Mwambao wa Ziwa Nyasa kutoka eneo la Makonde mpaka kihondo ili tuweze kupata barabara?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kutembelea jimbo la Mheshimiwa Ngalawa, kama kuna maeneo ambayo kuna changamoto ya milima maana kule milima ya Livingstone ndio inapita kule, ukanda ule, ni ukanda wa kutizama kwa jicho tofauti kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Mbunge naye amekiri kwamba kuna kazi nzuri ambayo inafanyika juu ya kuhakikisha kwamba wananchi wale wanakuwa na barabara ambayo inapitika vipindi vyote. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba kila eneo ambalo wako wananchi wetu, barabara zinapitika vipindi vyote, kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu na yeye pia tutahakikisha kwamba wananchi wake wanapata barabara ya uhakika.