Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Leonard Haule

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:- Jimbo la Mikumi linaitwa Jimbo la giza kutokana na kata zake nyingi kutokuwa na umeme, kama Kata ya Ulaya, Zombo, Tindiga, Mhenda, Kilangali, Vidunda na kadhalika:- Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Jimbo hilo ambalo limebarikiwa kuwa na Mbuga za Wanyama na vivutio kadha wa kadha?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwanza nioneshe masikitiko yangu makubwa sana kwa Jimbo lenye chanzo kikubwa cha umeme kama Kidatu lakini pia ni Jimbo la Utalii kuwa na vijiji kama 57 lakini ni 16 tu ambavyo vina umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, ni kweli mkandarasi kweli State Grid yuko kule site na kwa muda mrefu ameonekana kuchimba mashimo na sasa hivi hajaonekana kwa sababu anasema kwamba ana tatizo la
nguzo. Je, ni lini maeneo haya ya Zombo, Ulaya, Muhenda, Tindiga, Vidunda, Uleling’ombe, Kilangali na Mwinsagala wataweza kupata umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali na mbili, kwa kuwa kuna maeneo ambayo kuna nguzo na umeme umepita lakini maeneo hayo hayajapata umeme, mfano maeneo ya Ruaha Darajani, Kikwalaza, Mshimba lakini pia maeneo ya Ruhembe na Tambuka Reli, Kipekenya na maeneo ya Malolo. Je, ni lini serikali itawapatia umeme wananchi wa maeneo hayo kama ilivyofanya kwenye maeneo ya Nyanda za Juu Kusini.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge kwenye swali lake la kwanza la nyongeza amejielekezea katika kazi zinazoendelea katika Jimbo lake kupitia mkandarasi State. Amesema mkandarasi alionyesha kuna tatizo la nguzo, naomba nimtaarifu mkandarasi huyo nimewasiliana naye asubuhi hii na kwamba kweli kulikuwa na tatizo la nguzo. Lakini Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu na uongozi wa Mkoa wa Iringa ulifanya kikao kikubwa na ulifikia makubaliano na sasa wakandarasi wote nchi nzima wanapata nguzo na ninavyozungumza takribani nguzo 4000 zimeshaenda katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika eneo la Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwamba mkandarasi yupo katika Mkoa wa Morogoro na anaendelea na kazi na Mheshimiwa Mbunge amekiri na kwa kweli kwa kuwa nguzo zimeruhusiwa na hivi asubuhi nilivyokuwa nawasiliana naye, mkandarasi ametoa taarifa ya kwamba anaendelea kwenye maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeyataja kwenye swali lako la msingi na kwamba pia alikuwa ameagiza mita takribani 3000 na karibu zinafika mwezi wa pili Dar es Salaam. Kwa hiyo, kazi ya uunganishaji katika vijiji hivyo itaendelea vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili umejielekeza katika maeneo ambapo kuna miundombinu ya umeme kwa mfano Ruaha Darajani, lakini wananchi hawajaunganishiwa umeme. Nataka nikutaarifu Mheshimiwa Mbunge Serikali yetu ya Awamu ya Tano imekuja na mradi mwingine wa ujazilizi awamu ya pili ambao utaanza Machi, 2019 kwa gharama ya shilingi bilioni 197 na wafadhili wa Norway, Sweden na Serikali ya Ufaransa pamoja na Serikali ya Tanzania na mradi huu unaanza Machi kwa mikoa yote 26.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nitoe wito kwa TANESCO na REA kubainisha vitongoji zaidi ya 1000 na vijiji ambavyo vimepitiwa na miundombinu ya umeme mkubwa lakini hawajaunganishiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nichukue fursa hii pia kutoa wito kwa wananchi wote ambao miradi imekamilika ya Densification Awamu ya Kwanza ya Mradi wa BTIP Iringa – Shinyanga na mradi wa Makambako – Songea kulipia shilingi 27,000 na kuunganishwa umeme. Kwa sababu taarifa ambazo tunazo inaonekana wananchi wa maeneo hayo wengi bado hawajalipia na miradi ile inakaribia kukamilika. Kwa hiyo, nitoe wito walipie mapema ili kuepuka gharama wakati miradi itakapokabidhiwa TANESCO.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.