Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Janeth Maurice Massaburi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:- Kumekuwa na upungufu wa rasilimali watu katika taasisi za umma na baadhi ya watumishi kushindwa kufanya maamuzi:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ndani na nje ya nchi kwa watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo na kuleta tija kwa Taifa?
Supplementary Question 1
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa watumishi wa umma na ambayo yana mwelekeo wa kuifikisha Tanzania kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Je, Serikali imejipanga vipi kikanuni kuwa na mfumo endelevu na madhubuti wa uwajibikaji na uwajibishaji kwa awamu zote za utawala zinazofuata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni umuhimu wa kuajiri vijana waliopo kwenye private sector na wale wanaoshi nchi za nje (Diaspora) kwa kuwashirikisha pamoja ili tuweze kupata chachu ya maendeleo kwa kutumia ujuzi mbalimbali walionao?
Name
Dr. Mary Machuche Mwanjelwa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbeya Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Kuteuliwa ambaye pia ni wifi yangu Mheshimiwa Janeth Masaburi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameulizia kuhusu mfumo. Naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba sisi kama Serikali sasa hivi tumejipanga kuboresha mfumo mzuri zaidi tofauti na ule tuliokuwa nao ambao tulikuwa tunatumia LAWSON version 9 ambapo sasa hivi tuna mfumo mpya wa utumishi pamoja na mishahara. Mfumo huu unatengenezwa na vijana wetu wa Kitazania na wazalendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu wa utumishi na mishahara wenyewe utakuwa na uwezo mkubwa sana wa capture taasisi zote za umma nchini tofauti na ule ambao tunautumia sasa na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko mengi. Mfumo huo tunategemea uanze rasmi Juni, 2019 ambao utahusisha taasisi zote za umma na utaboresha hata mifumo mengine ya utendaji kazi wa mtumishi wa umma mfano OPRAS. Kwa maana hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumejipanga na mfumo huu ambao utakuwa mpya na uwezo mkubwa utaweza kuhakikisha unapata taarifa za kila mtumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amezungumzia juu ya kuajiri watumishi ambao watatoka katika taasisi binafsi. Naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali kwa wale wote ambao wanaomba ajira kwa mara ya kwanza hatuna restriction yoyote wala hatubagui na huwa tunatoa matangazo ya kazi na sasa hivi tumejiongeza zaidi tunatumia online kwa maana ya Ajira Portal. Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye anataka kuomba kazi Serikalini anakaribishwa mradi sifa, vigezo na mienendo yake na michakato inayotakiwa itafanyika. Ahsante.
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:- Kumekuwa na upungufu wa rasilimali watu katika taasisi za umma na baadhi ya watumishi kushindwa kufanya maamuzi:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ndani na nje ya nchi kwa watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo na kuleta tija kwa Taifa?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi niko Kamati ya Utawala, Mheshimiwa
Mzee Mkuchika na Waziri na Naibu Waziri wanafanya kazi na sisi vizuri nawapongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza ni kweli kwamba sasa hivi katika nchi yetu wako watumishi ambao hawatoi maamuzi kwa kisingizio maagizo kutoka juu, tumekuja hapa kwa kazi maalum, ushirikiano hafifu katika Idara mbalimbali na siku za karibuni tumesikia hata vipigo vinatokea maofisini na kadhalika. Pamoja na kazi nzuri ya Mheshimiwa Mzee Mkuchika, Waziri na Naibu wake hivi Serikali inafanya vetting kama zamani ili kupata watumishi wanaofaa au mnachukua tu kwa sababu ya ukabila, ya undugu, ya kulipana hisani kwa sababu watu kama hawa wanaaibisha Taifa hili?
Name
Dr. Mary Machuche Mwanjelwa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbeya Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la shemeji yangu Mheshimiwa Selasini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niseme tu kwamba Ofisi yangu ndiyo inayoshughulikia pia suala la maadili ya watumishi na viongozi na tumejipanga na linaendelea kufanyika vizuri. Kama tunavyoelewa sasa hivi kwamba utendaji kazi na maadili Serikalini yameongezeka kwa kiwango kikubwa. Ofisi yangu haijasita, bado tunaendelea kulipigania kuhakikisha kwamba wale wote wanaotumia madaraka yao vibaya wanachukuliwa hatua kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vetting, naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba vetting ipo na inaendelea. Ndiyo maana katika majibu yangu nilipokuwa namjibu Mheshimiwa Masaburi nilisema wananchi wote wanaruhusiwa kuomba kazi lakini utaratibu na mchakato maalum huwa unafanyika. Kwa maana hiyo, nazungumzia hili katika kusisitiza kwamba watumishi wote wa umma wanapaswa kuhakikisha wanatii, wanafuata na wanaheshimu miiko yote ya utumishi wa umma. Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, napenda kuongezea majibu ya swali la ndugu yangu Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya CCM inaajiri watumishi wa umma kwa sifa zilizotangazwa. Hatuajiri kuangalia mkoa, wala ukabila, wala dini, sisi Chama chetu kwenye mambo hayo ya ukabila na dini tumehama huko; sisi tunashughulika na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine aligusia kwamba wako watu wana kigugumizi kufanya maamuzi. Nataka nimhakikishie Serikali hii ya Awamu ya Tano inafanya maamuzi kwa wakati (promptly). Ametoa mfano, ingawa hakutaka kusema, nadhani amerudi nyumbani kwake Moshi kule, watu wamepigana ni kweli, waliohusika tayari tumewachukulia hatua, mmoja hayupo kazini na mwingine anachunguzwa. Hiyo inaonesha namna ni gani Serikali ya CCM inachukua hatua kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza suala la vetting; huo ni utaratibu wa Serikali. Huwezi ukamteua mtu kufanya kazi ya umma hasa nafasi ya uongozi bila kumfanyia vetting lakini wanaofanya vetting ni binadamu. Leo Mheshimiwa Selasini anaweza akawa Mbunge mzuri sana siku nyingine akateleza. Sasa husemi kwamba kwa kuwa alikuwa mzuri siku za nyuma aendelee tu. Ndiyo maana mnasikia tunafanya mabadiliko na tunatengua uteuzi. Kwa hiyo, nimhakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Selasini tuko pamoja. Nilidhani mwishoni utasema napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya CCM kwa hatua mlizochukua Mkoa wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.