Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Lucy Simon Magereli
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:- Tangazo la Serikali Namba 257 kifungu cha 6 kinaelekeza faini za makosa ya barabarani kulipwa kwa Askari aliyeandika faini au kwa OCD au Ofisi ya Mhasibu aliyeko karibu. GN hiyo imetoa nafasi ya kulipa ndani ya siku saba (7) na iwapo faini haitalipwa ndani ya siku saba (7) mkosaji atafikishwa Mahakamani ndani ya siku 10:- (a) Kwa nini Askari wa Usalama Barabarani huamua kushikilia magari ya wanaokamatwa wakati huohuo, wakati sheria inasema walipe ndani ya siku saba (7)? (b) Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna mashine za kielektroniki (POS) za kulipia faini na ANPR ambayo husaidia kufuatilia ambao wanakwepa kulipa faini walizoandikiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upatikanaji wa POS na ANPR ili kuepusha mifarakano na usumbufu unaojitokeza?
Supplementary Question 1
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza na nieleze masikitiko yangu kwamba swali langu nilileta mwaka 2016 lakini kwa bahati mbaya limekuja 2019. Nishukuru kwa maendeleo ambayo yamefanywa ya kusambaza hizo mashine za kielektroniki nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusambazwa mashine hizo sasa hivi Jeshi la Polisi limekuwa sehemu ya chanzo kikuu cha mapato ya Serikali na wanapangiwa viwango vya fedha za kukusanya. Kwa hiyo, uwepo wa mashine hizi pamoja na kwamba tulidhani ingekuwa ni suluhisho lakini imekuwa chanzo cha kuwabambika makosa watumia barabara ili kuzalisha mapatao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru watumia barabara kwa makosa haya ya kubambikizwa na kulazimishwa kulipa faini ili tu kufikia viwango za fedha walizokubaliana vitendo vinavyofanywa na askari wa usalama barabarani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hivi karibuni Mheshimiwa Kangi Lugola, Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani alitoa maelekezo kwamba gari linapokamatwa hata kama litakuwa na makosa zaidi ya moja basi liandikiwe kosa moja lakini hadi tunavyozungumza, magari mengi yanaandikiwa faini zaidi ya kosa moja na kutozwa faini na penalties kinyume na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri. Je, Serikali inaweza kurejea tena agizo lake kupitia Bunge letu Tukufu ili liwe maelekezo rasmi ya Serikali kwa watekeleza sharia? Ahsante.
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya kubambikiwa kesi ambayo ametuhumu Askari wa Usalama wa Barabarani, nimwambie tu kwamba yanapotokea matukio kama haya kwa baadhi ya askari wetu tunachukua hatua na hata hili agizo la Mheshimiwa Waziri lilikuwa linalenga kuziba mianya ya aina kama hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nchi ndiye mwenye dhamana ya mwisho ya Wizara hii na maagizo yake ni lazima yatekelezwe. Maagizo haya yanatekelezwa ikiwa kuna upungufu katika utekelezaji wake, kama labda kuna watu ambao hawatekelezi, hiyo taarifa hatujaipata rasmi lakini kimsingi Mheshimiwa Waziri ametoa agizo na linapaswa kutekelezwa kwa maslahi ya wananchi wa nchi yetu ambao wanatumia barabara.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved