Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
George Malima Lubeleje
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Primary Question
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:- Waheshimiwa Madiwani wana majukumu mengi ya kufanya katika kata zao; na posho wanayolipwa kwa mwezi hailingani kabisa na majukumu yao na ni ndogo sana:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza posho ya Waheshimiwa Madiwani?
Supplementary Question 1
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema kwamba halmashauri waongeze makusanyo ya mapato ya ndani (own source) na kwa kuwa Serikali ilichukua vyanzo vingi vya mapato ambavyo vilikuwa vinaipatia halmashauri mapato, sasa Serikali inasema halmashauri ziongeze makusanyo ya mapato ya ndani, hayo makusanyo ya ndani yatatoka wapi na kwa nini Serikali isiongeze ruzuku ili Madiwani waongozwe posho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Madiwani ni viongozi kama sisi Wabunge; na kwa kuwa viongozi wa kisiasa wengi wamewekwa kwenye Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa, kwa nini hawa Madiwani nao wasiwekwe kwenye sheria hii ili waweze kutambulika kisheria kwa sababu ni viongozi muhimu? Katika Uchaguzi Mkuu ni mafiga matatu, baada ya uchaguzi figa la tatu linameguka wanakuwa viongozi wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Malima Lubeleje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Mbunge anauliza kwamba kwa sababu kuna vyanzo vimechukuliwa na Serikali Kuu na kwa hiyo mapato ya halmashauri yamepungua ni kwa nini tusitoe ruzuku. Kwanza naomba ieleweke kwamba vyanzo vilivyochukuliwa ikiwemo kodi ya majengo inakusanywa na TRA kwa niaba ya Serikali nzima lakini fedha hizi zinarudishwa kwenye halmashauri kwa ujumla wake kwenda kufanyia kazi shughuli za maendeleo katika halmashauri zetu hizo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sasa hili jambo la ruzuku halijafanyiwa kazi, naomba tulipokee tulifanyie kazi, kadri uwezo utakavyoruhusu basi tutaona kama kuna uwezekano wa kupeleka ruzuku. Kwa sasa kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi ni kwamba posho za Madiwani na malipo mbalimbali zinatokana na vyanzo vya ndani na sasa tupo kwenye mchakato wa kuandaa bajeti ya 2019/2020, naomba halmashauri zetu ziangalie uwezekano wa kuongeza posho na mapato ili waweze kujilipa wenyewe kwa sababu ndipo msingi wa malipo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anazungumza habari ya sheria kuweza kuwatambua; hili ni jambo jema, lakini kwa sheria iliyopo huu ndiyo utaratibu wa kawaida, sasa kama kuna maoni mengine kama alivyopendekeza tupo tayari kuyapokea, tuyafanyie kazi na hatimaye kuyaingiza kwenye sheria ili waweze kulipwa kama watumishi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved