Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:- Michezo ni afya, furaha, burudani, undugu na pia huondoa au kupunguza uhalifu nchini. Kuwa na viwanja vyenye hadhi kama kile cha Jakaya Kikwete Youth Park huvutia vijana wengi nchini kupenda michezo:- Je, ni lini Serikali itaanza kujenga viwanja vyenye hadhi hiyo nchi nzima?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, ningependa tu niishauri Serikali pale ambapo Waheshimiwa Wabunge wanafanya mambo yanayoacha alama katika jamii watambuliwe. Uwanja wa Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park ilikuwa ni kazi nzuri iliyofanywa na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu. Mambo kama haya yakitajwa, kama Mheshimiwa Lema alivyojenga ile hospitali ya Mama na Mtoto kule Arusha, yanawatia moyo Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo wanaendelea kuhangaika kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo viwanja vingi sana vya michezo ambavyo vimevamiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Je, Wizara iko tayari kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, ili kurejesha viwanja hivi na kujenga viwanja vidogo vidogo kama huu wa Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park kwa ajili ya michezo ya watoto wetu ambao wanacheza hovyo barabarani na kuhatarisha maisha yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna viwanja vya mpira wa miguu hapa nchini, ambavyo kwa kweli ni vibovu. Hivi karibuni timu ya Yanga ilicheza kwenye uwanja fulani, sitaki niuseme na ilipata shida sana kwa kweli, yaani unaona hata wanavyopasiana wanavyopiga chenga na nini inaathiri matokeo. Sasa kwa nini viwanja kama hivi visifungwe ile michezo ya ligi TFF ikahamishia kwenye viwanja vya karibu ili kutoa nafasi viwanja kwa hivyo kukarabatiwa?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa maswali yake mazuri ambayo ameyauliza, lakini niseme kwamba ushauri ambao ameutoa tumeupokea na tutaendelea kuufanyia kazi. Nikianza na swali lake la kwanza ambalo amezungumzia viwanja kuvamiwa. Nikiri kwamba ni kweli kuna tatizo kubwa sana la viwanja kuvamiwa nchini Tanzania na hata juzi ambapo nilikuwa Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kibondo nilikuta kwamba kuna kiwanja kizuri kabisa cha mpira lakini kimevamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho naweza kusema ni kwamba, changamoto kubwa ambayo inasababisha viwanja hivi kuweza kuvamiwa ni kwa sababu kwanza viwanja vinakua havina Hati Miliki, hilo la kwanza, lakini unakuta viwanja vipo lakini havijazungushiwa wigo. Kwa hiyo nitumie nafasi hii kuweza kutoa wito kwa wamiliki wa hivyo viwanja, iwe ni Halmashauri, kampuni za watu binafsi au vyama vya kisiasa kuhakikisha kwamba cha kwanza, wanavitafutia Hati hivyo viwanja lakini jambo la pili waweze kuzungushia wigo hivyo viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake pili ameuliza kuhusu ubovu wa viwanja na ameshauri kwamba kwa nini hivyo viwanja visifungwe ili ukarabati uweze kufanyika. Niseme kwamba ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tumeupokea, lakini kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba suala la ukarabati wa viwanja si suala la Serikali peke yake, ni suala la Serikali lakini kushirikiana na wadau wote ambao wanamiliki viwanja hivyo. Kwa hiyo nitumie fursa hii pia kwa wadau wote ambao wanamiliki hivyo viwanja kuhakikisha kwamba wanatenga fedha, lakini vilevile wanashirikiriana na TFF kuhakikisha kwamba hivyo viwanja vinaweza kukarabatiwa ili basi wanamichezo wetu waweze kucheza michezo vizuri.

Name

Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:- Michezo ni afya, furaha, burudani, undugu na pia huondoa au kupunguza uhalifu nchini. Kuwa na viwanja vyenye hadhi kama kile cha Jakaya Kikwete Youth Park huvutia vijana wengi nchini kupenda michezo:- Je, ni lini Serikali itaanza kujenga viwanja vyenye hadhi hiyo nchi nzima?

Supplementary Question 2

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kuhusu viwanja, pamoja na kwamba hata viwanja vitakavyofanyika michezo ya AFCON naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa jana tumehakikishiwa kwamba timu yetu itakayoshiriki michezo ya AFCON itashinda nataka kujua tu wamefanya maandalizi gani, watuambie maandalizi yaliyofanyika ili tuwe na uhakika kwamba timu yetu sasa tunaenda kubakiza kombe hapa Tanzania?

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyonyeza la Mheshimiwa Mwamoto kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana, lakini vilevile naomba nirejee kauli ya Waziri Mkuu ya jana, kwamba tumejipanga vizuri. Timu yetu ya Taifa ya Vijana Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) iko kambini kwa wiki tatu sasa na kazi yetu kubwa sasa hivi ni kuipambanisha na timu mbalimbali za wakubwa wao hasa wa chini ya umri wa miaka 20, kuweza kuwaimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kulikuwa na mechi kubwa sana na timu nzuri katika Afrika Mashariki Azam FC under 20 na matokeo yake ni kwamba Serengeti Boys imewachapa kaka zao magoli matano kwa bila. Tukumbuke vilevile kwamba Azam FC ina baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho timu ya Serengeti inakwenda Arusha angalau kuji-acclimatize (kujizoesha) na hali ya Arusha na kuweza kupambana na timu mbalimbali kabla ya kwenda Uturuki kwa mwaliko wa UEFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tujivunie ubora wa timu yetu, kwamba imeweza kutambuliwa kama moja ya timu bora katika Afrika kuitwa kwenye mashindano ambayo yanaunganisha timu nne za Afrika na timu nne za Ulaya. Tunakwenda kule na mechi yetu ya kwanza itakuwa tarehe 4 mwezi wa tatu dhidi ya Guinea; na baadaye tutacheza na Australia na kumalizia na timu yka Uturuki. Sasa hivi naongea na wenzetu wa TBC tuweze kupata live coverage kutoka huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashindano hayo yataisha tarehe 11 Machi na timu hiyo haitarudi Tanzania, tunaitafutia pesa lazima iende Spain ikafanye mazoezi na mashindano kidogo na wenzao na baadaye iende Cameroon ikashindane na baadhi ya timu kule ndipo itarejea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, wiki ya kwanza mwezi wa Aprili tumekaribishwa na Rwanda kujipima nguvu na timu nne bora za Afrika ambazo ni Cameroon, Rwanda na Uganda. Baada ya hapo inarejea nchini kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya Nigeria ambayo nina uhakika tutaishangaza Afrika katika matokeo yake. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:- Michezo ni afya, furaha, burudani, undugu na pia huondoa au kupunguza uhalifu nchini. Kuwa na viwanja vyenye hadhi kama kile cha Jakaya Kikwete Youth Park huvutia vijana wengi nchini kupenda michezo:- Je, ni lini Serikali itaanza kujenga viwanja vyenye hadhi hiyo nchi nzima?

Supplementary Question 3

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nami nianze tu kwanza kwa kuishukuru Wizara kwa kuendelea na jitihada za kuboresha na kuimarisha Uwanja wa Nyamagana. Sasa kwa sababu tunaamini kwamba ili tuwe na vijana wengi ambao wanacheza mpira vizuri ni lazima tuwe na viwanja vingi kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Jiji la Mwanza tuna Milongo Sports Center ina viwanja takribani vitano kwa wakati mmoja. Ningependa sasa kumwomba Mheshimiwa Waziri apate nafasi aje atembelee viwanja hivi na tuone namna ya kuviboresha ili kupata vijana wengi zaidi; je, yuko tayari kufanya hivyo tukimaliza Bunge hili?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mabula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza Wabunge wote wa Jiji la Mwanza kwa jitihada kubwa sana na nzuri ambazo wanafanya katika kuboresha viwanja vyetu. Vilevile niseme kwamba ni juzi tu nilikuwa Wilaya ya Nyamagana na nikatembelea ule Uwanja wa Nyamagana ambao umekarabatiwa kwa jitihada za Halmashauri, Waheshimiwa Wabunge, pamoja na wadau. Niseme kwamba ombi lako nimelipokea na nitafika tena kwenye Jiji la Mwanza ili kuweza kuangalia namna gani ambavyo tutashirikiana pamoja. Ahsante.

Name

Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:- Michezo ni afya, furaha, burudani, undugu na pia huondoa au kupunguza uhalifu nchini. Kuwa na viwanja vyenye hadhi kama kile cha Jakaya Kikwete Youth Park huvutia vijana wengi nchini kupenda michezo:- Je, ni lini Serikali itaanza kujenga viwanja vyenye hadhi hiyo nchi nzima?

Supplementary Question 4

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wametupa upendeleo Jiji la Tanga kutaka kutujengea Uwanja wa kisasa, lakini cha kushangaza eneo lile halijazungushiwa uzio na watu wameshaanza kulivamia, sasa Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, je, ni lini harakati angalau za kuanza maandalizi na kujenga uzio katika lile eneo ili lisivamiwe utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Jiji la Tanga ni eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya kujenga uwanja changamani wa michezo kwa fedha ambazo tunategemea zitatoka FIFA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba as soon as fedha hizo zitakuwa zimefika, ujenzi wa uwanja huo utaanza. Kwa hiyo, nimtoe shaka kwamba, ujenzi utaanza mapema sana mara tu fedha zitakapokuwa zimefika. Ahsante.