Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Primary Question
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:- Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:- Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 1
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kueleza masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo wataalam wetu wanawapotosha Mawaziri wetu. Eneo tunalolizungumzia ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji inayogusa vijiji vitatu katika Kata ya Mwakijembe yenye ukubwa wa takribani hekta 450 na tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kuendeleza skimu hii. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba sehemu tunayoizungumzia ilikuwa ni shamba darasa isipokuwa ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lililochukuliwa siyo hekari moja kama inavyozungumziwa bali ni takribani hekari 50, watu takribani 28 wamekumbwa na kadhia hii. Kwa sababu Waziri amepotoshwa, je, yupo tayari kuja kujionea yeye mwenyewe kule Mkinga ili wananchi hao watendewe haki?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili nimekuwa nikilizungumza mara kwa mara hasa kwenye michango yangu ya maandishi nimekuwa nikitoa na takwimu ya uonevu huu na mara ya mwisho nilisema ni watu 14 na hii ilikuwa mwaka jana sasa imeongezeka wamekuwa watu 28 na sasa ni hekari karibu 50 zimechukuliwa. Je, Waziri yuko tayari kutoa tamko hapa la zuio kwamba kikosi kile kilichopo kule kiache tabia hii ya kuchukua ardhi ya wananchi bila ridhaa ya kijiji?
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa takwimu zilizopo katika Wizara yangu na zile anazotoa Mheshimiwa Mbunge zinapishana, nadhani ni busara tukafanya kile alichoomba kifanyike nacho ni mimi kufanya ziara katika eneo hilo ili kukagua kwa pamoja kati ya upande wetu sisi kama Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tukifuatana na wataalam wa Jeshi pamoja na watu wa Wilaya na Kijiji husika ili tuthibitishe ukubwa wa eneo lililochukuliwa na nani anayewajibika kulipa fidia. Endapo itathibitika kwamba Serikali kwa upande wetu Wizara ya Ulinzi inalazimika kulipa fidia basi tutafanya hivyo.
Name
Abdallah Majurah Bulembo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Primary Question
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:- Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:- Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 2
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi sitaki kukuuliza maswali kila siku lakini naomba swali hili utoe tamko. Wananchi wa Makoko katika Manispaa ya Musoma wanadai fidia mwaka wa 13, swali hili nimeshaliuliza humu, Katibu Mkuu amewapelekea barua ya kuwapa subira. Watu wamekufa, wamerithi, wameacha maeneo yao; miaka 13 Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naomba utoe tamko hapa Bungeni watu hawa watalipwa lini.
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alhaj Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi lipo katika maeneo mengi. Kila mwaka wakati tunawasilisha bajeti yetu nimekuwa nikisema kwamba fedha zikitengwa tutalipa fidia. Kwa bahati mbaya fedha zinazotengwa au zinazotolewa hazikidhi kulipa watu wote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha tunaoumalizia tumelipa fidia eneo la Kilwa kwa ajili ya Navy Base kuwepo pale lakini bado tunatarajia Wizara ya Fedha itatupatia fedha kabla ya mwisho wa mwaka huu wa bajeti ili tuendelee kulipa fidia hizo. Tunatambua kwamba eneo la Makoko linastahili kulipwa fidia pamoja na maeneo mengine kadhaa na tutafanya hivyo kadri fedha zinapopatikana.
Name
Charles John Mwijage
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Primary Question
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:- Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:- Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 3
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nichukue fursa hii kumuuliza swali dogo Mheshimiwa Waziri wa Jeshi la Ulinzi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo la Jeshi la Kambi ya Kaboya katika Vijiji vya Mayondwe na Bugasha uhakiki ulishafanyika na kwa sababu wakati wowote Waziri anategemea kupata pesa kutoka Wizara ya Fedha, anaweza kuwahakikishia wananchi hao kwamba baada ya kulipa Kilwa sasa ni zamu ya Kaboya kabla ya mwezi Juni?
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwijage, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali ni maeneo mengi ambayo tunastahili kulipa fidia na baadhi uhakiki umeshafanyika kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge. Natambua kwamba eneo la Kaboya linastahili fidia na uhakiki umekamilika tunachosubiri ni fedha. Kwa maana hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zilizotengwa katika bajeti endapo zitapatikana kabla ya mwisho wa mwaka huu basi Kaboya nayo tutaijumuisha katika maeneo yatakayolipwa fidia.
Name
Joseph Leonard Haule
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:- Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:- Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 4
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu sana nimekuwa nikizungumzia suala la mgogoro kati ya Wanajeshi pale Mikumi na Kitongoji cha Vikweme ambao walihamishwa kwenye Hifadhi ya Mikumi mbugani kwenda kule kwenye Vitongoji vya Vikweme tangu mwaka 1963 lakini Jeshi wamevamia eneo hilo na kuwaondoa wananchi wale kwa maumivu makali sana. Kwa kuwa suala hili nimeliongea mara nyingi, je, Waziri yupo tayari baada ya Bunge hili tuweze kuongozana ili aweze kuwasikiliza wananchi wa Jimbo la Mikumi pale Vikweme ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu na hasa ikizingatiwa kwamba wananchi wengi wa Mikumi tunategemea Kitongoji hiki kufanya shughuli zetu za kilimo na kujiletea maendeleo.
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumewahi kuzungumzia suala hili na kama nilivyosema awali maeneo mengi yana migogoro kati ya Jeshi na wananchi kuhusiana na masuala ya ardhi. Mimi nipo tayari kufanya hiyo ziara kama anavyoshauri Mheshimiwa Mbunge ili tukaangalie ni nani hasa mwenye haki katika eneo hilo na endapo itathibitika kwamba Jeshi linalazimika kulipa fidia kama nilivyosema, tutafanya hivyo.
Name
Freeman Aikaeli Mbowe
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:- Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:- Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 5
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Majeshi yetu na hususan Jeshi la Wananchi ndicho chombo ambacho tunakiamini sana kwamba kina wajibu wa kulinda mipaka yetu na usalama wa raia na nchi yetu katika ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni katika mpaka wa Namanga tulishuhudia kupitia vyombo vya habari vurugu kubwa zilizofanywa upande wa Kenya ambapo magari, abiria na mizigo kutoka Tanzania yakiwemo magari yalizuiliwa na wananchi wa Kenya na kusababisha vurugu kubwa katika mpaka ule. Mheshimiwa Waziri anatupa tamko gani kama Waziri wa Ulinzi kuhusu usalama wa nchi yetu katika mpaka ule na nini kilipelekea tukio lile likafanyika likasababisha vurugu zile?
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Freeman Mbowe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Jeshi la Ulinzi lina wajibu wa ulinzi wa mipaka lakini Vyombo hivi vya Ulinzi na Usalama vina majukumu tofauti. Suala la usalama wa raia ni suala la Polisi na kuna vyombo vingine vingi vya ulinzi na usalama ambavyo vina majukumu ya kulinda usalama katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nachoweza kusema ni kwamba mpaka wetu kati ya Tanzania na Kenya kwa upande huo hauna tatizo lolote. Ulinzi upo pale wa kutosha na hizi vurugu zilizotokea nadhani lilikuwa ni jukumu la vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba wanalishughulikia. Taarifa nilizonazo ni kwamba suala hili limeshughulikiwa na lilimalizwa. Kwa maana hiyo hatutarajii matukio kama haya yaendelee kutokea.