Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYNABU M. VULU (Kn.y. MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:- Ukarabati wa Kituo cha Afya Mbwera yakiwemo majengo ya upasuaji, Wodi ya Wazazi na mengineyo unakwenda kwa kasi sana:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme kwenye Kituo cha Afya Mbwera? (b) Je, ni lini kazi hiyo itaanza?

Supplementary Question 1

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mheshimiwa Ally Seif Ungando na wananchi wa Kibiti, napenda kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa juhudi ilizofanya, lakini pamoja na hayo, nina maswali mawili. Kwa kuwa umeme umeshafikia hatua hiyo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameielezea, ningependa kujua ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye maeneo ya Nyatanga, Kingwira, Zimbwini, Runyozi na Makaoni?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali iliahidi kaya 90 katika eneo la Kitembo na katika kaya hizo 90, kaya 40 bado hazijapata umeme, ningependa kujua Serikali imejipangaje katika hilo? Ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Zainab Vullu, Mbunge mwenzangu wa Viti Maalum wa Mkoa wa Pwani.

Katika maswali yake mawili ya nyongeza, amepongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge Ally Seif Ungando na mimi nimepokea kwa niaba ya Wizara, kwa kazi ambayo inaendelea katika maeneo ya Wilaya ya Kibiti na katika maeneo mbalimbali, lakini ameulizia maeneo ya Nyatanga, Zimbwini, yatapata lini umeme. Nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge mama Vullu kwamba katika REA III mzunguko wa pili unaoendelea, maeneo haya yameingizwa katika orodha na kazi inatarajiwa kuanza 2019 mwezi wa Saba. Nalitarajia Bunge hili wakati wa kuwasilisha Bajeti yetu ituunge mkono ili kazi ya kumaliza vijiji ambavyo vimesalia katika mradi wa REA III mzunguko wa kwanza viweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameelezea eneo la Kitembo nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na kumshukuru kwa sababu ni moja ya maeneo ambayo tunayatembelea kwenye ziara mimi pamoja na yeye Kitembo tumewasha umeme kama anavyosema, tumeshawaunganishia kaya 50, hizi kaya 40 kwa sababu mradi unakuwa na wigo wa wateja wa awali. Mradi unakuwa na kazi za awali, kaya zinazobaki TANESCO inaendelea na kazi yake ya kusambaza umeme. Kwa hiyo, naomba nielekeze TANESCO kuzingatia kwamba mradi unapokamilika na kukabidhiwa waendelee kuwasambazia umeme wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inaongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya uamuzi wa kisera, kwamba kwa sasa umeme utakaosambazwa na TANESCO, REA na wadau wowote, bei ya kuunganisha ni shilingi 27,000/=. Kwa hiyo hakuna kikwazo kingine kwamba kutakuwa na bei nyingine pengine shilingi 177,000/=, bei ni moja shilingi 27,000/=; kwa hiyo TANESCO waendelee na kazi ya kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ambao mradi wa REA umekamilika. Ahsante.

Name

Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Primary Question

MHE. ZAYNABU M. VULU (Kn.y. MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:- Ukarabati wa Kituo cha Afya Mbwera yakiwemo majengo ya upasuaji, Wodi ya Wazazi na mengineyo unakwenda kwa kasi sana:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme kwenye Kituo cha Afya Mbwera? (b) Je, ni lini kazi hiyo itaanza?

Supplementary Question 2

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwenye Kata ya Kolo, Jimbo la Kondoa Mjini tulipata ufadhili mkubwa sana wa wenzetu wa MKAJI kwa ajili ya kukarabati Zahanati kwa lengo la afya ya mama na mtoto, na waliweka lengo kubwa sana mkazo mkubwa kwenye huduma ya maji, kimekarabatiwa kisima kirefu, kimemalizika sasa hivi takriban miezi mitatu. Kinachokwamisha ni supply ya umeme pale ili huduma hiyo iweze kuanza kutumika. Tumewaomba TANESCO Wilaya, TANESCO Mkoa mpaka sasa hivi bado tunasubiria. Je, ni lini sasa wenzetu wa TANESCO watatuletea ule umeme ili zoezi zima la wenzetu wa MKAJI lianze kuleta tija?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kwamba hili swali lake ni zuri linahitaji utekelezaji, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi cha maswali na majibu na ratiba ya Bunge tukutane na pia nitafanya ziara maalum na wataalam wa TANESCO katika maeneo hayo ili kuhakikisha kisima hiki kinapata huduma hii ili dhamira iliyotarajiwa kwa ujenzi wa zahanati na ukarabati hiyo iweze kufikiwa, ili iweze kupata maji na huduma iweze kutolewa. Ahsante.