Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Katika kipindi cha hivi karibuni wananchi wamekuwa wakilalamikia mzunguko wa fedha kuwa mdogo:- Je, hali hiyo imesababishwa na nani?
Supplementary Question 1
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, bado nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya mwezi Februari, 2019 kwa maana ya Monthly Economic Review, inaonyesha kwamba kasi ya ukuaji ya ujazo wa fedha imeshuka kutoka asilimia 7.5 mwaka 2018 mpaka asilimia 3.3 mwaka 2019.
Je, Serikali haioni kuwa utekelezaji wa Sera ya Fedha umeleta matokeo tofauti kwa ukuaji wa ujazo wa fedha kuanguka zaidi kuliko mwaka 2018?
Swali la pili; kasi ya ukuaji ya mzunguko wa fedha nchini ni moja ya kiashiria muhimu sana cha kasi ya ukuaji wa uchumi; na ushahidi unaonyesha kwa miaka 20 kwamba unapokuwa na kasi ya ukuaji wa uchumi ya 7% maana yake kasi ya mzunguko wa fedha unakuwa katika double digit kati ya asilimia 12 mpaka 15. Kwa kutumia kiashiria cha mzunguko wa fedha na mfumuko wa bei, kwa nini Serikali isiache kutoa taarifa za uongo humu ndani ya Bunge na kwa Umma kwamba uchumi unakua kwa 7% ilhali hali halisi ni chini ya 4%.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nianze na swali lake la pili kwa sababu ameisingizia Serikali, ni kwamba Serikali siku zote inasema ukweli na haijawahi kudanganya Bunge, wala kudanganya sehemu yoyote. Nayasema haya kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) uliomalizika wiki mbili zilizopita, Tanzania imepongezwa kwa ukuaji wa uchumi mzuri kwa mfululizo wa miaka mitano. Kwa hiyo, siyo kwamba Serikali inayasema haya ndani ya Bunge peke yake, hapana. Serikali inayasema haya ndani ya Bunge, nje ya Bunge na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kwa taarifa yake limeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ukuaji mzuri wa uchumi kwa kuweka nyenzo nzuri zinazohakikisha ukuaji wa uchumi wetu kuwa imara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tusiwadanganye Watanzania, uchumi wa Tanzania uko imara. Kwa Afrika Mashariki sisi ni wa kwanza na kwa Afrika sisi hilo ni jambo la kawaida. Nendeni kwenye google, m-google halafu mtajua nini tunachokisema. Uchumi wetu uko imara.
Mheshimiwa Spika, uchumi wetu uko imara na tuna uhakika kama ambavyo prediction zetu zilionyesha. Kwa mwaka 2018 tutakua kwa asilimia 7.2 kama prediction zetu zilivyoonyesha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, ni sahihi kabisa alichokisema kwamba ujazi wa fedha ukilinganisha mwaka 2018 na mwaka 2019 taarifa iliyotelewa na Benki Kuu, ujazi wa fedha umepungua. Hiyo haimaanishi kwamba uchumi haufanyi vizuri. Unaposoma ile taarifa, soma na sababu, kwa nini ujazi wa fedha umepungua?
Mheshimiwa Spika, ujazi wa fedha umepungua kwa sababu Watanzania sasa hata hapa ndani tukijaribu kuchukua simu ya kila mmoja wetu, ndani ya kila simu ya mmoja wetu kuna fedha za kutosha ndani ya simu yake na anafanya transaction electronically kwa siku zaidi ya jinsi ambavyo anafanya cash transaction kwa fedha taslimu halisi.
Kwa hiyo, kunapokuwa na ongezeko la transaction electronically, fedha halisi sokoni zinapungua, lakini fedha zilizopo kwenye mzunguko zipo za kutosha. Kama nilivyosema, sera yetu ya fedha inahakikisha mzunguko wetu wa fedha unalingana na shughuli za kiuchumi ambazo zinaendelea ndani ya Taifa letu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved