Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Christopher Kajoro Chizza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Primary Question
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:- Katika Wilaya ya Kakonko kuna wachimbaji wadogo wa madini aina ya dhahabu katika Vijiji vya Myamwilonge, Nyakayenzi, Ruhuru na kuna dalili za kuwepo madini hayo katika sehemu nyingine. Aidha, kuna madini ya chokaa katika Milima ya Nkongogwa ambayo yana matumizi mengine ya viwandani:- Je, Serikali imejipangaje kufanya utafiti wa uwepo wa madini na kuwasaidia wachimbaji ili wayachimbe na kujipatia kipato?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu yanaleta matumaini. Nina swali moja tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge lililopita aliniahidi yeye mwenyewe jua linawaka kwamba angefuatana na mimi kwenda kuwasaidia wananchi hawa ambao tayari wameanza kuchimba madini haya, lakini bahati mbaya mambo yakawa mengi.
Sasa kwa kuwa wananchi hawa wameanza kuchimba madini kwa kutumia nyenzo duni, utaalam duni na wakati mwingine hata hawajui uzito wala purity ya madini; je, sasa anawaahidi nini wananchi hawa ambao wameanza kuchimba madini ili waweze kutumia sasa fursa hii na fursa za masoko ya madini ambayo yamefunguliwa kama lile la Geita ambalo amezindua Waziri Mkuu juzi, anawaahidi nini hasa katika uwezeshaji waweze kufanya shughuli hii kwa ufanisi zaidi?
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Chiza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na yeye kwamba nilimuahidi kweli nitakwenda Kigoma, hasa maeneo ya jimbo lake. Mimi tu nipende kusema kwamba nitashiriki naye, nitakwenda, tutakwenda hadi kwa wachimbaji, tutakwenda kufanya kazi na tutakwenda kuwaelimisha na kuwapa maelekezo ya Serikali yanavyostahili. Kwa hiyo kwa hilo mimi sina tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala la wachimbaji wadogo. Kweli tuna matatizo makubwa sana ya kimitaji, teknolojia, maeneo, tafiti kwa wachimbaji wadogowadogo. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga vizuri na tumeamua sasa hivi kupitia Geological Survey of Tanzania pamoja na STAMICO tutaendelea kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitawasaidia wachimbaji wadogowadogo ili tuweze kuwapa yale maeneo ambayo tukiwapa tunakuwa na uhakika kwamba wataweza kupata madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza STAMICO tayari tumekwisha kununua rig machine ambayo inaweza kufanya kazi ya drilling kwa wachimbaji wadogo kwa gharama ndogo. Kwa hiyo tunawaomba wachimbaji wadogowadogo waje waombe maombi yao katika Wizara yetu tuwafanyie tafiti mbalimbali kwa gharama ndogo kwa sababu kufanya tafiti ni gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunaendelea kutoa elimu ya uchimbaji, uchenjuaji, na uwepo wa masoko haya ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelifungua kule Geita na lingine juzi nimekwenda kufungua pale Kahama na maeneo mengine, tunaendelea na mikoa yote ambayo inakwenda kufungua masoko ya madini. Tunakwenda kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata ile tija ambayo wanadhamiria kuipata tofauti na sasa hivi walikuwa wanakwenda kuuza katika masoko ya pembeni wanadhulumiwa, wanauza kwa bei ndogo, vilevile wanaibiwa. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo kwa kuhakikisha kwamba wanapata tija. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved