Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini yamekuwa na athari kubwa kwenye uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa miji yetu:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondoa matumizi ya plastiki hapa nchini?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA HAMIS SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa Bungeni leo, hayaoneshi dhamira ya dhati kupiga marufuku mifuko ya plastiki hapa nchini. Ukiangalia majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, inadhamiria siku zijazo, siyo kesho wala mwakani, hatujui. Hivi tunavyoongea, kwenye masoko yetu wajasiriamali wengi wanauza mifuko mizuri, mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira, mifuko ambayo ni vikapu vya ukili na mifuko mingine ambayo inaweza kutumika isiharibu mazingira. Mifuko hiyo haina masoko, hainunuliwi kwa sababu mifuko ya plastiki inatolewa bure masokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kwamba tatizo siyo kukosekana kwa mfuko mbadala, tatizo ni Serikali kuendelea kulinda viwanda vinavyotengeneza mifuko hii inayoharibu mazingira?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hakuna Mtanzania yeyote au mdau yeyote asiyejua madhara ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Serikali hioni kuendelea na makongamano, sijui na vikao vya wadau ni kupoteza muda na gharama na Serikali sasa ichukue hatua za haraka kupiga marufuku mifuko hii hapa nchini kama ambavyo wenzetu wamefanya, Zanzibar wameweza, Rwanda wameweza, Kenya wameweza, maeneo mengine yote wameweza. Sisi tatizo nini? Naomba majibu ya uhakika.

Name

January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana sana Mheshimiwa Sakaya kwa kuongea kwa uchungu kabisa na kuonesha ni mwanamazingira kabisa fasaha. Naomba nimhakikishie kwamba, katika hotuba yetu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo itakuja tarehe 16 kwa mujibu wa ratiba ya mwezi huu, tunaweza kutangaza hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu wiki hii mimi nimeelekezwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kasim Majaliwa Majaliwa, nikutane na Taasisi za Serikali zinazohusika na jambo hili, NEMC, TBS, TRA, Uhamiaji, Polisi na Customs ili kuweka utaratibu wa namna tunavyoweza kupiga marufuku. Hapa nilipo, tayari ninazo kanuni nimeshazitengeneza ambazo zinangoja kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali. Kwa hiyo, kama tutakubaliana katika vikao vya wiki hii na vinayokuja, basi tarehe Mosi, Julai, inawezekana kabisa ikawa ndiyo mwisho wa matumizi ya plastiki hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali inalichukulia kwa uzito na tunalifanyia kazi. Ni kweli kabisa tumeongea na wadau wote, hakuna sababu yoyote ya kuendelea kutumia plastiki hapa nchini. Mimi kama Waziri wa Mazingira nakubali hilo. Mbadala upo na inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tukubaliane kwamba tutakapopiga marufuku, basi tuwe tumejiandaa kufanikiwa. Kwa sababu zipo nchi ambazo zimeamua kuchukua hatua hii, lakini hazikujipanga kwenye kufanya lile zoezi; mkajikuta kwamba mmetoa tangazo tu, lakini kitaasisi hamjajipanga, kiuratibu hamjajipanga, kwa hiyo, inakuwa ni bure tu. Kwa hiyo, tunataka tukitangaza tulifanye zoezi hili kwa namna ambayo tutafanikiwa. Tunaamini kabisa kwamba hatua hii itaibua ajira nyingine nyingi zaidi kuliko hata zile zilizopo kwenye mifuko ya plastiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuko pamoja kwenye hili.