Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Primary Question

MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:- Serikali iliahidi kumaliza migogoro ya ardhi kwa kupima maeneo ya wananchi mapema ili kuepuka bomoa bomoa bila fidia:- Je, ni lini jambo hilo litafikia mwisho?

Supplementary Question 1

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Waziri ambayo kimsingi hayajaonesha kutatua migogoro ya ardhi katika Taifa hili, swali la kwanza; migogoro hii imekuwa ni mingi katika mikoa, hususan Mikoa ya Dar es Salaam, Katavi, Mwanza na maeneo mengine. Cha kushangaza, majibu haya ya Serikali yanasema kwamba wametenga shilingi bilioni nne. Lengo hapa ni kutatua, kwamba wanapokuwa wanawaondoa wananchi kwenye maeneo yao, kwa sababu Serikali ndiyo inakuwa imefanya uzembe kuwashirikisha wananchi moja kwa moja kuwaondoa katika maeneo yao lakini pia katika suala la kuwalipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kata ambazo zimeathirika katika Manispaa ya Mpanda ni Kata ya Misunkumilo ambayo iliondolewa na Jeshi, Kata ya Shanwe ambayo ilipisha ujenzi wa barabara lakini pia Kata ya Uwanja wa Ndege ambayo kulikuwa na ujenzi wa Chuo cha Kilimo. Sasa wananchi hawa wanapata shida na hawaelewi hatma yao ya kulipwa fidia zao. Sasa Serikali imepanga nini ii kulipa wananchi hao?

swali la pili ni suala la upimaji shirikishi. Serikali imekuwa ikitoa vifaa kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, lakini hakuna ushirikishwaji wa moja kwa moja kwa wananchi kwa maana ya kwamba wanapima maeneo yao lakini kwa wananchi ambao wanakuwa hawana pesa ya kulipia viwanja, angalau basi Serikali ione namna ya kuweza kuchukua; kwa mfano, kama mwananchi ana viwanja vitatu au vine, basi anapimiwa eneo lake na anapewa hatimiliki ili baadaye aweze kulipa hiyo fedha au achukuliwe baadhi ya viwanja ili kukamilisha mchakato wa ulipaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimfahamishe Mheshimiwa Rhoda kwamba Serikali imeshachukua hatua za dhati kuhakikisha ya kwamba migogoro yote ya ardhi iliyoko kati ya wananchi na Taasisi mbalimbali ikiwemo Jeshi na wengineo inafikia ukomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameunda Tume ambayo ina Mawaziri wanane, ambao wamepitia maeneo karibu ya mikoa yote na kuweza kupitia maeneo yenye migogoro ili waweze kumshauri Mheshimiwa Rais nini kifanyike katika maeneo hasa ambayo yamekuwa na migogoro mingi. Kwa hiyo, kama kuna eneo lake ambalo pia lina mgogoro na Wanajeshi, nadhani hilo linachukuliwa hatua na baada ya muda siyo mrefu, basi Serikali itatoa maelekezo nini kifanyike katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika suala la kusema kwamba unamwachia mwananchi eneo lake, nadhani Halmashauri nyingi; nimepita katika mikoa zaidi ya 18 na nikatoa maelekezo na nilikuta wengine wameshaanza kufanya kazi yao vizuri. Mfano mzuri ni Halmashauri ya Kalambo ambao walikuta kwamba tayari wana makubaliano na wananchi, wanamwachia asilimia 60 na wao wanachukua 40; na ile asilimia wanammilikisha yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo kwa wananchi wetu, hata ungempa yote, hawezi kuilipia yote. Tumewaelekeza ya kwamba lazima ifanyike kama walivyokubaliana na ukishaipima ile ardhi inakuwa imeshaongezewa thamani. Kwa hiyo, hata kama atauza, yeye mwenyewe hawezi kumiliki, tayari umeshaongeza thamani na iko katika mpango ambao ni wa kimipango miji, kwa hiyo, haiwezi tena kuwa na ujenzi holela.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba tu Halmashauri zisimamie mambo haya kwa sababu ziko Halmashauri nyingi ambazo zinafanya wakiwemo Chemba na wengineo ambako tumepita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasisitiza Mheshimiwa Mbunge afuatilie kwenye Halmashairi yake ambayo ni Mamlaka ya Upangaji. Alichosema kwamba Serikali imetoa shilingi milioni nne, siyo shilingi milioni nne, ni shilingi 6,400,000,000/= ambazo zimekwenda kwenye hizo Halmashauri nilizotaja. Tuna imani wakizitumia vizuri wakapanga miji yao, suala la ujenzi holela halitakuwepo.