Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Anthony Calist Komu
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. ANTONY C. KOMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya mara kwa mara ya kuyapima upya mashamba yaliyotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha ambayo hivi sasa yamebadilishwa matumizi na kujengwa Shule, Zahanati, Hospitali, Makazi na kadhalika?
Supplementary Question 1
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna hiyo haja ya kupima upya hayo mashamba yaliyotaifishwa na kwamba jukumu hilo lipo kwenye Halmashauri, lakini kama inavyofahamika, sasa hivi Halmashauri nyingi nchini zina hali mbaya sana ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini.
Je, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa namna ya upendeleo, kama tutatenga fedha kwenye Halmashauri kwa ajili ya kuharakisha huo upimaji? Kwa sababu tatizo kule ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika hayo mashamba yaliyotaifishwa, yapo mashamba ambayo yamegawanywa kabisa kwa ujumla na matumizi yakabadilika, kwa hiyo, wamiliki ni wapya kabisa. Sasa kila wakijaribu kuomba kupimiwa upya inakuwa ni tatizo kwa sababu zile hati za awali hazijafutwa. Mfano hai ni shamba moja kule Uru lililokuwa chini ya Chama cha Msingi Uru Kati, shamba linaloitwa Kosata. Mfano Shule ya Sekondari ya Uru Seminari imeshaomba kwa zaidi ya miaka kumi kupimiwa lakini hati ile haijafutwa.
Je, Serikali itafuta lini hizo hati za mashamba ya aina hiyo?
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza kama Wizara ni lini itaweza kusaidia Halmashauri ambazo pengine zipo duni kiuchumi kwa ajili ya kuweza kuongeza kasi ya upimaji. Naomba niseme, jana wakati najibu swali moja hapa nadhani la Mheshimiwa Joyce, nilitoa kwa ufafanuzi mkubwa sana kwamba pamoja na kwamba mamlaka za upangaji miji ni Halmashauri zenyewe, lakini wizara imeweka juhudi kubwa kuhakikisha kwamba inazipa support kubwa ya kuwawezesha kuweza kupima maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi kubwa ya kwanza ambayo tulifanya ni kuweka vifaa vya upimaji katika kanda zote na vifaa vile vinatolewa bure katika Halmashauri na inasaidia katika kupima kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tulitoa pesa, shilingi bilioni 6.4 na nimesema jana, katika Halmashauri 25 ambazo tunawasaidia kwa ajili ya upimaji, wamechukua zile pesa ili kuweza kuongeza kasi ya upimaji. Kwa hiyo, Halmashauri yake kama nayo ni mhitaji, nadhani tutaangalia uwezekano kwa kipindi kinachokuja tuweze kuona ni jinsi gani tutawawezesha ili waweze kupima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Halmashauri zote wanatakiwa kutenga bajeti kwenye bajeti zao kwa ajili ya kuongeza kasi ya upimaji kwenye maeneo yao ili kupunguza migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ameongelea suala la shamba lile la ushirika ambalo kuna maeneo yamegawiwa kwa taasisi nyingine kwa mfano Jimbo Katoliki la Moshi wamepewa eneo hilo, Uru Seminari ambayo ameisema wamepewa eneo hilo lakini hawajaweza kumilikishwa kwa sababu nyaraka zinasemekana kwenye kile Chama cha Ushirika zimepotea. Mwezi Februari mwaka 2019 wametoa taarifa rasmi Polisi kuonyesha kwamba zimepotea. Sasa huwezi kumilikisha mtu mwingine wakati ile hati nyingine iliyokuwepo bado haijafutwa na haijaweza kupatikana kiasi cha kuweza kuwapa hati wale wengine. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa baada ya ule utaratibu wa kisheria kukamilika, basi na hawa wengine ambao wamepewa maeneo yale katika lile shamba lililokuwa awali lililobadilishiwa matumizi, nao watapata. Pia kwa sehemu kubwa inaweza ikafanyika kwenye zoezi la urasimishaji kwa sababu tayari kuna maeneo mengi yameshajengwa hospitali, shule na makazi. Kwa hiyo, hilo litafanyika kulingana na taratibu za kisheria mara taarifa zilizopelekwa Polisi zitakapokuwa zimefikia hatima yake. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved