Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. UPENDO F. PENEZA (K.n.y. MHE. PETER A. LIJUALIKALI) aliuliza:- Je, ni lini programu ya REA III itaanza kutekelezwa katika vijiji ndani ya Wilaya ya Kilombero?

Supplementary Question 1

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mbunge wa Jimbo husika Mheshimiwa Lijualikali anakubali kwamba ni kweli kazi inafanyika, lakini changamoto iliyopo ni kwamba umeme unawekwa kwa kurukaruka. Wakishafikisha kwenye centre vitongoji vingine havipati na kutoka kwenye centre kwenda kwenye vitongoji vingine kuna umbali mpaka wa kama kilomita sita mpaka kilomita nane, suala ambalo baadaye litakuwa gumu kwa wananchi kupeleka umeme katika hivyo vitongoji vingine.

Swali lake ni kwamba: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuboresha usambazaji wa umeme kuhakikisha kwamba wanapopeleka kwenye kijiji basi wasambaze katika maeneo yote na vitongoji vyote vya kijiji hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba pia niulize kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Geita Mjini ambako mimi natoka. Serikali ilituahidi ndani ya Bunge kwamba kuna maeneo ambayo yamekuwa mitaa sasa na zamani yalikuwa ni vijiji, lakini kiuhalisia bado yana mazingira kama ya vijiji hivi; Serikali iliahidi kwamba bado wale wananchi ingawa wanaishi kwenye mitaa ingewapa umeme kwa kupitia mradi wa REA. Maeneo hayo ni katika Kata za Ihanamilo; baadhi ya mitaa; Kata ya Kasamwa, Kata za Kanyara na Kata za Burela.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali itatusaidia kupeleka umeme katika maeneo hayo na katika kata hizo kwa kupitia mradi huu wa REA kama ilivyoahidi ndani ya Bunge? Ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kushuruku kwamba Mheshimiwa Mbunge Lijualikali ametambua kazi mbalimbali ambazo zinaendelea katika Jimbo la Kilombero kuhusu mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza. Ametoa ushauri kwamba ni namna gani Serikali inaweza ikaboresha zaidi katika usambazaji wa umeme inapofika kwenye eneo fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeliona hilo kwamba, kwa kuwa miradi hii ngazi yake kwanza ni ngazi ya kijiji, imetambua vijiji zaidi ya 3,559 kwa awamu hii ya kwanza, REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vina vitongoji. Kwa hiyo, Serikali ilibuni mradi ambao ilifanya majaribio ya ujazilizi kwa mikoa minane ambapo uligusa vitongoji 305 na iliwaunganisha wananchi kama 25,000 na mradi ule ulifanyika kwa mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa na mafanikio hayo, tutakuja na mradi mwingine densification awamu ya pili katika Bunge hili la Bajeti linaloendelea. Kwa hiyo tutaomba mtuidhinishie, lakini mradi huu unakwenda kutatua tatizo la vitongoji vinavyoachwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine, hilo linatambulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuamini kwamba gharama za kupelekea umeme kwenye kijiji kimoja; kilimeta moja tu ni shilingi milioni 50. Kwa hiyo, Serikali ambayo inafanya mambo mengi ya kimaendeleo lazima kwenda hatua kwa hatua. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge waendelee kutuunga mkono na vitongoji vingine vitafikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge Upendo Peneza, ameelezea masuala ya Halmashauri ya Geita. Kwanza kata zote ambazo alizitaja, bahati nzuri na Mheshimiwa Mbunge mwenyewe wa Jimbo naye amelizungumzia, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili, lakini naye nimpongeze pia amelielezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba maeneo yote ambayo yako katika Halmashauri za Miji na tunatambua kwamba bado yapo katika pia katika maeneo ya vijijini, kuna mradi unakuja peri-urban ambako maeneo ya kata ambazo zimetajwa zitashughulikiwa na bei ni ile ile shilingi 27,000/=. Kwa hiyo, niwatoe hofu wakazi wa maeneo yote ya miji na mitaa, mradi wa ujazilizi na mradi wa wa peri-urban utakuja kutatua tatizo ambalo limebaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.