Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:- Gesi ambayo imegunduliwa katika Mkoa wa Mtwara itanufaisha wananchi wote nchini na Taifa kwa ujumla:- Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kujenga Chuo kitakachotoa mafunzo ya gesi na mafuta katika Kanda ya Kusini ili vijana wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta hii?

Supplementary Question 1

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa nini Serikali haitaki kuwapa gesi wawekezaji wa kiwanda cha mbolea ambao wako tayari kujenga Msangamkuu, Mkoani Mtwara vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, miongoni mwa manufaa ya gesi kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni pamoja na kupelekewa umeme lakini mpaka sasa baadhi ya maeneo hakuna umeme Mkoani Mtwara. Naomba kujua kwa nini Serikali haipeleki umeme maeneo mengi ya Mkoa wa Mtwara?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Shamsia, wifi yangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuna mwekezaji, ni kweli wapo wawekezaji kampuni ya WD capital ya Egypt pamoja na Oman Petra Chemical ya Oman na LMG ya Ujerumani ambayo iliingia makubalino na Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwekeza kiwanda cha mbolea katika Mji wa Msangamkuu ambayo itatumia malighafi ya gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme sio sahihi sana kwamba walikataliwa kupewa gesi, lakini kikwazo kilikuwa bei ya gesi ambao wawekezaji wetu walikuwa wanaitaka. Kwa mfano, sambamba na huyo pia kuna mradi wa Kampuni ya Ferrestal ambayo waliingia ubia na Kampuni yetu TPDC lakini wote hao walikuwa bei yao ya awali ambayo walikuwa wanaitaka ni iwe USD 2.26 ambako gharama za uzalishaji wa gesi hizi kwa mujibu wa EWURA ni USD 5.6. Kwa hiyo utaona gape yake lakini Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayovutia wawekezaji ili kupitia maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliridhia tuanze mchakato wa mazungumzo. Kupitia mchakato wa mazungumzo ambao ulihusisha TIC ambayo yalifanyika mwezi Machi mwaka huu 2019, tumefikia bei ambayo wenzetu wawekezaji hawa wamerejea ili kuitafakari na baada ya wiki mbili walisema watarejea tena na bei hiyo ni kama USD 3.36 ambayo tunaamini pengine hiyo inaweza sasa ikafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niwathibitishie wakazi wa maeneo ya Kilwa ambako Ferrestal na TPDC watajenga kiwanda hicho na wakazi wa maeneo ya Msangamkuu Mkoani Mtwara kwamba, fursa ya ujenzi wa viwanda vya mbolea ambao faida kubwa itatoa ajira na mapato bado ipo na Serikali hii ya Awamu ya Tano kupitia hata Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na hata Taasisi ya TIC na taasisi zingine tutahakikisha kwamba fursa hii itafanyika kwa ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameulizia kwa nini Mkoa wa Mtwara kwa kuwa unatoa gesi haujapelekewa umeme kwa kiwango ambacho Mheshimiwa Mbunge ameulizia. Nataka niseme ni kweli Mkoa wetu wa Mtwara tunautegemea sana kwa gesi megawati 1,600, zinazozalishwa sasa asilimia 52 inatokana na gesi. Pia Mkoa wa Mtwara kwa REA awamu ya tatu inaendelea ina vijiji 167, lakini Manispaa ya Mtwara Mikindani baadhi ya maeneo hata mimi niliyatembelea Mkangaula, Mkanalebi na pale maeneo ya mjini na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo tulikuwa naye pamoja na amekuwa wakiliulizia mara kadhaa hapa ndani ya Bunge kwa kazi nzuri ya kufuatilia miradi hii nimhakikishie tu ujazilizi awamu ya pili unaendelea na utaugusa Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo mengine na hata Mkoa wa Lindi kwa sababu bado tunatarajia gesi kutoa mchango mkubwa katika kuzalisha umeme ahsante sana.

Name

Alfredina Apolinary Kahigi

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:- Gesi ambayo imegunduliwa katika Mkoa wa Mtwara itanufaisha wananchi wote nchini na Taifa kwa ujumla:- Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kujenga Chuo kitakachotoa mafunzo ya gesi na mafuta katika Kanda ya Kusini ili vijana wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta hii?

Supplementary Question 2

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuulizia swali la nyongeza. Je, ni vigezo gani ambavyo vimepelekea kupeleka gesi ya bei nafuu majumbani Mkoani Dar es Salaam, sehemu za Mikocheni badala ya kuipeleka Mtwara mahali ambako gesi inaanzia. Ahsante?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Kahigi, kwanza nimpongeze kwa kutambua utanzania uliopo kwa sababu yeye anatokea Mkoa wa Kagera, lakini ameuliza swali linalohusiana na masuala ya gesi, kwa nini kwa watu wa Mtwara hawakuunganishiwa hii gesi ya majumbani. Nataka nimthibitishie kupitia Serikali yetu na TPDC kwa sasa na Mheshimiwa Waziri wetu wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Merdad Kalemani alizindua mradi wa usambazaji gesi majumbani Mkoa wa Mtwara na Dar es Salaam na ni kweli kwamba Dar es Salaam tuna takribani viwanda zaidi ya 20 ambavyo vimeunganishiwa, tuna nyumba nyingi lakini ndio utaratibu za kuunganisha zaidi zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimthibitishie Mheshimiwa Kahigi kwamba hata sasa hivi tunasubiri tu vifaa na kuanzia mwezi wa Nne wakazi wa Mkoa wa Mtwara kwenye nyumba za maeneo ya railway pale wataunganishiwa gesi, Chuo cha ufundi Mtwara Technical kitaunganishiwa gesi, pia na maeneo ya Mkuranga viwanda vyaGypsum nao wote wataunganishiwa gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme, miradi hii ya kusambaza gesi asilia majumbani ni mradi ambao unahitaji mtaji mkubwa. Tunaishukuru sana Wizara ya Fedha kwa kuridhia kwamba TPDC waendelee na mchakato wa kuhuisha sekta binafsi katika uwekezaji wa mradi huu ambao unatarajia kutumia takriban bilioni 200 katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dodoma na Tanga na pia kuna mpango wa kujenga bomba la gesi kuelekea Uganda, zote ni kutumia hizo fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nithibitishe kwamba kwa kweli Serikali yetu ya Awamu ya Tano inatambua matumizi ya gesi asilia ukiacha kuzalisha umeme lakini kwa viwandani na majumbani ili kulinda mazingira yetu kwa wananchi kuacha kukata miti, watumie gesi mbadala. Ahsante sana.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:- Gesi ambayo imegunduliwa katika Mkoa wa Mtwara itanufaisha wananchi wote nchini na Taifa kwa ujumla:- Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kujenga Chuo kitakachotoa mafunzo ya gesi na mafuta katika Kanda ya Kusini ili vijana wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta hii?

Supplementary Question 3

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimemsikiliza vizuri sana Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu akijibu hili swali, nami naliona ni jambo la muhimu sana kwa sababu uharibifu wa mazingira katika nchi hii umekuwa mkubwa sana na kwa sababu nchi yetu inatumia pesa nyingi sana za kigeni kuagiza mafuta kwa ajili ya magari na mitambo. Je, ni lini Serikali italeta hapa Bungeni mpango mkakati wa namna gesi yetu itakavyotumika majumbani na kwenye magari na mitambo mingine ili kuweza kuokoa pesa nyingi za kigeni ambazo zinatumika kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nje?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selasini,
kaka yangu na Mbunge wa Jimbo la Rombo ambalo ameuliza ni lini Serikali italeta mpango mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme Serikali kupitia TPDC ina mpango mkakati wa matumizi ya gesi, tangu gesi ilivyogunduliwa na kwa kuwa tuna gesi nyingi zaidi ya trilioni 55 Cubic feet, gesi hii imepangiwa mkakati wa matumizi yake. Kuna gesi ya kutumia kwenye masuala ya uzalishaji wa umeme, kuna kiwango cha gesi cha kutumia kwa ajili ya viwanda, kuna kiwango cha gesi cha kutumia kwa ajili ya majumbani, kuna gesi ya kiwango cha kutumia kwa ajili ya magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali lake aliloliuliza ni kwamba huo mkakati tunaowasilisha upo wa kimaandishi kabisa, Gas System Master Plan ambayo imeainisha matumizi yake na kiwango kimepangwa kabisa hadi 2035. Nachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, ndiyo maana nimesema mchakato wa matumizi yote haya hata sasa hivi kipo kituo Dar es Salaam pale Ubungo, unaweza ukabadilisha gari lako kutoka matumizi ya mafuta ya kawaida diesel kwenda kwenye matumizi ya gesi. Tunachofanya sasa ni kutaka kuongeza vituo vingi zaidi ili huduma hiyo ipanuke, kwa hiyo, jambo hilo lipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimesema hapa kwenye swali la nyongeza la mama yangu Mheshimiwa Mama Kahigi kwamba mipango yote inahitaji uwekezaji wa kutosha. Tunafurahi kwamba Serikali yetu kwa kuungwa mkono, Serikali ya Oman ilikuja hapa na kulikuwa na MoU tumeshaisaini lakini zaidi inataka kuisaidia sekta hii ya gesi hasa usambazaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua hilo na umuhimu wa utunzaji wa mazingira pia. Ndiyo maana sasa hivi hii gesi ya LPG inayotoka nje ya nchi tumeona tuipangie mkakati kwa muda kwamba lazima nayo iingie kwenye bulk procurement kusudi iingie kwa wingi kwa madhumuni ya kushusha bei na kutumika kwa wingi wakati tunasubiri utekelezaji wa mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha gesi hii yetu ya asilia tunaisambaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie hata mradi wa LNG wa Lindi wa kusindika gesi ili kurahisisha usafirishaji wake, sasa hivi mazungumzo yameanza tunatarajia utaanza 2024. Mradi huu ukishaanza tutakuwa na uwezo wa ku-export gesi zaidi na kusambaza ndani ya nchi na kujenga miundombinu ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, ahsante.