Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Juma Kombo Hamad
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Wingwi
Primary Question
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:- Vitendo vya utekaji kwa watu wasio na hatia na kuwatesa, kuwahujumu na hata kuwaua vinaendelea kukithiri nchini:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia, kulinda na kuhakikisha inakomesha vitendo hivyo haraka sana? (b) Je, hadi sasa ni watu wangapi ambao wamekamatwa na kuchukuliwa hatua kutokana na uhalifu huo?
Supplementary Question 1
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba yapo matukio ambayo yalitikisa sana ya aina hii Tanzania. Matukio haya ni pamoja na kitendo cha jaribio la mauaji ya Mheshimiwa Tundu Lissu, kutekwa kwa Mohamed Dewji, kutekwa, kupigwa na hatimaye kuuawa kwa Mheshimiwa Ali Juma Suleiman pale Unguja, matukio ya Kilwa na matukio ya kutekwa vijana saba pale Mkoa wa Kaskazini Pemba, Jimbo la Mtambwe. Je, Serikali inatuambia kwamba pamoja na matukio haya makubwa na mazito na ya kutisha, ndiyo ni mtu mmoja tu hadi sasa ambaye amekamatwa na kuchukuliwa hatua?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kutaka kufahamu, je, Serikali ipo tayari sasa kuunda Tume ili kuchunguza matukio haya ili kuyabainisha na kuwabainisha wanaohusika na matukio haya ili kuchukuliwa hatua za kisheria?
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ametaja matukio mbalimbali ambayo yametokea kwa wakati tofauti. Nataka tu nimthibitishie kwamba matukio haya kila moja Jeshi la Polisi liliyachukulia kwa uzito unaostahili na yapo katika hatua mbalimbali za upelelezi, yako ambayo upelelezi wake umeshakamilika na yameshawasilishwa kwa DPP, mengine yamepiga hatua hata zaidi ya hapo. Kwa hiyo, kuyazungumzia kwa pamoja matukio ambayo ni tofauti na yana mazingira tofauti inakuwa ni changamoto. Hata hivyo, nimthibitishie kwamba, kwa sababu suala la upepelezi mchakato, ni imani yetu kwamba matukio haya yataweza kufikia katika hatua nzuri na hatimaye haki itaweza kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na hoja yake ya kuundwa Tume, sijui sijaelewa anazungumzia Tume ya aina gani lakini nataka nimthibitishie tu kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pale ambapo imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ambayo yanapelekwa katika vyombo vyetu vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, tumekuwa na utaratibu wa kuunda Tume. Kuna Tume mbalimbali tumekuwa tukiunda na zimekuwa zikifanya kazi vizuri, kwa hiyo, si jambo geni.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved