Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:- Je, ni lini uzalishaji wa madini ya Niobium utaanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kutokana na majibu hayo, inaonyesha kuwa mgodi huu utakuwa ni neema sana kwa nchi yetu kwa sababu ya uzalishaji wa hayo madini ya Ferro-Niobium ambayo ni muhimu sana kwa ujenzi wa madaraja, Reli ya Standard Gauge pamoja na mabomba ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu huo, napenda kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni kwa kiasi gani hayo madini ya Ferro-Niobium pamoja na Niobium yenyewe yataongezewa madini ya chuma? Ni kwa kiasi gani haya madini ya chuma tutatumia madini yanayochimbwa hapahapa nchini kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vilevile imeonyeshwa kuwa kuna fidia kwa ajili ya Gereza la Songwe. Je, mwekezaji au wawekezaji wana mkakati gani badala ya kutoa fidia tu lakini waboreshe miundombinu ya gereza hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, vituo vya afya na huduma zingine za elimu hasa kwa wananchi wa Kata ya Bonde la Songwe ambapo kiwanda hicho na mgodi huo upo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Ferro- Niobium ni matokeo ya uchakataji wa madini hayo utakaofanyika. Pale Mbeya uchimbaji utakuwa ni wa Niobium peke yake lakini Niobium haiwezi kutumika peke yake ni mpaka pale utakapoichanganya na iron, ndiyo maana tunaita Ferro-Niobium kwa maana ya kutengeneza high strength low-alloy, kwa maana ya material ya kuunganisha vyuma. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba itatumika kwenye madaraja na kwenye pipes, ni kweli madini haya yakishakuwa Ferro-Niobium yanatumika katika kuunganisha vyuma vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge analitambua hilo na sisi kama Serikali tunalitambua hili. Kwa umuhimu wa material haya ndiyo maana katika jibu la msingi nimesema kwamba hii kampuni ikishaweka pale kiwanda, kwa maana ikishachimba Niobium itachanganywa na hiyo Ferro kwa maana ya iron kisha itauzwa nchi za nje. Kwa mfano, Amerika Kaskazini wanahitaji sana bidhaa hii kwa ajili ya utengenezaji au uunganishaji wa vyuma vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni material ambayo yanahitajika sana duniani na sisi kama Serikali tunatambua. Tunasema kabisa kwamba tukishaweka kiwanda hiki pale, wakishachimba Niobium yetu haitatosha mahitaji kwa sababu itakuwa ni kiwanda peke yake Afrika ambacho kitakuwa kimejengwa pale Songwe na Niobium itakayohitajika, itahitajika hata ile ambayo ni nje ya Tanzania, ina maana Congo na Zambia wataleta Niobium yao hapa. Kwa hiyo, tutatumia Niobium karibu ya Afrika nzima katika kiwanda hiki ambacho kitajengwa Songwe. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu wa kiwanda hiki na sisi kama Serikali tumeshikamana kihakikisha kwamba sasa tunakwenda kuhakikisha machimbo haya yanaanza na utengenezaji wa kiwanda kwa maana ya kuongeza thamani kinaanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, tunatambua kweli machimbo au mgodi huu, yako chini ya Gereza la Songwe. Tunapenda kusema kwamba ile ziara ya Mheshimiwa Rais aliyokuwa amekwanda Mbeya imekuwa ni chachu kubwa sana kuhakikisha kwamba zile mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Uwekezaji tunakweda kukaa pamoja kuangalia ni namna gani sasa mwekezaji huyu atalipa fidia na kuweza kuhamisha gereza lile kulipeleka pembeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua yuko tayari kulipa kiasi cha dola milioni saba kujenga gereza jipya ambalo litabeba wafungwa 500 na kujenga nyumba mpya kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya 120 na ataweka miundombinu ya umwagiliaji pamoja na barabara kuhakikisha kwamba anaboresha maisha na mazingira ya gereza lile ambalo litajengwa pale pembeni. Kwa hiyo, mamlaka husika zinafanya kazi kuhakikisha kwamba tunamsaidia mwekezaji huyu na masuala yote ya kodi tumeshayaweka sawa, tuna hakika kabisa tutakwenda kuanza mradi huu muhimu kwa Tanzania. Ahsante sana.