Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Primary Question
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:- Kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa Shule za Msingi Wilayani Mwanga:- Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu 384 wanaohitajika?
Supplementary Question 1
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa kuwapa pole sana wananchi wa Machame na hasa familia ya Marehemu Dkt. Reginald Mengi kwa msiba uliowapata. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho haye mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika, sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, kwanza, uhaba wa walimu 384 tumepewa walimu 21! Katika shule zetu, shule 50 zina walimu wawili wawili na shule zingine 40 zina walimu watatu watatu, sasa ujue hizo zingine ndiyo… na shule za msingi zina madarasa nane, darasa la awali na madarasa saba, kwa hiyo, hali iliyoko pale ni ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, na kwa sababu uhaba huu umetokana na walimu kustaafu, kuhama na kufariki. Suala la fedha halipo hapa, kwa sababu nafasi zipo, na mishahara ipo, ni kwa nini sasa Serikali haichukui hatua ikaajiri bila kutumia visingizio ambavyo havina msingi.
Mheshimiwa Spika, pili, ni lini Serikali itabadilisha urasimu huu, kama mwalimu yupo na yuko kwenye ikama, na amestaafu. Kwa nini Serikali hairuhusu halmashauri ikaajiri kutoka kwenye soko mara moja ili kutoathiri upatikanaji wa elimu katika shule. Inaacha mpaka shule zinakuwa na mwalimu mmoja?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwikwabe Mwita Waitara, maswali hayo muhimu sana, Mwanga upungufu wa walimu 300, Kongwa upungufu walimu 1000. Majibu tafadhali.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli, tuna upungufu wa walimu wa shule za msingi 66,000 nchi nzima, na upungufu wa walimu wa sekondari 14,000, kwa hiyo, ni kweli kwamba kuna upungufu, ni jambo ambalo liko wazi.
Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, hizi ajira mpya ni ajira za kuziba nafasi. Sasa hivi inayofuata ni ajira zile za kawaida za kila mwaka za kuongeza na kupunguza upungufu uliopo. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba Serikali imeshaliona hili, tulifanya uhakiki, pamoja na watumishi hewa, waliofariki, waliofukuzwa kazi na wengine wamestafu na wengine wameacha kwa sababu mbalimbali. Kwa hiyo, hili ilikuwa ni kuziba nafasi hizi, sasa inakuja ya ajira za kila mwaka za kuweza kuziba kwa utaratibu wa kawaida na hili linafanyiwa kazi na Serikali inajua kwa kweli kuwa kuna upungufu mkubwa nchini wa walimu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kwamba, ni kuziba nafasi kwa maana ya kutoa kibali kwa halmashauri. Hizi ni ajira, cha muhimu hapa siyo kuruhusu utaratibu usioelekeweka utumike kuajiri walimu, kumekuwa na mambo mengi sana katika halmashauri zetu ambayo yanafanyika katika ajira hizi, kwa hiyo, tunajiridhisha kwanza. Lakini cha muhimu ni kwamba tumekubaliana kama Serikali kuchukua hatua mahususi kupunguza upungufu wa walimu shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Susan Limbweni Kiwanga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Mlimba
Primary Question
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:- Kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa Shule za Msingi Wilayani Mwanga:- Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu 384 wanaohitajika?
Supplementary Question 2
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kama ilivyo kwa Mheshimiwa Maghembe Mwanga, Wilaya ya Kilombero yenye majimbo mawili ilikuwa na upungufu wa walimu 1,118 na hivi juzi tu tumeletewa walimu 34, wanne wa sayansi sekondari na 30 wa msingi na kufanya nakisi upungufu huo ubaki 1,084.
Je, Serikali ni lini sasa itapeleka walimu ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, ili watoto wale wapate chakula cha akili, ukizingatia na miundombinu yetu si rafiki?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama nilivyosema, tumeajiri walimu 4,549, tuna shule za msingi 16,000 za Serikali na tuna shule zaidi ya 4000 za sekondari. Katika hali ya kawaida upungufu huo naupokea kama Serikali ni kweli, kuna upungufu mkubwa na tusingeweza kupeleka kila mahali. Lakini tuliangalia kwa mfano kuna shule ambazo pale kulikuwa na wakumu ambao wanapelekwa shule za msingi, wameenda mahitaji maalumu, wameenda na masomo ya sayansi na hisabati.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, angalau tukaangalia shule ambazo zina upungufu mkubwa zaidi tukapeleka pale, kwingine tumepeleka walimu mpaka watano, wengine wanne.
Mheshimiwa Spika, lakini, Mheshimiwa Susan Kiwanga wiki iliyopita aliuliza swali hap ana walimu hao. Tumeshatoa maelekezo, kwanza kuna walimu wapo kwenye halmashauri, makao makuu ya wilaya au ya mji, lakini unakuita pembezoni kule unakuta walimu ni wachache, lakini walimu wapo. Tumeshapeleka fedha katika halmashauri zote nchini za kuweza ku-balance ikama.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatarajia kwamba kazi hii itafanyika kwa kusimamiwa na Makatibu Tawala Mikoa na Wakurugenzi, ndani ya wiki mbili mpaka tatu, tupate taarifa rasmi.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ilikuwa kuhamisha walimu kupeleka pembezoni ilikuwa ni ngumu kwa sababu fedha hazipo, sasa fedha wameshapelekewa Halmashauri zote, zinatakiwa kazi ifanyike, halafu ajira inayofuata tutazingatia maeneo yote ambayo yana upungufu mkubwa. Shule za msingi, hisabati na masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Spika, ahsante, likiwemo na eneo la Kongwa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved