Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Angelina Adam Malembeka
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA aliuliza:- Matukio ya kubakwa na ulawiti kwa watoto nchini yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na watuhumiwa walio wengi huachiwa au humalizana na wazazi wa waathirika kifamilia:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kesi hizo hazimalizwi kifamilia? (b) Je, ni mkakati gani umewekwa ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa hao wanapopatikana na hatia wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia mbaya? (c) Je, watoto waliopatwa na matukio hayo wamewekewa mazingira gani ili kuwaondoshea msongo wa mawazo na kuendelea na elimu bila kubughudhiwa na wenzao.
Supplementary Question 1
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa, adhabu mojawapo aliyoitaja ni kifungo cha maisha kwa wale ambao watapatikana hatia na huko gerezani tayari wameshakuwa na tabia kama hiyo, haoni kwamba kwa kuwaweka gerezani maisha wataendelea kufanya shughuli hiyo, kwa nini adhabu isiongezwe na waweze kuhasiwa ili wasirudie tena kitendo hicho?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba vitendo vya ubakaji vinajirudia mara kwa mara; Je, anaweza kunipa taarifa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ni kesi ngapi zimepelekwa Mahakamani na ngapi zimetolewa hukumu. Ahsante.
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge yeye anaona adhabu ya gereza haitoshi, hata kwenda jela maisha haitoshi ila anataka vile vile wahasiwe. Siwezi kuwa na jibu hapa kwa sababu hili ndilo Bunge linalotunga sheria za nchi, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge aje na hilo wazo liletwe mbele ya Bunge hapa, ni ninyi mtakaopitisha kwamba wanaume wahasiwe wanaokutwa na hilo tatizo au la, lakini siyo Serikali kuja na shauri hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anataka kujua statistics, kujua ukubwa wa tatizo hili. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo la kubaka na kulawiti nchi hii sasa hivi limefikia mahali pabaya kwa sababu, ukichukua takwimu za miaka mitatu au miaka minne iliyopita, tuna matukio kumi na tisa kila siku ya Mungu ya kubaka na kulawiti. Hayo matukio 19 ya kila siku ya Mungu ni yale ambayo yanaripotiwa, sasa siyo ajabu yakawa mara tatu ya hapo yale ambayo yanapita bila kuripotiwa na kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili ni tatizo kubwa, Waheshimiwa Wabunge lazima tushirikiane. Kati ya mwezi Januari mpaka mwezi Machi mwaka huu tu nimepata taarifa hapa kwamba tuna mashauri 2,031, miezi mitatu tu! Mpaka sasa naipongeza Mahakama kwamba pamoja na uchache wao wameweza kuzikamilisha kesi 111, watuhumiwa 96 wamefungwa. watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi, lakini bado kesi 1,920 kwa miezi mitatu bado hazijakamilika. Hiyo ndiyo changamoto tuliyonayo ambayo naona Waheshimiwa Wabunge wote ni kazi yetu kuweza kuitatua.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved