Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maulid Said Abdallah Mtulia
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. MAULID S. A. MTULIA aliuliza:- Vijana wetu wanafanya kazi za sanaa nzuri sana lakini kipato wanachokipata hakilingani na ubora wa kazi zao:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana hawa kupata stahiki ya kazi zao? (b) Je, sera na sheria zinasaidiaje wasanii wetu kumiliki na kunufaika na kazi zao za sanaa?
Supplementary Question 1
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitoe shukrani zangu za dhati kwa majibu mazuri ya Serikali. Vilevile niendelee kuhimiza Serikali kwamba mabadiliko ya Sera na Sheria ya Bodi ya Filamu yafanyike kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wasanii wetu wamedhulumiwa kazi zao na wasambazaji walikuwa wanawaingiza mikataba kama wasimamizi badala ya wamiliki wa kazi; kwa kuwa sheria ipo kulinda haki za wasanii; na kwa kuwa nchi za wenzetu mfano Nigeria iliwahi kutoa tamko kuhakikisha kazi zote za wasani umiliki urudishwe kwa wasanii wenyewe, je, Serikali yetu ya Tanzania iko tayari sasa kutoa tamko kuhakikisha wale wote waliodhulumu kazi za wasanii umiliki unarudi kwa wasani wenyewe ili waweze kunufanika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wasanii wetu wanaendelea kuzalisha kazi nzuri kabisa; na kwa kuwa walaji wengi katika jamii wanahitaji kuendelea kuziona kazi za wasanii na katikati yake kuna ombwe kubwa kwamba wasanii, waandaaji na walaji hawaonani, je, Serikali ipo tayari kuja na suluhisho kuhakikisha kazi za wasanii zinafika kwa walaji ili wasanii waepukane na kutembeza CD mkononi wao wenyewe?
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Said Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa jinsi ambavyo amekuwa akipambania maslahi ya wananchi wa Kinondoni, ukizingatia kwamba wasanii wengi walioko katika jiji la Dar es Salaam wanaishi katika Wilaya yake ya Kinondoni. Kwa hiyo, nampongeza sana kwa kupambania maslahi ya wasanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali lake la kwanza ambapo ametaka kujua kama Serikali tuna mpango gani wa kurejesha zile hakimiliki ambazo zimechukuliwa kutoka kwa wasanii. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa Sheria ya Hakimiliki ya mwaka 1999 ambayo tunayo sasa hivi inatoa haki na uhuru kwa msanii mwenyewe kuamua ni namna gani ambavyo atataka kuuza haki yake. Kama akitaka kuuza kazi zake zote kwa maana kwamba anauza pamoja na ile master ya kazi yake au kuuza baadhi kazi zake. Kwa hiyo, ni suala la msanii mwenyewe kuamua anataka kuuza kazi zake kwa njia gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Serikali kwa kutambua kwamba suala hilo limeleta mchanganyiko mkubwa sana na halina maslahi kwa wasanii, kitu ambacho tunafanya kwanza ni kutoa elimu kwa wasanii kuweza kutambua haki na thamani ya kazi zao, kwa sababu tumeona madhara makubwa sana ambayo yamekuwa yakiwapata wasanii pale ambapo wanauza mpaka umiliki wa zile kazi zao. Kwa hiyo, tunaelimisha wasanii kwanza waweze kutambua kwamba kazi zao zina thamani, ukiuza leo kazi yako pamoja na master ni kitu ambacho kitaendelea kutumika miaka mingi matokeo yake hayatakuwa mazuri kwa miaka ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea kutoa wito kwa wasanii wote nchini Tanzania kwanza kutambua thamani ya kazi yao na kuona kwamba siyo jambo jema kuuza mpaka umiliki wa kazi zao. Hata hivyo, kwa sheria ambayo tunayo inatoa haki kwa msanii kuamua ni namna gani ambavyo atauza kazi yake. Kwa hiyo, sisi kama Serikali hatuwezi kutoa kauli ya moja kwa moja kwa sababu sheria imewapa uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwenye swali lake la pili ambalo amezungumzia kuhusu tatizo la usambazaji, ni kweli kwamba kwa miaka ya hivi karibuni tasnia yetu ya sanaa imekumbwa na changamoto nyingi ikiwepo suala la usambazaji. Kama ambavyo tunajua tatizo la usambazaji kwa miaka ya hivi karibuni lilisababishwa na kukosekana kwa kazi ambazo zina ubora na ubunifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usambazaji ni biashara kama biashara zingine. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tunaamini kwamba hakuna mfanyabiashara atawekeza mtaji wake kwenye biashara ambayo anaamini kwamba haiwezi kumpa faida hapo baadaye. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea kutoa wito kwa wasanii kwanza kutengeneza kazi ambazo zina ubora na zitaleta ushindani kwenye soko lakini zitavutia wasambazaji wengi kuja kuwekeza mitaji kwenye kazi zao hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa sababu tunajua kwamba sasa hivi pia kuna mabadiliko ya sayansi na teknolojia na tumeshuhudia wasanii wengi sana wamehama kutoka kwenye mfumo wa kusambaza kazi zao kwa njia ya CD wanatumia njia ya mtandao. Kuna msanii anaitwa Wema Sepetu, kwenye filamu yake ya Heaven Sent. amefanya vizuri sana, amesambaza kazi yake kwa njia ya mtandao na mauzo yamekuwa mazuri. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wasanii sasa waangalie namna gani ambavyo wataenda mbele zaidi kwa mabadiliko haya ya sayansi na teknolojia ili waanze kusambaza kazi zao kwa njia ya kimtandao.
Name
Joseph Leonard Haule
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. MAULID S. A. MTULIA aliuliza:- Vijana wetu wanafanya kazi za sanaa nzuri sana lakini kipato wanachokipata hakilingani na ubora wa kazi zao:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana hawa kupata stahiki ya kazi zao? (b) Je, sera na sheria zinasaidiaje wasanii wetu kumiliki na kunufaika na kazi zao za sanaa?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasanii wa Tanzania changamoto yao kubwa sana na namba moja ambayo inawakabili ni wizi wa kazi zao. Tumekuwa tukiona kazi zao zikiuzwa kwa holela kwenye maeneo mbalimbali lakini Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, Na.7 ya mwaka 1999 imeonekana kuwa haina meno wala haiwasaidii wasani wa Tanzania. Je, ni lini Serikali italeta sheria hii hapa Bungeni ili tuweze kuifanyia mabadiliko ili wasanii wa Tanzania ambao wanaleta sifa kubwa kwa Tanzania kwa kupitia sanaa yao waweze kufaidika na kazi zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Profesa Jay kwa swali nzuri la nyongeza kwa sababu yeye pia ni msanii, kwa hiyo, anatambua changamoto ambazo zinawakumba wasanii nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna changamoto kubwa sana ya suala la wizi ya kazi za sanaa, lakini sisi kama Wizara tumechukua hatua kadhaa. Hatua mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunawahamasisha wasanii waweze kusajili kazi yao COSOTA ili pale ambapo wanapata matatizo iwe rahisi kuweza kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile amezungumzia changamoto kubwa ya sheria, tukiri kwamba hii sheria ina upungufu lakini Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ipo kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa hiyo, kama Wizara ambacho tunafanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba kitengo hiki cha COSOTA kinahama kutoka Viwanda na Biashara kuja kwenye Wizara yetu ya Habari ili tuangalie ni namna gani ambavyo tutaifanyia marekebisho sheria hii. Ahsante.