Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Afya za wanawake wengi vijijini zinaathiriwa na moshi wa kuni wanazopikia kwenye majiko ya mafiga matatu ambayo yanatumia kuni nyingi na hivyo kuchochea kasi ya ukataji miti:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa matumizi ya majiko ya mafiga matatu kote nchini? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuondoa majiko hayo kwenye shule zote za msingi na sekondari?
Supplementary Question 1
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu yao mazuri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; sasa hivi ni takribani miaka 53 toka tumepata uhuru na majiko haya yamekuwa yakitumika pamoja na athari zake. Je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha kampeni mahususi ya kutokomeza matumizi ya majiko ya mafiga matatu katika shule za sekondari, vyuo, primary na kote huko ili kuondoa athari hizo kama ilivyofanya kampeni ya kuboresha maabara na kuleta madawati kwa shule zote hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna makampuni binafsi ambayo yanasambaza gesi hizo za kupikia (liquid gas) na pia kwenye mitungi midogo ambayo ni affordable ikiwemo Mihan na Oryx. Sasa Serikali iko tayari kushirikiana na makampuni hayo ili kupunguza athari za moshi unaowaumiza sana akina mama walioko vijijini na kwingineko na bado hawajapata elimu ya matumizi ya majiko hayo kwamba wanaumia ili waweze kupatiwa majiko hayo kwa bei nafuu? (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa mama yangu Shally Raymond. Kwanza nimpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye eneo lake la Mkoa wa Kilimanjaro hususan kwa masuala ya wanawake na inadhihirisha kwa swali hili ambalo ameliuliza linalohusiana na masuala ya majiko ya mafiga matatu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza la nyongeza ameulizia kama Serikali ipo tayari kuanzisha kampeni ya kuondokana na majiko haya hususan katika shule za sekondari na msingi.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, tunatambua kwamba majiko haya ya mafiga matatu yana athari ya kimazingira na kiafya lakini kwa kuwa tumelitambua hilo, Serikali pia ina mpango wa usambazaji wa gesi asilia katika mikoa mbalimbali ambapo imeanza na mikoa saba ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga, Dodoma na Morogoro lakini sambamba na hilo, Serikali pia imekuwa iki-support makampuni yanayohusiana na gesi ya LPG.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa hatua hizi zinaendelea katika kuhakikisha kwamba kwanza gesi asilia inasambazwa katika maeneo mbalimbali ambayo ina bei nafuu, lakini pili kwa kushirikiana na makampuni yanayoingiza nchini LPG ili iweze kushusha bei, nina uhakika kwamba tutafikia hatua hiyo ya kupeleka nishati hii ambayo itatumika katika shule za sekondari.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, pia kuna makampuni mbalimbali ambayo yanashirikiana katika suala zima la usambazaji wa nishati jadidifu katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, nitoe wito tu katika makampuni hayo kuendelea kuiunga mkono Serikali ili iweze kufikia hatua ya kutangaza hiyo kampeni na ni jambo jema. Namwomba yeye pamoja na Wabunge wote wa Viti Maalum, Wabunge wote na wananchi mbalimbali tuhamasishe utunzaji wa mazingira na utumiaji wa nishati mbadala hasa katika kupikia ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli yapo makampuni kama nane ambayo yanahusika na masuala ya uingizaji wa gesi ya LPG ikiwemo Oil Gas Tanzania Ltd, Taifa Gas, Mount Meru Gas lakini pamoja na hayo kuna Lake Gas, Oilcom na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali imefanya? Tumeona kwa kuwa kiwango cha matumizi ya LPG kimeongezeka kutoka kwa mfano tani 90,000 mwaka 2016 mpaka tani 147,000 mwaka 2018. Kwa hiyo, ni wazi matumizi yameongezeka, kwa hiyo, tulichofanya, tunatafakari namna ambavyo gesi ya LPG inaweza ikaingizwa kwa mfumo wa uagizwaji wa pamoja. Tupo katika mazungumzo na wadau wa makampuni haya na taasisi mbalimbali ili kuwezesha kuweka mazingira wezeshi ambayo yataisaidia hata EWURA kuweza kupanga bei ambayo inaweza ikawasaidia watanzania kutumia gesi hii ili kulinda mazingira yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa makampuni ambayo yanaagiza; kwanza nawapongeza kwa uwekezaji wanaofanya, waendelee kujenga miundombinu katika mikoa mbalimbali ili hii gesi ya LPG iweze kuwafikia Watanzania wote. Serikali itaendelea kuandaa mazingira wezeshi ili kuwezesha huduma hii ipatikane kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Name
Mussa Azzan Zungu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ilala
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Afya za wanawake wengi vijijini zinaathiriwa na moshi wa kuni wanazopikia kwenye majiko ya mafiga matatu ambayo yanatumia kuni nyingi na hivyo kuchochea kasi ya ukataji miti:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa matumizi ya majiko ya mafiga matatu kote nchini? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuondoa majiko hayo kwenye shule zote za msingi na sekondari?
Supplementary Question 2
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Athari ya moshi ni sawa na athari ya umeme unaopita juu ya nyumba za wananchi. Kuna mradi Mchikichini, Mtaa wa Ilala Kota eneo la Baghdad ambapo TANESCO walikubaliana na wananchi kupitisha umeme mkubwa sana juu ya nyumba zao lakini kwa kigezo cha kuwalipa fidia. Umeme umepita, umeme ulikuwa usiwashwe mpaka fidia ilipwe, lakini umeme umewashwa na fidia haijalipwa, watu wako chini ya umeme mkubwa na wanaathirika kiafya.
Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kujua ni lini sasa Serikali au TANESCO itawalipa fidia wananchi hawa wa Mchikichini ambao wako hapo kwa zaidi ya miaka 50, huduma zote wanapata pale. Kuna kigezo kililetwa kuwa eneo lile ni hatarishi. Wananchi hawa wamekaa hapa miaka 50 wana huduma za maji, umeme na wanalipa bili zote na kikubwa kabisa inapokuja uchaguzi maboksi ya kura yanapelekwa maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na TANESCO wawafikirie wananchi hawa ambao ni masikini, wawalipe fidia waondoke ili waondokane na athari ya kuathirika na umeme huu mkubwa katika nyumba zao. (Makofi)
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zungu kwa kuulizia na kufuatilia masuala ya fidia kwa wananchi Mchikichini. Ni kweli kabisa wananchi wa Mchikichini walipitiwa na umeme mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Ilala miaka sita ama saba iliyopita. Ni kweli katika eneo hilo bahati nzuri sana eneo hilo lilichukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Dar es Salaam lakini ni kweli wananchi hao wanatambulika na kwamba walikuwa wakidai fidia.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunafanya majadiliano ya kina sana na Manispaa ya Ilala ili kuhakikisha kwamba wananchi ambao wanadai fidia ni wale ambao kweli waliathirika na fidia. Pili kwa sababu eneo hilo lilichukuliwa na Halmashauri ya Manispaa, tunafanya mazungumzo ili wananchi hao waendelee kupata haki yao kulingana na wanavyostahili.
Mheshimiwa Spika, la pili, nampongeza Mheshimiwa Zungu, wiki mbili zilizopita tumekaa na Mheshimiwa Zungu kupitia kwa Kamishna wetu wa Nishati na tumefanyia kazi kwa kina suala hili. Wananchi hao tunawasihi wawe watulivu wakati suala hili linafuatiliwa kati ya Wizara na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili waweze kupatiwa haki yao ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana. (Makofi)