Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:- Wilaya ya Rufiji ni moja ya Wilaya kongwe nchini na inakadiriwa kuwa na watu takribani 350,000; eneo la Wilaya ni kubwa na huwalazimu wananchi kusafiri umbali wa kilometa 100 kufuata huduma za kibenki. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma za kibenki katika Wilaya ya Rufiji?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Rufiji ni Wilaya kongwe sana iliyozaa zaidi ya Wilaya tano lakini pia imezaa Taifa la Fiji kama ambavyo wewe mwenyewe unafahamu. Lakini pia eneo la Rufiji, Kibiti na Kilwa hakuna benki yoyote ya biashara na Serikali sasa inapeleka zaidi ya trilioni saba za ujenzi wa uzalishaji wa umeme katika Bwala la Mto Rufiji ambapo tunategemea kuwepo kwa watumishi, wafanyakazi zaidi ya 6,000 mpaka 7,000.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kwamba tawi la benki katika Wilaya yetu ya Rufiji haliepukiki? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, eneo la Rufiji lina ukubwa wa zaidi ya hekari 500,000 ambao lipo ndani ya Bonde la Mto Rufiji, lakini pia kwa kuwa Serikali inatekeleza Mradi wa Umeme wa Rufiji, Serikali pamoja na Wilaya ya Rufiji imetenga zaidi ya hekari 150,000 kwa ajili ya kwenye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni muhimu sasa kuwepo Rufiji ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Rufiji kuchangamkia fursa za maendeleo, fursa za kilimo, fursa za biashara katika Mradi wetu wa Umeme wa Rufiji? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu kwamba Serikali haioni kwamba haiepukiki sasa kufungua tawi Rufiji, kama nilivyosema benki nyingi zinaendeshwa kibiashara na benki nyingi huwa zinaangalia commercial viability ya eneo husika kabla hawajaweza kupeleka tawi la benki husika kwenye eneo husika. Kwa hiyo, kama ambavyo nimesema kwenye jibu la msingi, mabenki yetu yanafanya utafiti huo na tathmini kujiridhisha na nini kinatakiwa kufanyika kwenye maeneo husika. Hata hivyo, nimwambie Mheshimiwa Mchengerwa kwamba baada ya swali lake hili kama Serikali tumeanza kuifanyia kazi na tumeongea na Mkurugenzi wa TPB PLC na Mkurugenzi ameomba yafanyike yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza anaomba apate maombi mahsusi ili kuweza sasa kutuma timu yake kwenda kufanya kufanya feasibility study na kujiridhisha na commercial viability ya eneo la Rufiji ili kwenda kufungua tawi la Benki ya TPB kutokana na potentials zote kama zilivyoelezwa na Mheshimiwa Mchengerwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusu Benki ya Kilimo, kama alivyosema yeye mwenyewe Benki ya Kilimo ni benki ya maendeleo, hivyo lazima kila inapokwenda kufunguliwa ielewe kabisa wanakwenda kuhudumia aina gani ya wananchi ambao wako kwenye miradi mikubwa ya kimaendeleo. Pia Rufiji hawako mbali sana na Dar es Salaam ambako Benki yetu ya Kilimo ya Maendeleo ndipo Makao Makuu yake yalipo ambapo inahudumia maeneo yote ya Pwani, maeneo ya Morogoro. Kwa hiyo, niwaombe sana wakulima wetu wakubwa ambao wanahitaji mikopo ya maendeleo wafike Dar es Salaam na watahudumia na Benki yetu ya Kilimo ya Maendeleo. (Makofi)

Name

Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:- Wilaya ya Rufiji ni moja ya Wilaya kongwe nchini na inakadiriwa kuwa na watu takribani 350,000; eneo la Wilaya ni kubwa na huwalazimu wananchi kusafiri umbali wa kilometa 100 kufuata huduma za kibenki. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma za kibenki katika Wilaya ya Rufiji?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Igunga kwa kupindi cha miaka mitano sasa shughuli zake za uchumi zimeongezeka sana, watu wanalima, watu wanafuga na kuna fedha nyingi mzunguko ni mkubwa, lakini tatizo ni kwamba tuna benki moja tu Benki ya NMB. Benki ya CRDB walikuja wakafanya evaluation wakaona economic viability pale ni nzuri na wakaja wakatembea, lakini mpaka sasa hivi hawajaanzisha benki. Naomba Serikali, ni wakati sasa kama wanaweza kutusaidia kuiambia Benki ya CRDB wafungue tawi pale Igunga. Ahsante sana.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Peter Dalaly Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa yake ya kwamba Benki ya CRDB ilifika na kufanya economic analysis na commercial viability ya Wilaya yetu ya Igunga, na mimi nimepokea maombi yake, nitawasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa CRDB kuhusu kujua utafiti huo umefika wapi na nini maamuzi yao, kama inaonekana kuna commercial viability nina uhakika mkubwa kwa sababu CRDB ni moja ya benki inayowafikia wananchi, watafika Igunga.

Name

Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:- Wilaya ya Rufiji ni moja ya Wilaya kongwe nchini na inakadiriwa kuwa na watu takribani 350,000; eneo la Wilaya ni kubwa na huwalazimu wananchi kusafiri umbali wa kilometa 100 kufuata huduma za kibenki. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma za kibenki katika Wilaya ya Rufiji?

Supplementary Question 3

MHE. RHODA E. KUMCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na changamoto za kukosa huduma za kibenki katika Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mlele pamoja na Wilaya ya Tanganyika ni moja ya Wilaya ambazo zinakosa huduma za kibenki na ukizingatia asilimia 80 ya wakulima walioko kule wanafanya biashara kubwa na wana pesa nyingi wanasafirisha kwa njia ya magari. Sasa usalama wa fedha zao kutoka katika Wilaya hizi wanatembea zaidi ya kilometa 60 mpaka katika Wilaya ya Mpanda.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha tunapata matawi ya kibenki ili wakulima hawa waweze kusafirisha fedha zao katika mazingira yaliyo salama? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Rhoda Kunchela, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, inashangaza kidogo kusema wananchi bado wanasafirisha pesa kwa magari wakati Serikali imefungua na imeongeza mawanda mapana kabisa ya huduma za kibenki hapa nchini. Hakuna eneo lolote utakapofika hapa nchini ukakosa huduma za kifedha za mawakala wa benki zetu mbalimbali na huduma za simu banking katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, ndio maana Tanzania inaongoza kwa Afrika kwa huduma za fedha jumuishi. Kwa hiyo, niwaombe sana wananchi wetu Wilaya ya Mlele, Wilaya ya Katavi waweze kuzitumia fursa hizi zilizopo baada ya Serikali yao kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini. Mawakala wengi wa huduma za fedha wapo kwenye maeneo yote nchini na sasa kila mwananchi ana simu yake, tumeweza kusajili simu kwa hiyo sasa hivi ni rahisi sana kufanya transactions.

Sasa hivi unapofanya transaction niwaambie wananchi wa Tanzania huna wasiwasi wa kutuma pesa yako kwa simu kwa sababu mfumo umeunganishwa na Benki Kuu ya Tanzania, kwa hiyo, unajua kabisa kabla hujatuma kuliko kukaa na kuanza kufikiri fedha yangu imepotelea njiani, sasa unaulizwa kabisa unamtumia fulani bin fulani, una uhakika kwa hiyo hakuna wasiwasi wowote. Niwaombe Watanzania watumie fursa hii ya huduma za fedha jumuishi kwa maendeleo yao na maendeleo ya Taifa letu.