Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Katika miaka ya hivi karibuni nchi yetu imekuwa na majina mengi katika Idara ya Ukaguzi toka Ofisi ya CAG kama vile Hati safi, Hati inayoridhisha na Hati chafu:- (a) Je, Shirika au Halmashauri kupata hati safi ni ishara kwamba Shirika au Halmashauri husika halina ubadhirifu wa mali ya Umma kwa kuwa kuna kila dalili kuwa kutolewa kwa hati safi ni dalili ya wazi ya kuficha ubadhirifu katika baadhi ya Mashirika na Taasisi za Umma? (b) Je, lini Serikali itafuta utaratibu huo ambao umekuwa kinga ya ubadhirifu wa mali ya Umma?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yametolewa na Naibu Waziri, lakini mimi shida yangu ni moja tu. Mimi sio Mhasibu sana lakini ukitazama ukweli uliopo ni kwamba ukaguzi huu ambao ni wa Kimataifa unaonyesha nyaraka za kihesabu na vitabu vya kihesabu vinavyokaguliwa kama viko sawa, lakini havionyeshi matumizi ya ndani kama shirika limepata hati safi kwa maana kwamba halina ubadhirifu. Sasa je, Serikali inaonaje sasa, utaratibu wa Kimataifa uendelee lakini tuwe na utaratibu wa ndani ili kutambua ubadhirifu unaotokea kwenye mashirika yaliyo na hati safi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kuna dhana ya ukaguzi ambapo wanaona kama kuna matatizo makubwa yanatokea kwenye athari za kihesabu; sasa haya matatizo makubwa na haya madogo anayoyataja sijayaona kwenye majibu yake; pengine angeweza kutusaidia kwamba haya matatizo makubwa ya kiathari za hesabu ni yapi kwenye shughuli za kimahesabu?

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nayajibu maswali yake yote mawili kwa sababu yote jibu lake ni moja. Zipo aina tofauti za kaguzi zinazofanyika ukiacha kaguzi za mahesabu kama nilivyosema ili kujibu maswali yake yote mawili kwamba ni matatizo gani makubwa na madogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kunapokuwa na matatizo hayo mengine ambayo yako nje ya taarifa za kihasibu, huwa kuna ukaguzi wa ufanisi (performance audit) ili kuweza kuijuza Serikali juu ya namna bora ya kutumia rasilimali zake katika kubana matumizi; pia kuhimiza taasisi za Umma kuboresha utendaji wake wa kazi kufikia malengo kwa tija na kupata thamani halisi ya fedha.

Kwa hiyo, hapa tunakwenda kwenye miradi yenyewe kuangalia mchakato mzima wa mradi ulifanyikaje na mradi je, unajibu hali halisi ya thamani ya fedha kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna aina ya pili ya ukaguzi ambayo ni ukaguzi maalum (special audit). Ukaguzi huu maalum huombwa maalum na mtu specific au taasisi yenyewe ikiwa imegundua kuna matatizo hata kama taasisi yake ina hati inayoridhisha. Kwa hiyo, hii inakuwa na hadidu za rejea ambazo zimetolewa na mtu aliyeona kuna matatizo kwenye taasisi hiyo kwa hiyo inafanyika special audit ili kujibu hayo matatizo yaliyoonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit). Huu ni ukaguzi wa kisayansi ambao nao unakuwa na hadidu za rejea, tunakwenda zaidi ya special audit kujua matatizo haya yamesababishwa na nini kwenye taasisi husika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuendelee kuziamini ofisi zetu na hasa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa sababu wanafanya kazi zao kitaalamu zaidi.