Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:- Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria na kuyapeleka Mkoa wa Tabora katika Miji ya Igunga, Nzega, Manispaa ya Tabora, Sikonge, Isikizya na Urambo:- (a) Je, ni vijiji gani vya Mashariki vya Jimbo la Tabora Kaskazini – Uyui vitapatiwa maji kutokana na mradi huo? (b) Kwa vile ni idadi ndogo tu ya vijiji kati ya 82 vya Jimbo la Tabora Kaskazini ndiyo vitapatiwa maji na mradi huo: Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipata maji vijiji vyote katika Jimbo la Tabora Kaskazini?

Supplementary Question 1

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza, naomba nitoe kwa dhati kabisa shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa miradi mingi aliyoweka katika Jimbo langu. Naomba niitaje hapa kwa niaba ya Bunge ili lielewe miradi gani ipo Jimboni kwangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria ambao ni sehemu ya shilingi bilioni 600; Kituo cha Afya cha Upuge, shilingi milioni 850; Hospitali ya ngazi ya Wilaya Isikizye shilingi bilioni mbili; Kituo cha VETA kinachojengwa Isikizye, sasa ni shilingi bilioni tano; Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi mabilioni na umeme wa REA wa vijiji 18 mabilioni ya shilingi. Naomba salamu hizi na pongezi zimfikie Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Je Serikali ina mpango gani kupelekea maji vile vijiji 42 vilivyobakia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wataalam wa maji ili kuchunguza vyanzo vya maji katika vijiji vya Kata za Ufuluma, Shitage, Nsimbo, Bukumbi, Makazi na Igulungu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri aliyekuja kufuatilia mradi huko kwetu, nasi tumemwekea binti aende akaoe. Karibu sana Mheshimiwa Aweso. (Kicheko)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, lakini nashukuru kwa zawadi aliyonipa. Nataka nimhakikishie mimi beberu, siyo jogoo la pasaka bwana, nipo tayari. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kama Serikali ambacho nataka kusema ni kwamba tumejipanga vizuri katika kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la maji katika Mkoa wa Tabora. Tuna mradi mkubwa zaidi ya shilingi bilioni 600. Pamoja na hayo, kutokana na mapenzi makubwa na mahaba ya Mkoa wa Tabora, tumeshapeleka shilingi 8,345,000,000/= katika kuhakikisha tunaendelea kutatua tatizo la maji na fedha hizi tutatekeleza kwa kutumia wataalam wetu wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kupeleka wataalam kufanya usanifu kwa vijiji ambavyo havijapata maji ili viendelee kupata huduma hii muhimu sana ya maji. Ahsante sana. (Makofi)