Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Leonard Haule
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itafuta umiliki wa mashamba pori ya muda mrefu ya Mauzi Estate, Miyombo Estate, Sumagro Estate Kisanga Estate (Lyori Estate) yaliyopo kwenye kata za Tindiga, Masanze, Kilangali na Kisanga na kuyagawa kwa wananchi wanyonge ili waweze kupata maeneo hayo wanayoyahitaji sana ili kufanya shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nisema kwa masikitiko makubwa sana Wilaya ya Kilosa ni moja kati ya Wilaya zinazoongoza kwa migogoro mikubwa sana ya mashamba na migogoro mikubwa sana kati ya wakulima na wafugaji kutokana na upungufu wa ardhi.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika Kata ya Tindiga kumekuwa na mgogoro mkubwa sana kati ya Kijiji cha Tindiga na NARCO ambao wamemega eneo la Tindiga na kuwapa wafugaji lakini kulikuwa na kesi tangu mwaka 2013 mpaka 2019 wananchi wa Kijiji cha Tindiga wameshinda lakini mpaka leo wanazuiwa kulima na ndiyo tunaowategemea kwa kilimo cha mpunga.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumetokea maafa makubwa sana akina mama wamebakwa na wakulima wamepigwa vibaya sana na kulazwa hospitali kwa sababu ya kuzuiwa kwenda kulima. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wa Tindiga ambao wameshinda kwenye Mahakama ya Ardhi ili warudishiwe ardhi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilitoa mashamba kwa wawekezaji katika Kata ya Kisanga, Kata ya Masanze pia Sumargo pale Kilangale. Hata hivyo, hawa wawekezaji wameshindwa kutumia mashamba haya ipasavyo na kupoteza ajira kwa wananchi na Serikali inakosa mapato mengi kwa sababu yale mashamba ni pori na hayatumiki. Imeleta migogoro mikubwa sana pale Masanze mtu alipgwa risasi akafariki, pale Kisanga mwananchi alipigwa risasi akafariki, pale Sumargo, Kilangali migogoro ni mikubwa watu wanaumia sana. Wizara ya Ardhi mnatoa kauli gani kwa Wilaya ya Kilosa ili wananchi waweze kurudishiwa mamshamba haya na kuyaendeleza kwa kilimo ili kusaidia Taifa letu la Tanzania? (Makofi)
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Haule, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza juu ya wananchi wa Tindiga, wiki iliyopita niliongea na wananchi hawa waliletwa na Mheshimiwa Mbunge, nimekubaliana naye aniletee mimi barua na vielelezo hivyo vya kesi, maana mimi siwezi kujua yanayoendelea na kesi na mimi nina wanasheria, walete hizo hukumu za kesi kama kweli wameshinda mimi nitawasaidia ili wapate haki yao. Tulishaelewana na nafikiri alitaka hapa sasa wananchi wengi zaidi wasikie. Serikali lazima itekeleze uamuzi wa Mahakama na Serikali haiwezi kumwonea mtu. Kwa hiyo, fanyeni yale niliyowaelekeza leteni barua na vielelezo vile ili tuweze kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, la pili, swali hili ni swali la msingi ambalo umeuliza. Katika mashamba ambayo yameshafutwa Mkoa wa Morogoro 15 yanatoka Wilaya ya Kilosa. Niliunda timu ya wizara, ilipokwenda kukagua mashamba yote ya Kilosa tukagundua kuna mashamba mengine mapya 23 ambayo yana sifa ya kufutwa pamoja na haya uliyoyataja.
Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu wa kufuta hauanzii Wizarani unaanzia Wilaya ya Kilosa. Tulikuwa na timu ya hovyo pale wilayani Maafisa Ardhi waliokuwa wanafanya kazi ile pale wao sio Maafisa Ardhi walikuwa wamejivisha tu Uafisa Ardhi lakini hatukuwa na Afisa Ardhi. Kwa hiyo, tumefanya utaratibu tumeleta Maafisa Ardhi, kuna Afisa Ardhi mzuri sana tumemtoa kutoka Mkoa wa Mbeya tumempeleka pale sasa ndio wanaanza kazi ya utaratibu wa awali wa kisheria wa kusababisha haya mashamba yafutwe.
Mheshimiwa Spika, lazima notice ya wale wenye mashamba itolewe na Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kilosa hamkuwa naye. Kwa hiyo, nimeelekeza huyo Afisa Ardhi aanze na mashamba haya. Hivi sasa ameshatoa notice ya siku 90 kwa wenye mashamba wajieleze kwanza hatua itapanda itafika kwangu tukiridhika na maelezo yao kwamba wanazo sifa za kufutiwa tutampalekea Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa sheria.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved