Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:- Halmashauri ya Mbeya ina upungufu mkubwa wa maji karibu kwenye Vijiji zaidi ya 153 na hasa katika Kata ya Mjele. Je, Serikali ina mpango gani wakupeleka maji kwenye Vijiji hivyo na hasa Vijiji vya Mjele, Chang‟ombe na Ipwizi?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza nianze kuipongeza Serikali na kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Mbeya.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa bajeti ya ziada ya shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya mradi wa maji uliotolewa kwa ajili ya Mji wa Mbalizi pamoja na Kata za Bonde la Songwe na Ilota. Pamoja na pongezi hizo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni lini miradi ya maji itapelekwa kwenye Vijiji vya Ilembo, Santilia, Inyala pamoja na Ikukwa ambapo kunajengwa vituo vya kisasa vya afya na pia kuna Hospitali ya Wilaya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Mradi wa Mbalizi utakamilika kuhakikisha wananchi wa Bonde la Songwe, Ilota na Mji Mdogo wa Mbalizi wanapata huduma ya maji ya uhakika? Nashukuru sana. (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayofanya katika Jimbo lake. Sisi kama viongozi wa Wizara, mimi pamoja na Waziri wangu tulishafika kule kuhakikisha Mradi wa Mbalizi wa kiasi cha shilingi bilioni 3 tunausimamia ili ukamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa hivi baadhi ya kazi zinafanywa na wataalam wetu wa ndani wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya. Ndani ya mwezi Machi, mradi ule utakamilika na wananchi wa Mbalizi watapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi katika Vijiji vya Santilia pamoja na Ilembo na Ikukwa tulipata fedha zaidi ya shilingi bilioni 25 za Lipa kwa Matokeo na wafadhili wa DFID na Kijiji hiki cha Santilia kipo. Sasa tupo katika hatua ya manunuzi kuhakikisha tunaukarabati mradi ule na wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu ya maji.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kumhakikishia kwa Vijiji vya Ilembo na Ikupwa katika awamu hii inayokuja ya fedha za Lipa kwa Matokeo tutaviweka katika kuhakikisha nao wanapata huduma hii muhimu sana ya maji. Ahsante sana.