Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Joseph Monko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:- Katika mitihani ya Taifa ya Vitendo kwa Kidato cha Nne utaratibu mpya ulioanzishwa mwaka 2017 ambao ni bora zaidi ulibadilika na kupelekewa checklist ambayo sasa inahitaji vifaa vingi zaidi na practical nyingi ikilinganishwa na hapo awali ambapo ‘instructions’ ya mwezi mmoja ilitolewa kabla:- (a) Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha za vifaa vya Maabara kufidia ongezeko la gharama za vifaa hivyo ambavyo vinazidi fedha iliyoingizwa kwa mwaka? (b) Shule nyingi sasa zimelundika madeni ya Maabara na hushindwa kulipa: Je, Serikali iko tayari kulipa madeni haya yaliyosababishwa na utaratibu huu mpya?
Supplementary Question 1
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuulizwa maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ukamilishaji wa maabara katika sekondari ni sehemu muhimu sana ya utoaji wa mafunzo kwa vitendo; na kwa kuwa Halmashauri nyingi nchini zimeshindwa kukamilisha maabara kwenye sekondari zetu: Je, Serikali ina mpango gani wa kukamlisha maabara hizo ili vijana wetu waweze kufanya mafunzo kwa vitendo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa katika swali la msingi, Mheshimiwa Waziri amesema, Mkoa wa Singida utapata vifaa kwenye shule 59: Je, ni shule zipi katika Jimbo la Singida Kaskazini zitakazopatiwa vifaa vivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge sawa na Waheshimiwa Wabunge wengine kwa kuendelea kufuatilia na kusimamia elimu ili vijana wetu wapate maisha mazuri huko baadaye kwa kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza, kama Serikali ina mpango wa kupeleka fedha kukamilisha maabara katika mashule yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ina mpango mkakati, fedha hizi ambazo tunapata za kutoka Halmashauri zetu, fedha za kutoka Serikali kuu, fedha za kutoka katika wafadhili mbalimbali, pamoja na kazi nyingine za kujenga madarasa, lakini pia tunatumia kukamilisha maabara hizi. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba, mwaka huu wa fedha tumetenga fedha nyingi pia. Wakati ukifika tutaanza kutekeleza mradi huu na kila Halmashauri na kwenye mashule tutapeleka fedha ili kukamlisha maabara, likiwemo la Jimbo la Mheshimiwa Monko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anauliza, shule ambazo zina mpango wa kupelekewa vifaa vya maabara. Katika Jimbo la Mheshimiwa Monko, Singida Vijijini, shule kwa mfano ya Sekondari Madenga, Shule ya Sekondari Nyeri, Shule ya Sekondari Ugandi, Shule ya Sekondari Dokta Salmini, Shule ya Sekondari Mandewa, Shule ya Sekondari Mtururuni, Shule ya Sekondari Mganga na Shule ya Sekondari Utemini. Shule hizi pamoja na nyingine zitapata vifaa vya maabara mwaka huu ambao tunaendelea nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Name
Oliver Daniel Semuguruka
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:- Katika mitihani ya Taifa ya Vitendo kwa Kidato cha Nne utaratibu mpya ulioanzishwa mwaka 2017 ambao ni bora zaidi ulibadilika na kupelekewa checklist ambayo sasa inahitaji vifaa vingi zaidi na practical nyingi ikilinganishwa na hapo awali ambapo ‘instructions’ ya mwezi mmoja ilitolewa kabla:- (a) Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha za vifaa vya Maabara kufidia ongezeko la gharama za vifaa hivyo ambavyo vinazidi fedha iliyoingizwa kwa mwaka? (b) Shule nyingi sasa zimelundika madeni ya Maabara na hushindwa kulipa: Je, Serikali iko tayari kulipa madeni haya yaliyosababishwa na utaratibu huu mpya?
Supplementary Question 2
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo na nyongeza. Kumekuwa na taarifa za kupotosha juu ya michango mashuleni hasa baada ya elimu bure:-
Je, ni nini maelezo ya Serikali kuhusu suala hili? (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, kwa kufuatilia suala la elimu na hasa hususan watoto wa kike, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi hasa wanawake wanafanya kusemea wanawake wenzao ili na wenyewe baadaye wawe wana mambo mazuri huko mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, nimefanya ziara mbalimbali kwenye Halmashauri nyingi tangu nimepata nafasi hii ya kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, lakini ni kweli kwamba kumekuwa na watu wanapotosha. Wengine wanapotosha kwa kutojua, lakini wengine wanapotosha kwa makusudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango mashuleni haijazuiliwa. Kilichofanyika, umewekwa utaratibu. Huko nyuma ilikuwa kuna michango mingi mashuleni na inaratibiwa na Walimu. Ilikuwa wanaunda timu yao, kiasi kwamba badala ya kuwa na jukumu kubwa la kufundisha na kusimamia elimu, ikawa wengi wanagombana na wanafunzi na wazazi ili michango iende pale shuleni. Baada ya Serikali kuliona hilo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa waraka wa mwaka 2015 ambao umeanza kutumika mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba waraka huu Waheshimiwa Wabunge waupate kwa kuwa unapatikana, wausome. Waraka huu unaelekeza namna michango inavyoweza kuratibiwa katika shule zetu na umetaja kila mtu na kazi yake. Kama ni ngazi ya kijiji, kama ni ngazi ya mtaa, kama ni Kamati ya Shule au Bodi ya Shule, kama ni Waheshimiwa Madiwani kwa maana ya WDC, kama ni Waheshimiwa Wabunge na Halmashauri ngazi ya mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango kama ni kwenye shule kwa mfano, kuna upungufu wa Walimu na tunajua kwamba tuna upungufu wa Walimu hasa masomo ya sayansi kwa sekondari na msingi. Wazazi wenyewe kwa utashi, wakaamua kuona kuna ulazima wa kupata mwalimu hata wa kujitolea kwa michango kidogo. Kikao cha wazazi kinaitishwa, kinasimamiwa ama na Mkurugenzi au na Mkuu wa Wilaya ili wazazi ambao hawana uzwezo wasilazimishwe. Pia baada ya kukubaliana, watoto ambao wazazi wao au walezi hawatakuwa na uwezo kuchanga, ni marufuku kuwazuia kutoenda shuleni kusoma ili wakatafute michango hiyo, wachange wale wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo utaratibu uliotolewa na walaka unaeleza, Waheshimiwa Wabunge wausome, wale ambao wanapotosha wananchi kwamba michango hairuhusiwi. Haiwezekani kuna watu wanakaa kwenye kijiji fulani, kwenye kata fulani, wana uwezo kwa mfano kuchimba kisima cha maji katika shule, hawawezi kuzuiliwa. Cha muhimu, ni lazima tujue nani anachanga na fedha inasimamiwa na nani? Walimu wabaki na jukumu la kufundisha na watu wengine tusaidie miundombinu hii. Kazi ya kuifanya elimu iwe bora Tanzania, ni kazi ya Serikali, kazi ya Wabunge na kazi ya wadau mbalimbali wote ambao wanapenda maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)