Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa Hatimiliki kwa Vijiji vilivyopimwa na kusajiliwa ambavyo bado havijapewa Hati?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa moja ya chimbuko la migogoro ya mipaka katika vijiji vyetu ni kutokuwepo kwa alama imara na zinazoonekana kati ya mipaka iliyobainishwa kati ya Kijiji na Kijiji, Kata na Kata, Tarafa na Tarafa mpaka hata Wilaya na Wilaya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakiki kuweka alama madhubuti na kutengeneza ramani zitakazowezesha jamii zenye migogoro ya mipaka kujitambua na kuheshimu mipaka hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa katika Jimbo langu la Longido tuna migogoro michache sugu ambayo imekuwepo tangu Wilaya ya Longido ianzishwe zaidi ya miaka 20 iliyopita, ambayo ni mpaka wa Kijiji cha Wosiwosi Kata ya Gilailumbwa na Kata ya Matali Kijiji cha Matali ‘B’ na mpaka huo huo ulio Kaskazini mwa ziwa Natron una mgogoro na eneo la Ngorongoro ambapo Kitongoji cha Ilbilin kimevamiwa na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na kuanzisha vituo vyao vya kudumu pamoja na eneo la Engaruka na sehemu ya Kitumbeine vijiji vya Sokon na Nadare.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili kuja katika Jimbo langu atusaidie kutatua migogoro hiyo sugu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.(Makofi)
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishamkubalia hata kwenye Kamati, huyu ni Mjumbe wa Kamati yangu na ni Mjumbe makini sana na ni mchambuzi mzuri sana wa masuala ya ardhi. Tulishakubaliana kwamba tutatafuta nafasi ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwaka huu tufike huko kwenye site ili tuzungumze pamoja na viongozi wenzangu wa Wilaya namna bora ya kukabiliana na hiyo migogoro. Kwa hiyo, Dkt. Kiruswa nitakuja huko kushirikiana ili kuhakikisha hiyo mipaka inatatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili juu ya alama zinavyoonekana, katika uwekaji wa mipaka ya vijiji na vijiji huwa kunakuwepo na alama. Labda nimjulishe kwamba Seriakli kupitia Wizara ya TAMISEMI ndiyo huwa inatangaza, Mheshimiwa Rais ndiyo huwa anatangaza uanzishwaji wa mamlaka wa WIlaya, Mikoa na Vijiji vinatangazwa kwenye Ofisi ya Rais, kwa hiyo kuna mipaka ambayo huwa inawekwa pamoja na coordinates zinawekwa kwenye GN, zinatangazwa kwenye GN kwamba Wilaya fulani na Wilaya fulani itapakana na alama za msingi huwa zinawekwa kwenye GN na kwenye vijiji tunapopima huwa kunakuwa na alama zinatangazwa na zinawekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kama kuna matatizo ya kutokukubaliana kati ya kijiji na kijiji huko kwenye Wilaya yake nitakwenda lakini alama hizi za vijiji huwa zinawekwa na wanakijiji wanakubaliana ni alama gani na kila tunapopima huwa tunaweka mawe ambayo yanakuwa na alama na namba ambazo zile coordinates ndiyo zinaingizwa kwenye GN inayotangazwa maeneo ya mipaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mawe yale huwa tunaweka, sema labda pengine mawe yale yanafukiwa chini labda yeye angependa yawekwe juu, kwa hiyo kama kuna maeneo ambayo yana mwingiliano mkubwa, tuko tayari kuweka alama zinazoonekana badala ya zile ambazo tunaweka chini. Lakini sehemu kubwa huwa tunaweka alama na zile alama zina namba ambazo huwa zinatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved