Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Halmashauri ya Manispaa ya Moshi haina Hospitali ya Wilaya na kuifanya Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi izidiwe na idadi ya wagonjwa:- Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kujenga Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Moshi?

Supplementary Question 1

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa mpango huu wa Serikali wa kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Moshi Arusha, lakini nilikuwa naomba Serikali, kwa sababu tunaelekea kwenye bajeti; na kwa sababu mchakato huo wa kupandisha hadhi kituo cha afya ni wa muda mrefu kidogo; ni lini sasa mpango huo utakamilika ili bajeti ya kukarabati hiyo miundombinu kwa ajili ya kuwa Hospitali ya Wilaya iweze kuingizwa katika bajeti ya mwaka huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, bado Moshi tuna tatizo kubwa la Vituo vya Afya. Tuna Vituo vya Afya viwili tu ambavyo vimeshazidiwa tayari; Kituo cha Afya cha Pasua na Kituo cha Afya cha Majengo. Nami naishukuru Serikali kwa kutupa shilingi milioni 400. Tumeleta maombi ya muda mrefu Serikalini ya kutusaidia kupandisha hadhi Vituo vya Afya vya Shirimatunda, Longuo B na Msaranga.

Je, ni lini Serikali itakubaliana na ombi letu? Kama hilo ombi haliwezekani, ni lini sasa itatujengea kituo kingine kimoja cha afya katika Manispaa ya Moshi?

Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii nimwombe Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu yeye ni sehemu ya Madiwani na katika mchakato wa kuhakikisha kwamba tunabadilisha hicho Kituo cha Afya ni pamoja na wao kutekeleza wajibu wao. Atusaidie kusukuma Halmashauri yake kufanya taratibu zile ambazo anatakiwa kuzifanya halafu sisi tuweze kumalizia.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameongelea juu ya suala zima la kubadilisha Zahanati kuwa Vituo vya Afya, ametaja nyingi lakini pia akawa na ombi kuwa, kama hilo haliwezekani ni vizuri basi tukafikiria suala la kujenga Kituo cha Afya kingine. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba Zahanati zinaendelea kuwepo kama Zahanati kwa sababu Zahanati na Vituo vya Afya ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, siyo azma ya Serikali kubadilisha Zahanati kuwa Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, Zahanati zile zilizopo ziendelee kuwa Zahanati ila ombi la kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Afya kipya, hilo tunaliweka katika matazamio ya siku za usoni.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Halmashauri ya Manispaa ya Moshi haina Hospitali ya Wilaya na kuifanya Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi izidiwe na idadi ya wagonjwa:- Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kujenga Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Moshi?

Supplementary Question 2

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa swali la msingi ni kuhusu Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mawenzi kusema ukweli imezidiwa sana; namna gani Serikali inaona umuhimu wa kuimarisha hivi Vituo vya Afya kama alivyouliza Mheshimiwa Japhary Michael na hasa Kituo cha Afya cha Kirua Vunjo Magharibi ambapo tangu kimefungulia wa Mheshimiwa Abdu Jumbe mwaka 1973 miundombinu yake ni chakavu sana na wala hakina hadhi ya kuwa Zahanati ili kiimarike kiweze kutoa huduma kama vituo vingine vya afya?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba vile Vituo vya Afya vilivyojengwa miaka ya zamani vilikidhi haja kwa kipindi hicho. Ukilinganisha na Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa sasa, vile vingine vyote vya zamani vinaoneka vimechakaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwanza tulianza kukarabati vile ambavyo vipo lakini pia tukaanza kujenga upya. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya vinakuwa na hadhi ya Vituo vya Afya ili viweze kutoa upasuaji wa dharura kwa mama mjamzito.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia, kama ambavyo Serikali imekuwa ikipitia kuona takwimu Vituo vya Afya vipi vichakavu na cha kwake tutakipitia.