Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:- Kazi zote za Utawala na fedha katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya zinasimamiwa na Mganga Mfawidhi wa Wilaya wa eneo husika:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa elimu ya Utawala na Usimamizi wa Fedha Madaktari hao ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi?

Supplementary Question 1

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa ruhusa yako naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais, Jemedari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa juhudi zake na msimamo wake wa kuhakikisha Watanzania tunapata huduma za afya. Ukiangalia kwenye Mkoa wetu wa Pwani, Vituo vingi vya Afya, Zahanati na Hospitali za Mkoa zimepata vifaa tiba na wataalam mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza: Kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameonyesha njia ya kutaka Watanzania wapate huduma bora na sahihi kwa wananchi wake: Je, hawaoni kwamba kwa kuwafanya Waganga Wafawidhi na wa Vituo vya Afya au Zahanati kusimamia masuala ya Uhasibu ni kuipelekea kada hiyo kuacha kazi zake za kutibu na kuhangaika maeneo mbalimbali kwenda kununua dawa, kwenda kufuata vifaa tiba na kuacha kutibu wagonjwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa Serikali imeonyesha nia ya kuomba kibali kwa ajili ya Wahasibu na mpaka leo hii hicho kibali hakijapatikana; kwa nini msichukue wataalam wa uhasibu ambao wamemaliza masomo yao, wako maeneo mbalimbali Tanzania na wakafanya kazi hizo kwa kujitolea?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi ambazo Mheshimiwa Mbunge ametoa. Naye amekuwa ni miongoni mwa champions ambao wamekuwa wakipigiania suala zima la afya, naye anastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika swali lake anaongelea suala zima la kwamba Waganga wanaacha kazi zao za kitaaluma na wanaanza kufanya kazi ya fedha; katika majibu yangu ya msingi nimemwambia kwamba tumeajiri watumishi wa Kada ya Uhasibu 335.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kwa muda mfupi ambao tumewapa hiyo taaluma ni ili wawe na uelewa wa jumla, lakini Uhasibu ni professional ambayo haiwezi ikasomewa ndani ya muda mfupi huo. Kwa hiyo, hawaachi kazi yao ambayo wameajiriwa nayo kuanza kufanya kazi ya usimamizi wa fedha, lakini ni vizuri at least wakajua nini ambacho kinaendelea kulikoni kutojua kabisa. Huo ndiyo msingi wa elimu ambayo imetolewa kwa hao Waganga.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anasema kwamba ni vizuri, pamoja na kwamba tumeomba kibali cha kuajiri, sasa kuna wengine ambao wamemaliza taaluma ya Uhasibu wako Mtaani tuwaajiri wajitolee. Sina uhakika sana na kwa sera yetu haijatokea mahali hata pamoja ambapo tunataka mtu afanye kazi asilipwe.

Mheshimiwa Spika, tuendelee kuwa na subira, Serikali ni sikivu na jana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya utawala alisema tunaenda kuajiri watumishi mbalimbali 45,000. Ni imani yangu kubwa katika hao watakaoajiriwa ni pamoja na Wahasibu wakaokwenda kufanya kazi hizo.