Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Willy Qulwi Qambalo

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Karatu

Primary Question

MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:- Mabaraza ya Ardhi ya Kata ni chombo muhimu sana katika kutatua migogoro ya ardhi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni uwezeshaji (chakula na nauli) na wajumbe wa mabaraza hayo ili wafanye kazi zao kwa weledi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wajumbe wanawezeshwa ili waweze kutoa haki?

Supplementary Question 1

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na maelekezo yaliyotolewa kwa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili kuyawezesha Mabaraza haya, lakini ni ukweli usiopingika kwamba Halmashauri nyingi bado hazijaona umuhimu wa kutenga fedha ili Mabaraza haya yafanye kazi zao kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza; kwa kuwa suala kutoa maamuzi kwenye masuala ya ardhi ni suala muhimu sana: Kwa nini Serikali isichukue sasa jukumu hili kama ambavyo imechukua jukumu la kuyawezesha yale Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ili haki iweze kutendeka vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wajumbe wa Mabaraza haya wanapoteuliwa, wanapewa semina ya masaa kadhaa, baadaye wanaapishwa, lakini semina ya masaa kadhaa kwa mtazamo wangu haitoshi kwa watu wanaofanya kazi muhimu ya kutoa maamuzi kama haya: Kwa nini Serikali isije na mpango mahsusi wa mafunzo kwa Wajumbe hawa ili waweze kufanya kazi yao kwa weledi? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli kwamba mabaraza haya yanasimamiwa na Halmashauri na Mheshimiwa Mbunge anasema Serikali ichukue jukumu hili la kusimamia Mabaraza ya Kata. Katika mgawanyo wa kazi kwa maana ya Ugatuzi wa Madaraka (D by D) tumegawana kwamba Halmashauri itasimamia Mabaraza ya Kata ya Ardhi halafu na Serikali Kuu itaanzia ngazi ya Wilaya kwenda kule juu na Mheshimiwa Mbunge ni Diwani katika Halmashauri yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, Mabaraza haya hata baada ya kuwa yameteuliwa, usimamizi wake na uangalizi unasimamiwa na Halmashauri chini ya ulezi wa Mwanasheria wa Halmashauri zetu. Kwa hiyo kama kuna upungufu katika eneo hili ni muhimu kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema tuchukue hatua na kuelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe maelekezo hapa kwa Wakurugenzi wote na Waheshimiwa Wabunge mtusaidie. Kwenye Bajeti ambayo inatengwa pale, mpaka wameelekezwa vikao vingapi wakae katika maeneo hayo ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Kwenye Bajeti ambayo inaendelea sasa tupitie: Je, kipengele hiki kimewekwa katika Bajeti yetu? Kama kuna tatizo, Bajeti ikifika hapa tuwasiliane ili tuweze kufanya marekebisho hayo. Wakurugenzi wana wajibu huo wa kusimamia, kutenga fedha na kuwezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba mafunzo yanatolewa kwa muda mfupi sana, lakini suala la mafunzo ni jambo endelevu. Kama kuna upungufu katika eneo lile Mwanasheria na Viongozi wa Halmashauri; na kama wanashindwa wataomba usaidizi katika ngazi ya Taifa, wanaweza kufanya mafunzo kadri inavyohitajika kutoka muda hadi muda mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo maelekezo ya Serikali, naomba wazingatie. Kama kuna upungufu tuwasiliane tuweze kuchukua hatua kwa maana ya case by case. Ahsante.

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:- Mabaraza ya Ardhi ya Kata ni chombo muhimu sana katika kutatua migogoro ya ardhi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni uwezeshaji (chakula na nauli) na wajumbe wa mabaraza hayo ili wafanye kazi zao kwa weledi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wajumbe wanawezeshwa ili waweze kutoa haki?

Supplementary Question 2

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa bahati nzuri nimewahi kwenda mara kadhaa kwenye Mabaraza ya Kata. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Mwanasheria wa Halmashauri anasimamia Mabaraza hayo, lakini kiukweli kabisa hakuna usimamizi wa kisheria unaopatikana pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu: Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu mahsusi ili kusudi Mwanasheria apatikane wa kueleza na kuhakikisha wananchi wanatendewa haki kwa sababu unakuta Baraza la Kata linahukumu kesi ya shilingi milioni 10 wakati wao mwisho wao ni shilingi milioni tatu. Ni kwa sababu ya kukosa Mwanasheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, Serikali imejipangaje kuhusu hilo? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Siyo kweli kwamba Wanasheria hawasimamii haya Mabaraza ya Kata. Kama nilivyosema, kwenye majibu yangu yaliyotangulia hapa, kama kuna malalamiko kwenye eneo specific, Mheshimiwa Mbunge ni vizuri akataja ili tuweze kuchukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mfano. Kule Kivule tulikuwa na shida kwenye Baraza la Kata, tulimwita Mwanasheria wa Halmashauri ile ya Manispaa ya Ilala akaja akasikiliza malalamiko yaliyokuwepo, gharama kubwa ya uendeshaji wa kesi, uonevu na kuvuka kiwango ambacho kimewekwa kwa mujibu wa sheria, tulivunja Baraza tukaweka viongozi wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna malalamiko katika eneo mahsusi tupewe taarifa. Vilevile tujue kwamba Wanasheria wako kwa mujibu wa Sheria hii ili haya Mabaraza ya Kata na yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1985 na imeendelea kufanyiwa marekebisho kadri muda unavyoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama kuna malalamiko, lazima tuchukue hatua. Hata hivyo, Mwanasheria wa Halmashauri ana uwezo, kwa sababu hazungumzi mtu mmoja, Idara ya Sheria kwenye Halmashauri ina wajibu huo. Ila kama kuna Mwanasheria kwenye Halmashauri yoyote hapa Tanzania, ameshindwa kufanya wajibu wake na haendi kila siku, Mbunge umepeleka malalamiko, wananchi wamelalamika, wamehukumu kesi kinyume na utaratibu, tupe taarifa tuweze kuchukua hatua kwa Mwanasheria huyo wakati wowote kuanzia sasa. Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Kwanza namshukuru Naibu Waziri, TAMISEMI kwa kujibu vizuri. Pia pamoja na hiyo aliyosema Naibu Waziri, changamoto hii kama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia tumeiona kwa sababu watu wale mashauri yao mengi yanahusiana na ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Wizara yetu kwa kusaidiana na Msajili wa Mabaraza, akishirikiana na Wanasheria katika Halmashauri, tumeweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa zile Kamati zote za Mabaraza ya Ardhi ya Kata pamoja na Vijiji ili kuweza kuwapa elimu na ukomo wa namna wao wanavyotakiwa kusimamia. Kwa sababu wanapokwama, mashauri mengi yanaenda kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeona kwamba tujenge msingi kule chini ili watu waweze kufanya kazi zao vizuri kwa weledi ili kupunguza malalamiko ambayo Waheshimiwa Wabunge wanayasema.

Name

Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:- Mabaraza ya Ardhi ya Kata ni chombo muhimu sana katika kutatua migogoro ya ardhi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni uwezeshaji (chakula na nauli) na wajumbe wa mabaraza hayo ili wafanye kazi zao kwa weledi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wajumbe wanawezeshwa ili waweze kutoa haki?

Supplementary Question 3

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi linalohusu Baraza la Kata, pia Mkoa wetu wa Songwe hauna Baraza la Ardhi la Wilaya. Nimekuwa nalalamika sana kwenye Bunge hili na Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwamba jambo hili watalishughulikia haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wananchi wangu wa Songwe wanakwenda Mbeya kusikiliza kesi zao na inasababisha gharama kubwa sana za kwenda kufika kule kusikiliza kesi na kurudi.

Je, ni lini Baraza la Kata litaanzishwa katika Mkoa wetu wa Songwe?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa mujibu wa Sheria, tunatakiwa kuwa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kila Wilaya. Mpaka sasa Mabaraza yaliyoanzishwa kisheria yameshafikia 100, lakini yanayofanya kazi yako 54.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema kwamba tuko tayari kuanzisha Baraza katika Wilaya yoyote ili mradi pawepo na miundombinu ambayo itawezesha kuanzishwa kwa Baraza hilo. Kwa sababu kama Wizara, hatujengi majengo kwa ajili ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Kwa hiyo, kama wakiwa tayari; na nilipokuwa kule mwezi uliopita, waliitoa hoja hiyo, nikasema tunachohitaji ni kuonyeshwa eneo ambalo litatosheleza kuweza kuwa na Ofisi ya Baraza la Ardhi na Nyumba ya Wilaya. (Makofi)