Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Edwin Amandus Ngonyani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:- Wananchi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori waliopo Namtumbo miaka 14 iliyopita walikubaliana kuacha ardhi yao kwa shughuli za hifadhi na kwamba ardhi hiyo isitumike kwa makazi wala kilimo cha mazao ya kudumu isipokuwa mpunga pekee. Wananchi washiriki kutunza njia za asili za wanyama hususan tembo na walikubaliana kwamba mipaka ya ardhi husika ingepitiwa upya baada ya kupita miaka 10 kuanzia mwaka 1996 walipoingia makubaliano:- (a) Je, kwa nini Serikali imekiuka makubaliano hayo na kuwakaribisha wafugaji kwenye maeneo ya wananchi yaliyokuwa yakitumika kwa kilimo cha mpunga? (b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wakulima ambao mashamba yao ya mpunga yameathiriwa na ng’ombe wanaochunga katika mashamba hayo?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nitoe shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa makubwa aliyoyafanya katika Wilaya ya Namtumbo. Alipofika tarehe 5 Aprili, 2019 katika Kijiji cha Nchomoro katika mambo ambayo wananchi walimlalamikia ni pamoja na kutaka maeneo ya kulima mpunga katika maeneo ambayo wamezoea kuyalima. Maeneo hayo ni Luvele, Bomalili, Nahimba, Makangaga na Mpigamiti katika Kijiji cha Nchomoro na Nangunguve, Namayani na Mkuti katika Vijiji vya Mteramwai na Songambele pamoja na eneo la Nandonga la Kijiji cha Likuyu Sekamaganga. Jibu ambalo Mheshimiwa Rais alilitoa linafanana kabisa na kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, tatizo langu tu katika utekelezaji, Halmashauri pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya bado hawajapata fedha za kupitia upya hayo maeneo ili kupata maeneo ya kilimo, ufugaji pamoja na hifadhi na hivyo kuondoa mgogoro huo moja kwa moja lakini fedha za kufanya doria kila wakati zinapatikana. Sijui suala hili la fedha kama Wizara inaweza kutusaidia zipatikane ili tatizo hili liondoke moja kwa moja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mimi kama Mbunge wao katika maeneo hayo kila napopita changamoto hii ya kukosa ardhi ya kilimo hasa kilimo cha mpunga katika maeneo yote yanayozunguka hifadhi za Mbalang’andu, Kimbanda na Kisungule ndiyo kubwa. Dawa pekee ni kupitia upya mipaka ya maeneo hayo na kupata maeneo rasmi ya kilimo, uhifadhi na mifugo. Je, ni lini Serikali itatusaidia kuondoa hili tatizo moja kwa moja kwa kufanya hayo mapitio haraka inavyowezekana kama makubaliano yalivyokuwepo toka awali? (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwasemea na kuwatetea watu wake ili kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima katika Jimbo lake na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la msingi anataka kujua kwa nini ahadi ya Mheshimiwa Rais haijatekelezwa lakini pia kazi ya kupitia na kutenga maeneo haijafanyika kwa maana ya Halmashauri na Mkuu wa Wilaya labda kama kuna upungufu wa fedha. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mambo ambayo hatuwezi kufanya mchezo nayo ni pamoja na kuchezea ahadi za Mheshimiwa Rais kama amepita mahali na kuahidi. Kwa hiyo, naomba nimuelekeze Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo na Mkurugenzi wakae pamoja wajadiliane, watuambie changamoto iliyopo ili tuweze kusaidiana kwa pamoja na Wizara kuondoa changamoto hii lakini pamoja na kuondoa kero kwa wananchi wale na magomvi yasiyokuwa na lazima lakini kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais katika eneo hilo la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge anauliza namna ambavyo tuliweza kusaidia kupima maeneo haya kuondoa changamoto mbalimbali katika mazingira ambayo ameyazungumza. Mheshimiwa Mbunge tumeshazungumza juzi na jana na Mheshimiwa Waziri ameshalipokea hili, tumetoa maelekezo maeneo yote ambayo kuna migogoro hii ya ardhi kama kuna changamoto ya fedha, mambo ya mipaka na vitu mbalimbali viangaliwe. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais amechukua hatua hata maeneo ya hifadhi zile za Taifa (National Parks) ametoa maelekezo Mawaziri wamepita kuchukua changamoto mbalimbali. Mheshimiwa Rais angependa wananchi wakulima na wafugaji wapate maeneo yao, mipaka itambuliwe na waishi kwa amani bila magomvi ili waweze kujiletea maendeleo. Mheshimiwa Mbunge naomba utupe fursa tuifanyie kazi, viongozi wa eneo hili watoe taarifa, tushirikiane pamoja na tuondoe changamoto katika maeneo haya ya mipaka. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved