Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Agnes Mathew Marwa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNESS M. MARWA aliuliza:- Wananchi wengi walibomolewa nyumba zao na Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo, Wilayani Tarime na wengine hawajalipwa fidia ya maeneo yao mpaka sasa. Aidha, mgodi pia umeanza kuchimba chini ya maeneo ya watu (Underground mining):- Je, ni lini mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo utalipa fidia kwa wananchi hawa?
Supplementary Question 1
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza lenye vipengele viwili.
Mheshimiwa Spika, kwanza, kutokana na shilingi na vifaa vya ujenzi kupanda thamani kila mwaka, deni la wananchi wa Nyamongo wanaodai fidia ni miaka sasa. Je, watakapolipa hizo fedha watawalipa pamoja na riba kwa sababu sasa vifaa vya ujenzi vimepanda?
Mheshimiwa Spika, pili, kutokana na uthamini kila siku kufanyika kwa haohao wakazi wa Nyamongo lakini hawalipwi ukizingatia hali halisi kwamba na wao wana familia zao, wana watoto wanawasomesha na biashara zao na mahitaji yao ambayo yamesimama kusubiria kuondolewa katika maeneo yale. Je, Serikali ina mpango gani wa kulimaliza hili suala sasa ili wale waliobaki walipwe fedha zao?
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agness Marwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nieleze kwamba tumekuwa karibu sana Mheshimiwa Agness Marwa kushughulikia masuala ya fidia kwa wananchi wa Nyamongo. Kwa kweli, amekuwa mstari wa mbele kuwapigania kila wakati na kutualika mara kwa mara kwenda Nyamongo kwa ajili ya kukutana na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ziko fidia ambazo fedha zilishatolewa muda mrefu lakini bahati mbaya hazijalipwa kwa wananchi. Hii ni kwa sababu tu wako wananchi ambao walikataa zile fedha, kwa hiyo, zikawekwa Halmashauri. Kwa hiyo, nadhani si sahihi sana kuupa tena mzigo mgodi kwamba wao walipe na fidia ya interest kwa sababu fedha hazijachukuliwa. Wale wananchi waliokataa mwanzo walikuwa 138, wale wananchi wengine 70 wakachukua cheque zao wakabaki 64, niwaombe wakachukue cheque zao kwa sababu tayari uthamini ule ulikwishafanyika muda mrefu na fedha zao shilingi 1,900,000,000 ziko pale kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili ambalo ameuliza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba jambo hili la fidia sasa lifike mwisho. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Mgodi wa Barrick kuingia pamoja na Serikali kama mbia, tunachukua kila hatua kufuta yale makosa ambayo yalikuwa yanafanyika ACACIA. ACACIA walikuwa na utaratibu, mnaweza mkafanya uthamini leo kesho wakakataa kulipa tu kwa vigezo vingine. Nataka nimhakikishie kwamba tumeshazungumza na mbia mwenzetu Barrick anayekuja, jambo hili sasa litafika mwisho na Mthamini Mkuu ameshawasilisha vitabu vya uthamini ambavyo nimetaja wananchi zaidi ya 1,838 wamekwisha kufanyiwa uthamini. Kwa hiyo, tutalipa kwa wakati baada ya taratibu hizo kukamilika. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved