Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Augustino Manyanda Masele
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Primary Question
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:- Mikoa ya Kanda ya Ziwa imeathirika na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu mkubwa wa mazingira:- Je, ni lini Serikali itajenga vyuo vya uhifadhi wa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira na elimu ya utalii hasa baada ya kuanzishwa kwa hifadhi za Taifa Burigi- Chato, Kigosi, Ibanda – Rumanyika, Rubondo na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla.
Supplementary Question 1
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo :-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa ni mkubwa sana katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Mkoa wa Geita kwa maana ya kwamba hifadhi za misitu zinatoweka kwa haraka sana kwa mfano Hifadhi ya Msitu ya Geita, Rwamgasa, Rwande na Miyenze inatoweka kwa haraka. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuweza kudhibiti hali ya uharibifu wa mazingira na utowekaji wa misitu unaofanyika kwa sasa katika mkoa huo wa Geita.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe haina maafisa wanyamapori, je, Serikali ipo tayari sasa kutupatia maafisa wanyamapori ili huduma yao iweze kuonekana kwa wananchi wa Wilaya ya Mbogwe, ahsante. (Makofi)
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akiwasiliana na mimi kuhusu uharibifu wa misitu aliyoitaja; Misitu ya Rwamgasa na Rwande ambayo kwa ujumla imevamiwa sana na wachimbaji wadogowadogo na wakataji wa kuni na mkaa lakini tumeshirikiana nae kutoa maelekezo ili kuilinda. Kwa hiyo, naomba nimpongeze sana kwa juhudi hizo ambazo ameendelea kuzionesha.
Mheshimiwa Spika, uharibifu wa misitu ambao unaendelea karibu nchi nzima ni tatizo ambalo ningependa kulitolea maelekezo. Imekuwepo tabia ya Halmashauri nyingi kufikiri jukumu la kulinda misitu ni la TFS au Wizara lakini misitu hii mingi ipo kwenye maeneo ya Halmashauri na mingi ni misitu ya vijiji na Halmashauri na misitu michache inayosimamiwa na TFS inalinda vizuri. Kwa hiyo, nizielekeze tu Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashirikiana vizuri na maafisa wetu wa TFS kulinda na kudhibiti wanaoharibu misitu hii kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili la nyongeza amesema Halmashauri ya Mbogwe haina afisa wa wanyamapori. Na naomba tu nitumie nafasi hii pia kuwaambia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kwamba katika maombi yao ya watumishi tunawaelekeza Halmashauri zote ambazo zinapakana na hifadhi ambazo zimekuwa na historia ya migogoro ya wanyama na binadamu kuhakikisha kwamba wanaomba kuwa na maafisa wa wanyamapori katika halmashauri hizo kwa sababu hawa ni watu wa kwanza ku-respond na matukio ya wanyama waharibifu wanaoenda kwenye maeneo ya makazi ya watu.
Kwa hiyo, naelekeza halmashauri hiyo katika maombi yao ya watumishi ya mwaka huu waweze kuomba afisa wa wanyamapori.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved